Saturday, May 26, 2018

KAIMU DC KIBAHA, MAJID MWANGA, ATAKA VIJANA JKT KULINDA AFYA ZAO.


Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akikagua gwaride la vijana wa kujitolea Operesheni Merelani waliopata mafunzo ya awali ya kijeshi sherehe hizo zilifanyika uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha katika Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
 
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Merelani uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha katika Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
.............................................
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj Majid Mwanga amewataka vijana wanaomaliza mafunzo ya JKT kutunza afya zao ili waweze kushiriki katika shughuli za kujenga Taifa kikamilifu.

Majidi aliyasema hayo wakati wa kufunga  mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea operesheni Mererani yaliyofanyika katika kikosi cha jeshi 832 KJ-RUVU JKT.

Alisema kazi ya jeshi ni kazi inayohitai utayari, ari na afya njema hivyo askari ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo anatakiwa awe na afya iliyo imarika.

Aliongeza kuwa katika U tatu walizojifunza yaani Uadilifu, Uzalendo na Uaminifu wasisahau kuwa ni lazima kuwa na afya nzuri itakayomfanya askari kuwa mchangamfu na mwenye nguvu wa kupambana na mazingira ya aina yoyote.

Alisema kutokana na umri wa vijana hao, vipo vishawishi vingi katika jamii vinavyoweza kupelekea kufanya mambo yatakayosababisha kudhoofika kwa afya zao hivyo ni lazima wachukue tahadhari.

Alifafanua kuwa hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini hasa katika wilaya za Kibaha na Bagamoyo inatisha hivyo vijana wa JKT wanapaswa kulitambua hilo na kujua namna ya kukabiliana na hali hiyo ili kujilinda na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Katika hatua nyingine aliwataka kuishi maisha ya kiaskari kwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kama walivyoapa na kuongeza kuwa kiapo ni kifungo.

Alisema haitarajiwi askari aliyepata mafunzo na kula kiapo cha utii afanye vitendo vinavyokwenda kinyume na kiapo chake kwani yeye anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.

Kwa upande wake Mkuu JKT nchini Meja Jenarali Martini Busungu katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkuu wa utawala JKT Makao Makuu, Kanali Hawa Kodi aliwataka vijana hao waliopata mafunzo ya JKT kuwa mfano wa kuigwa katika jamii na ipatikane tofauti kati yao na wale ambao hawakupata mafunzo hayo.

Alisema mafunzo hayo yatumike vizuri katika jamii na wala yasiwe kwaajili ya kuwapiga raia wema na badala yake wawe ndio walinzi wa raia na kuhakikisha wanapinga kwa namna yoyote vitendo vya kihalifu.

Aliongeza kwa kuwataka vijana hao kushirikiana na mamlaka zinazohusika ili kuwafichua waovu, wasaliti na wale wote wasioitakia mema nchi ya Tanzania.

Aidha, alisema katika kipindi hiki ambacho maadili ya kitanzania yameporomoka kwa kuiga tamaduni za watu wa kigeni, Jeshi la Kujenga Taifa lina mchango mkubwa katika kuhakikisha vijana wanakuwa katika maadili mema ya kitanzania ili kulinda heshima ya nchi yetu katika uso wa dunia.
Alisema tamaduni za kigeni nyingi zina athari kubwa katika ustawi wa maadili ya vijana hapa nchini hivyo ni wajibu wa watanzania wote kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa katika malezzi ya vijana ili kupata wazalendo wa nchi yetu.

Awali akisoma taarifa ya vijana hao, Mkuu wa Kikosi cha jeshi cha 832 KJ-RUVU JKT, Kanali Charles Mbuge alisema vijana hao wamejifunza mambo mbalimbali ya kijeshi ikiwa ni pamoja na uvumilivu, nidhamu, na kujituma wanapopewa majukumu.

