Tuesday, May 8, 2018

SERIKALI KUFUTA LESENI 587 ZA MADINI.

Serikali imesema itazifuta leseni za madini 587 ambazo hazijaendelezwa ili kukomesha tabia ya ulanguzi wa leseni hizo.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni Wilayani Bagamoyo na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wamiliki wa migodi ya madini wa Halmashauri ya Chalinze na wajumbe serikali za vijiji.

Biteko alisema wapo watu ambao wamechukua leseni za madini lakini mpaka sasa hawajaziendeleza na hivyo kukwamisha juhudi za mandeleo ya vijiji husika na Taifa kwa ujumla.

Aidha alibainisha kuwa wapo ambao wamechukua leseni lakini hawana mpango wa kuanza kazi na badala yake wanasubiri mwenye kuhitaji ili wamuuzie na kuonya kuwa watazifuta.

Alisema tayari mchakato umeshaanza wa kufuta leseni za madini 587 ambazo hazijaendelezwa.

Katika hatua nyingine aliwataka wawekezaji wote walioahidi kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijiji kutekeleza haraka iwezekanavyo na kwamba amemuagiza Mkuu wa wilaya kushughulikia hilo na kwamba taarifa yake aipate baada ya siku saba tu.

Alisema wawekezaji wengi wameingia makubaliano na serikali za vijiji na kisha hawatekelezi makubaliano hayo na hatimae kuzorotesha shughuli za maendeleo.

Awali akizungumza mbele ya Naibu waziri wa Madini, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema mgongaano wa sheria ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya madini kwa serikali za vijiji ukilinganisha mamlaka iliyonayo wizara ya madini na serikali za vijiji.

Alisema wakati mchakato wa kijiji unaendelea ili kujiridhisha na muwekezaji tayari muwekezaji ameshapewa leseni na wizara au kibali kutoka kamishna wa madini wa kanda jambo ambalo linaleta mkanganyiko
 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wamiliki wa Migodi ya madini pamoa na waumbe wa serikali za vijiji katika Halmashauri ya Chalinze.

 
  Wamiliki wa Migodi ya madini pamoa na waumbe wa serikali za vijiji katika Halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani)

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alha, Maid Mwanga akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akizungumza kwenye Mkutano huo.

No comments:

Post a Comment