Sunday, May 20, 2018

MUFTI ZUBEIR ATAKA WAISLAMU WAITAFUTE ELIMU.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakari Zuberi amesema swala la elimu katika uislamu lina histoeia kubwa kutokana na umuhimu wake hivyo waislamu hawapaswi kujiweka mbali na elimu.

Sheikh Zubeir alitoa kauli hiyo mjini Kibaha Mkowa wa Pwani, wakakti wa kuzindua mafunzo ya uislamu kwa kinababa na kinamama yanayoendeshwa kila mwaka ifikapo mwezi wa Ramadhani.

Alisema kutokana na umuhimu wa Elimu Mtume Muhammad Swalallaahu Alayhi Wasallama aliteremshiwa Aya zinazomtaka msome ili aweze kutekeleza mambo mbalimbali kwa kutumia elimu ikiwemo ibada.

Alisema kuwa uislamu ni dini inayohitaji watu wasome na kuongeza kuwa haikubainishwa kitu gani cha kusoma na kwamba swala la kutafuta elimu halina mipaka ya kitu gani cha kusoma bali kinachozingatiwa ni elimu yenye manufaa na inayosomwa kwaajili ya Mwenyezimungu.

Akizungumzia mpango huo wa kutoa elimu kwa kina baba na kina mama Mkoani Pwani ulioanzishwa na kaimu sheikh wa Mkoa wa Pwani Sheikh Khamis Mtupa, Sheikh Zuberi alisema ni mpango mzuri unofaa kuigwa na masheikh wengine ili kueneza elimu kwa umma wa kiislamu.

Aliongeza kwa kusema kuwa Uislamu hautenganishwi na elimu na wala elimu haitenganishwi na uislamu hivyo waislamu wanapaswa kusoma masomo mbalimbali ikiwemo Maarifa ya uislamu, Uchumi, Ujasiliamali pamoja na kusoma umuhimu wa mahusiano mema baina ya mtu na mtu kama alivyoishi Mtume Muhammad Swalallaahu Alayhi Wasalam.

Aidha, sheikh zubeir aliwataka waandaaji wa masomo hayo kutilia uzito katika somo la amani kwani uislamu ndio dini inayopaswa kuongoza katika kulinda amani na sio kuivuruga amani.

Alisema kwa umuhimu wa somo la amani iko haja ya watoa mada kuandaa vipindi na kuvirusha kupitia vyombo vya habari ili somo la amani lienee miongoni mwa jamii.

Awali akisoma taarifa juu ya namna darsa hizo zinavyoendeshwa na aina ya masomo wanayosomesha Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa alisema washiriki wa darsa hizo watasomeshwa masomo mbalimbali yatakayowajengea uwezo katika nayna tofauti tofauti.

Nae  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga alisema mkoa wa Pwani katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhani vyakula vyote vinapatikana kwa wingi katika masoko ya mkoa huo kwa bei za kawaida.

Aidha, alimuhakikishia Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kuwa,  mafuta ya kula na sukari vipo vya kutosha katika Mkoa huo na kwamba tayari ukaguzi umeshafanywa na Mkuu wa mkoa kuhakikisha vitu vyote vipo na vinapatikana bila ya usumbufu wowote.

Akizungumzia swala amani katika Mkoa wa Pwani Mhandisi Ndikilo alisema Mkoa huo kwa sasa hauna matukio ya uvunjifu wa amani huku kamati ya ulinzi na usalama inaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ikiwemo sehemu za kufanyia ibada.

Mpngo huo wa Mafunzo ya uislamu kwa kinababa na kinamama Mkoa wa Pwani yanayofanyika kila mwezi wa Ramadhai umetimiza miaka kumi sasa toka kuanzishwa kwake mwaka 2008 na Kaimu Sheikh wa Mkoa huo Alhaj Hamisi Mtupa.
  
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakari Zuberi (kulia) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga (kushoto) ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Pwani Hamisi Mtupa akisoma taarifa mpango wa darsa hizo mbele ya mgeni rasmi Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakari Zuberi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo
                                              

No comments:

Post a Comment