Wednesday, May 16, 2018

CCM BAGAMOYO YAIKAMUA CHALIWASA ITOE MAJI.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdu Rashidi Zahoro akiongoza Mkutano Maalu wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo.
.....................................
Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo katika kikao chake maalum kimetaka ufafanuzi wa kina kuhusu tatizo la maji linaloikabili Halmashauri ya Chalinze.

Wakizungumza katika Mkutano huo wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilayani humo walisema kwa muda mrefu sasa Chalinze kumekuwa na tatizo la Maji bila ya kupatiwa ufumbuzi wowote licha ya kuwepo Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Chalinze, (CHALIWASA)

Aidha wajumbe hao walimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA)  kutoa ufafanuzi wa kutosha ili wajumbe hao waweze kuwaelimisha wananchi juu ya tatizo hilo la maji.

Akijibu hoja ya za wajumbe mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchomba alianza kwa kutoa historia ya mradi jambo ambalo wajumbe hawakulizika na kutaka majibu ya kwanini maji hayapatikani.

Aidha Mhandisi Mchomba alisema maji hayatoshi kusambaza eneo lote linalohudumiwa na CHALIWASA na hivyo huduma hiyo hutolewa kwa mgao jambo linalopelekea baadhi ya maeneo kukosa maji kwa siku kadhaa.

Akizungumzia uzalishaji wa maji katika mradi huo Mhandisi Mchomba alisema kwa siku wanan uwezo wa kuzalisha lita laki tatu tu ambapo katika Halmashauri ya Chalinze peke Mradi huo unahudumia vijiji 55 kati ya vijiji 58 vya Halmashauri hiyo.

Aliongeza kuwa, licha ya kuhudumia Halmashauri ya Chalinze mradi huo unahudumia wilaya tano zikiwemo Kibaha, Bagamoyo, Morogoro vijijini ambapo ukilinganisha ukubwa wa eneo la kutoa huduma na uwezo wa kuzalisha maji ni wazi kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa maji.

Kufuatia maelezo hayo wajumbe wa mkutano huo maalu wa CCM hawakuridhika na majibu hayo na kuomba taarifa kwa Mwenyekiti ambapo wajumbe walitaka kuelezwa kwa kifupi ni si kuleta historia ambayo wasingeweza kuwasilisha kwa wananchi ili wawaelewe.

Baada ya mjadala kuendelea Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdu Rashidi Zahoro amemtaka Mhandisi huyo kuwa na majibu ya uhakika ili wajumbe waridhike na kuwafahamisha wananchi.

Miongoni mwa mambo yaliyowachukiza wananchi ni pamoja ni pamoja na kuwa maji hayatoki siku zote lakini siku ya kufika kiongozi wa kitaifa maji yanatoka.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya vizimba vya CHALIWASA vikitumika kama duka badala ya sehemu ya kupatia maji.

Tatizo la maji katika Halmashauri ya chalinze limekuwa la muda mrefu ambapo mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi.

Awali akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa mwaka 2017 kwa miradi mbalimbali, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ambae ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya, Alhaj Majid Mwanga alisema Serikali ya wilaya imeweka mikakati ya upatikanaji wa maji ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu ya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Alisema wadau hao wakiongozwa na DAWASA ambao ndio wanaoshughulikia ujenzi wa miundombinu, DAWSC pamoja CHALIWASA ambazo zote ni taasisi za serikali zinazoshughulikia huduma ya maji.

Aidha, alisema pamoja na taasisi hizo za serikali, Serikali ya wilaya imeweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana ipasavyo wilayani humo.

Aliwataja wadau ambao waliweza kushirikiana na serikali ya wilaya katika kufanikisha huduma ya maji ni Pamoja na The Islamic Foundation yenye makao yake makuu mjini Morogoro ambayo iliweza kuchimba visima virefu na vifupi 50, katika kipindi cha mwaka 2017 tu, Dhi Nureyn Islamic Foundation yenye makao yake makuu mjini Iringa ilichimba visima 14 pamoja na jenereta katika maeneo ambayo hayakuwa na umeme, wengine ni taasisi ya waturuki ya REHEMA visima 40 na  Jumuiya ya watu wa Korea kusini walichimba visima 15.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kufuatia uchimbaji wa visima hivyo hali ya upatikananji wa maji Halmashauri ya Bagamoyo imefikia asilimia 66 kwa mjini na asilimia na 74 kwa vijijini huku Halmashauri ya Chalinze ikiwa ni asilimia 56 mjini  na asilimia 58 vijijini.
Moja kati ya vizimba vya maji vya CHALIWASA katika Halmashauri ya Chalinze ambacho kimegeuzwa duka baada ya huduma ya maji kukosekana kwa muda mrefu kama kilivyokutwa na mpiga picha wetu.

 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno ambae ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya akizungumza katika Mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha mwaka 2017.

Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo wakiwa katika Mkutano maalum ambao ulifanyika ukumbi wa Sekondari ya Lugoba.

Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiy, Edes Lukoa, (mwenye suti) katika mkutano maalumwa Halmashauri kuu ya CCM.


Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fatuma Latu (wa tatu kushoto) katika mkutano maalumwa Halmashauri kuu ya CCM.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchombaakitoa maelezo kuhusu CHALIWASA.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdul Rashidi Zahoro (katikati) akiongoza mkutano maalum wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya, Kulia ni Katibu wa CCM wilaya Kombo Kamote na kushoto ni Katibu mwenezi John Francis (Bolizozo). 

 Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo wakiwa katika Mkutano maalum ambao ulifanyika ukumbi wa Sekondari ya Lugoba.

No comments:

Post a Comment