Aliongeza kuwa katika mafunzo hayo waliweza kujifunza ufugaji wa aina mbalimbali, uandaaji wa bustani za mbogamboga pamoja na kuibua vipai vya sanaa na Michezo na taaluma za aina mbalimbali..

Kanali Mbuge aliwataka vijana hao wakawe askari bora na wawe tayari kutumikia nchi yao ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi pindi watakapohitaika kufanya hivyo.

Aidha, alisema wakufunzi wa vijana hao wametimiza majukumu yao ya kuwajenga katika tabia njema na uzalendo na kwamba  kwa sasa wamebadilika tabia zao na kuongeza maarifa juu ya ufahamu wa mambo mbalimbali.

Wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi, vijana hao wahitimu wa mafunzo ya awali ya kijeshi wa Operesheni Meralani, walisema katika kipindi chote cha mafunzo yao waliweza kupata taaluma ya stadi za maisha na stadi za kazi kwa kujifunza kwa nadharia na vitendo kazi za mikono na ujasiliamali ikiwemo ufugaji wa kuku, Bata, Samaki, na kilimo cha bustani za mbogamboga.

Walisema elimu hiyo waliyoipata itawasaidia kujikwamua kimaisha kwa kujiongezea kipato na kuondokana na umasikini.

Jumla ya vijana 1408 wamehitimu mafunzo yao ya awali ya kijeshi katika kikosi cha jeshi 832 KJ-Ruvu JKT, ambao miongoni mwao wavulana ni 960 na wasichana 448.
 
 Kaimu Mkuu wa utawala JKT Makao Makuu, Kanali Hawa Kodi akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Merelani uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha katika Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
 Mkuu wa Kikosi cha jeshi 832 KJ-RUVU JKT, Kanali Charles Mbuge akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya awali kwa vijana wa kujitolea Operesheni Merelani uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha katika Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
 Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akipata utambulisho wa vikundi tayari kwa maonyesho mbalimbali ikiwemo gwaride la mwendo wa haraka na mwendo pole kupita mbele yake.
Picha juu ni gwaride la mwendo pole na picha chini ni gwaride la mwendo wa haraka Vijana wahitimu wa mafunzo ya awali ya kijeshi wakiongozwa na wakufunzi wao wakipita mbele ya mgeni rasmi, katika uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
Wakufunzi na maafisa wa ngazi mbalimbali wa jeshi wakishuhudia vijana wao katika kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi yaliyofanyika
uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
 
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo (kushoto) akizungumza jambo na  Mkuu wa Kikosi cha jeshi 832 KJ-RUVU JKT, Kanali Charles Mbuge (kulia).
 
Meza kuu, katikati ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, kushoto ni  Kaimu Mkuu wa utawala JKT Makao Makuu, Kanali Hawa Kodi ambae alimuwakilisha Mkuu wa JKT nchini Meja Jenarali Martini Busungu katika shughuli hiyo na kulia ni Mkuu wa Kikosi cha jeshi 832 KJ-RUVU JKT, Kanali Charles Mbuge.
Wageni waalikwa, wazazi wa vijana hao, ndugu jamaa na marafiki wakishuhudia sherehe hizo za kufunga mafunzo ya awali kwa vijana wa kujitolea Operesheni Merelani uwanja wa mabatini huko Mlandizi wilayani Kibaha katika Kikosi cha Jeshi 832 KJ-RUVU JKT.
  Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Alhaj Majid Mwanga, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, akiangalia bwawa la samaki alipokuwa akikagua miradi mbalimbali ya ujasiliamali inayotekelezwa na kikosi cha jeshi cha 832 KJ- RUVU JKT. 

Picha juu na chini ni Vijana wahitimu wa mafunzo ya awali ya kijeshi katika Kikosi cha jeshi 832 KJ- RUVU JKT wakionyesha mazao wanayolima katika kikosi hicho ikiwa ni sehemu ya mafunzo waliyopatiwa.

No comments:

Post a Comment