Friday, May 18, 2018

JAFO ATOA SIKU TANO KWA HALMASHAURI 10 KUJIELEZA KUHUSU MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI YA AFYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo akifungua kikao kazi juu ya utekelezaji wa miradi ya afya inayotekelezwa chini ya Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kilichowajumuisha Makatibu Tawala kutoka mikoa yote
nchini.
 .............................................
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Seleman Jafo ametoa siku tano
kwa wakurugenzi na waganga wakuu wa halmashauri 10 nchini kutoa
maelezo ya kina kwa nini halmashari hizo hazijafika asilimia kumi ya
matumizi ya fedha za miradi ya afya.


Jafo ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi juu ya utekelezaji
wa miradi ya afya inayotekelezwa chini ya Mamlaka za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kilichowajumuisha Makatibu Tawala kutoka mikoa yote
nchini.


Amesema halmashauri hizo zimeshindwa kutumia fedha zilizotolewa kwa
ajili ya miradi ya afya kama inavyotakiwa ambapo matumizi yake
yanaonekana kuwa chini ya kiwango, huku akizitaja halmashauri hizo kuwa
ni halmashauri ya wilaya ya Karatu, Mpimbwe, Mbulu Dc, Songwe,
Simanjiro, Mkinga, Mkuranga, Namtumbo, Nzega TC pamoja na Kilindi.


“Halmasharu hizi zina kila dalili ya kupata hati chafu, naagiza hadi kufika
siku ya Jumatano niwe nimepata majibu ya kuridhisha ni kwanini
hawajatumia fedha walizopewa kama maelezo yanavyotaka, tukiacha
kufanya kazi kwa mazoea tutapata matokeo mazuri, lakini kwa hali hii
tusitegemee matokeo mazuri kwa baadhi ya maeneo” Alisema Jafo


Kuwa upande mwingine Waziri Jafo aliwaagiza Makatibu Tawala hao
kuwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwekeana malengo na
watumishi wao kwa kuwafanya tathmini ya uwajibikaji kila mwaka ili
kuongeza ufanisi na uwajibikaji kazini kwani bado wapo baadhi ya
watumishi wanafanya kazi kwa mazoea.


Amesema kuwa iwapo mtumishi wataonekana amefanya kazi chini ya
kiwango cha alama 50 kama ni mkuu wa idara atawajibishwa kwa
kushushwa cheo, na yule ambaye ataonekana kufanya vizuri zaidi alishauri
anastahili kupewa zawadi ya mfanyakazi bora wakati wa maadhimisho ya
siku ya wafanyakazi Duniani-Mei Mosi.


Aidha Waziri Jafo amesema kwa sasa kipaumbele cha utoaji wa fedha
kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitatolewa kwa kuzingatia kipimo cha
matokeo mazuri kwa halmashauri husika, kwani kwa kufanya hivyo
itasaidia kuongeza uwajibikaji.


Wakati huo huo Waziri huyo aliagiza halmashauri zote nchini kuweka
mfumo wa matumizi ya mfuko wa afya ya jamii wa CHF iliyoboreshwa
sambamba ya kuhimiza matumizi ya ukusanyaji wa mapato wa njia ya
kimtandao ili kuepuka upotevu wa fedha za serikali.


Akizungumzia mafanikio ya mfuko huo Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii
TAMISEMI, Nkinda Shekalaghe amesema kuwa hadi sasa mfuko huo
haujafikia lengo lililowekwa na serikali la kuunganisha wananchi kwa
asilimia 30 hadi kufikia mwaka 2015, kwani kwa mwaka 2016/2017
wamefikia asilimia 24.


Alitaja baadhi ya changamoto zinazoukabili mfuko huo kuwa ni pamoja na
utayari wa wananchi kujiunga na mfuko, huduma duni za afya, kutokuwepo
kwa mfumo rasmi wa utoaji wa taarifa pamoja na kiwango kidogo cha
uchangiaji ambapo amesema tayai wameshachukua hatua mbalimba
katika kukabiliana na changamoto hizo.
 

No comments:

Post a Comment