Serikali
imesema itaendelea na usambazaji wa umeme vijijini kupitia miradi
inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kasi zaidi ili vijiji
vyote vilivyoingizwa kwenye Mradi vifikiwe na umeme.
Kauli
hiyo imetolewa Bungeni na Naibu Waziri wa Nishati Subira Hamisi Mgalu wakati wa
kuchangia Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 ambapo amewahakikishia
wabunge kuwa Serikali kupitia wizara ya Nishati imejipanga kwa kasi mpya ya
utekelezaji wa Miradi hiyo.
Naibu
waziri huyo wa Nishati alisema wizara imepokea changamoto mbalimbali
zilizojitokeza wakati wa kusambaza umeme vijijini kwenye Miradi inayotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijiini (REA) na
kwamba tayari wizara imejipanga kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi
ili kazi isipate vikwazo.
Katika
kuchangia Bajeti ya wizara ya Nishati wabunge walitaka kujua vijiji ambavyo
havijafikiwa na umeme ni mkakati upi wa wizara kuhakikisha vijiji hivyo
vinapata umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Naibu
waziri Subira Mgalu alifafanua kazi zilizofanywa na zile ambazo zinaendelea
kufanywa kupitia REA na kuongeza kuwa hakuna kijiji ambacho kipo kwenye mpango
kitakachorukwa kwenye utekelezaji.
Alisema
wizara imepokea changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa REA
awamu ya kwanza ya pili na ya tatu na kwamba tayari wizara imeweka mpango
mkakati wa kushughulikia kasoro zote zilizojitokeza.
Aliongeza
kwa kusema kuwa kutokana na malalamiko ya wabunge wengi kwamba kuna baadhi ya
vijiji vimerukwa, vitongoji na baadhi ya taasisi za uma hazijafikiwa na umeme
tayari hayo yote yanafanyiwa kazi kwaajili ya utekelezaji
Katika
kuhakikisha hayo yanafanyiwa kazi, tayari wizara imekuja na orodha ya vijiji
vipya 1541 ambavyo vinahitaji kufikiwa na miradi ya REA endapo Bunge
litaidhinisha.
Alisema
tayari mpaka sasa vijiji 545 vimefikiwa na umeme huku vijiji 502 miundombinu
inaendelea kujengwa ili navyo vifikiwe na umeme.
Aidha,
alisema serikali kupitia Benki kuu imeshafungua Barua za mikopo (Leters of
Credit) za bilioni 268 kwa kampuni 18 na kuongeza kuwa hali hiyo itaongeza kasi
ya utekelezaji wa miradi.
Naibu
waziri Subira Mgalu alisema kuwa Miradi ya umeme vijijini ipo ya aina nyingi
ikiwemo wa (Densification –Round I) ambapo Awamu ya Kwanza (Densification –Round I) ulianza mwezi Aprili, 2017
katika mikoa nane (8) ya Pwani, Tanga, Arusha, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Mara
Alisema hadi kufikia mwezi Mei, 2018 awamu hiyo imekamilika
kwa asilimia 98. ambapo jumla ya vijiji 300 kati ya 305 vimepatiwa umeme pamoja
na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 12,084
kati ya 53,000, ambao Gharama ya utekelezaji kwa awamu hiyo ni Shilingi bilioni
62.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, Mradi wa Densification
awamu ya pili utahusisha vitongoji vilivyomo katika vijiji 4,090 vilivyosalia
na unakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi bilioni 1,938. na kwamba Awamu hiyo itaanza kutekelezwa mwezi
Julai, 2018.
Naibu
waziri wa Nishati aliendelea kufafanua kuwa, baada ya kubaini mahitaji ya umeme ni
makubwa upo Mradi mpya unaojulikna kama Mradi
wa Usambazaji Umeme katika Vijiji vilivyopo Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban
Rural Electrification Program) ambao utasaidia kuwafikia watu wengi maeneo hayo.
Alisema Mradi wa Peri-Urban unalenga kusambaza umeme katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa
miji ili kuboresha huduma za kijamii na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo, vya
kati na vikubwa katika maeneo hayo.
Aidha, aliongeza kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) wamekamilisha usanifu wa mradi wa majaribio utakaotekelezwa katika Mkoa wa
Pwani na Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.
Mradi huo utavinufaisha vijiji/vitongoji zaidi ya
250 na kuwaunga wateja wa awali wapatao 37,000 na kusema kuwa Mradi huo
unafadhiliwa na Serikali ya Norway
kwa gharama ya Shilingi bilioni 83. na kwamba unatarajiwa kukamilika mwezi
Aprili,2019.
Alisema
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika mpango wake ni
kufikisha umeme vijiji vyote 7200 ifikapo mwaka 2020 hivyo wao kama
viongozi katika wizara yenye dhamana ya Nishati ni kuhakikisha wanakwenda
sambamba na malengo ya Rais Dkt. Magufuli.
Wakati
huohuo Naibu waziri huyo wa Nishati alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB)
imeonyesha nia ya kusaidia usambazaji wa umeme katika miji mikubwa ya Mwanza,
Arusha Dodoma ambapo tayari upembuzi yakinifu unaendelea kuhusu miradi hiyo.
Aidha,
Naibu waziri huyo wa Nishati ametoa wito kwa wasimamizi wa Miradi na Wakandarasi kote
nchini kuwashirikisha wenyeviti wa serikali za mitaa, Wabunge, na Wakuu wa wilaya
ili kuhakikisha Miradi hiyo inatekelezwa kwa uwazi bila ya upendeleo utakaypelekea manung'uniko kutoka kwa wananchi au wawakilishi wao ambao ni wabunge.
Alisema
wananchi wanatakiwa kuchangia kuunganishwa umeme kwa gharama ya 27,000 tu na si
zaidi ya hiyo na kwamba ameonya wale watakaokiuka maagizo hayo.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Hamisi Mgalu akitoa ufafanuzi Bungeni kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
imeandikwa na Athumani Shomari wa bagamoyokwanza.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment