Friday, May 18, 2018

MAJID MWANGA AFUNGA MAFUNZO YA SUMA JKT GUARD LTD KIBAHA.


Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga alipokuwa akifunga Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
 
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga, akizungumza wakati wa kufunga  Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
....................................

Taasisi za Serikali na zile za Binafsi wilayani Kibaha,  zimetakiwa kutumia walinzi waliopata mafunzo ya kitaalamu katika kukabiliana na majanga mbalimbali ili kuepuka usumbufu.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga alipokuwa akifunga Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.

Alisema vijana hao wamepata mafunzo mbalimbali ya kujihami na kupambana na uhalifu hivyo kuwatumia ni kuwa na uhakika wa ulinzi lakini pia ni kuonyesha uzalendo na imani kubwa kwa vijana hao ambao wamezalishwa na vikosi vya jeshi vyenye uzalendo.

Kaimu Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alisema kufuatia kuwatumia vijana wanaotoka JKT hali ya hifadhi za misitu katika wilaya ya za Bagamoyo na Kibaha zimeimarika kwakuwa sasa hakuna mtu aneweza kuvamia kutokana na ulinzi wa SUMA JKT GUARD LTD.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaasa vijana wahitimu wa Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMA JKT GUARD LTD.) kuwa waadilifu, waaminifu na watiifu kwa viongozi wao ili kujenga nidhamu ya Jeshi na kulinda heshima ya kiapo walichokula kwa mujibu wa sheria.

Wakati huo huo Majid alitoa rai kwa Viongozi wa SUMA JKT GUARD LTD kuangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya  walinzi wao ili kuwapa moyo wa kufanya kazi hasa ukizingatia umuhimu wa sehemu wanazolinda na familia walizonazo.

Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT, Kanali Endrew Mkinga aliwataka vijana hao wahitimu wa SUMA JKT GUARD LTD kuwa na nidhamu heshima na uadilifu ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.

Askari ni mpinga rushwa namba moja hivyo ni wakawa wazalendo katika kuhakikisha kuwa wanakataa na kupambana na rushwa ndani na nje ya kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kikosi cha 832 KJ, Meja James Michael alisema vijana hao wamejifunza masomo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi binafsi kwa askari.

Aliongeza kuwa kutokana na mafunzo hayo vijana hao wako imara kupambana na aina yoyote ya uhalifu ikiwa ni pamoa na kujilinda wenyewe.

Awali wakisoma Risala mbele ya Mgeni Rasmi wahitimu hao walisema mafunzo wayoyapata yamewajengea uwezo katika nyanja mbalimbali ambapo watayatumia kuimarisha ulinzi na kujiongezea kipato kutokana na kazi watakazopata kwa taluma hizo.

Aidha waliongeza kuwa muda wote watakuwa watiifu kwa viongozi wao na kupokea maelekezo yatakayopelekea kuwajibika katika maeneo mbalimbali watakayopangiwa.
 
 Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga, (katikati) kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT, Kanali Endrew Mkinga na kushoto Kaimu Mkuu wa kikosi cha 832 KJ, Meja James Michael
wakati wa kufunga  Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
 
wahitimu wakiwa wametulia kwa nidhamu kusikiliza hutuba za viongozi wakati kufunga mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.


No comments:

Post a Comment