Tuesday, August 29, 2017

DADA POWA, KAKA POWA, MARUFUKU BAGAMOYO.



Mkuu wa Wiaya ya Bagamoyo, Alhajj, Majid Mwanga amemuagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, kuwakamata wale wote wanaojishughulisha na biashara ya ngono wanawake na mashoga,  maarufu kama dada powa, na kaka powa, ili kukomesha vitendo hivyo katika Wilaya ya Bagamoyo.

Mh. Majid, aliyasema hayo wakati wa kuzindua Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiaya ya Bagamoyo uliozinduliwa jana Tarehe 28 Agosti 2017. katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.

Alisema katika mitaa ya Bagamoyo wapo kina dada powa na kaka powa, ambao ni kichocheo cha maambukizi ya VVU na UKIMWI na kwamba sasa ni marufuku kuona dada powa na kaka powa katika wilaya ya Bagamoyo.

Aliongeza kwa kumtaka Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, kufanya doria katika mitaa ya Bagamoyo ambayo inafahamika kwa biashara ya ngono na kuwakamata wale wote wanaohusika lengo likiwa ni kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI lakini pia ni kurudisha utamaduni wa Bagamoyo ambao ni kuwa na maadili mema na sio kujiuza.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo, alimtaka Mkuu wa Polisi pia kuwakamata wale wanaouza pombe hovyo, wauzaji wa dawa za kulevya na Bangi kwakuwa hivyo vyote ni visababishi vya maambukizi ya VVU na UKIMWI. katika wilaya ya Bagamoyo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya pia alimuagiza mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo kuwakamata  wacheza ngoma wakiwa nusu uchi katika mitaa ya Bagamoyo kwani ni vitendo vinavyokiuka maadili ya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla.

''Wapo wanaocheza ngoma wakiwa uchi na wengine wakipita kwenye magari na kutoa viuno nje na wengine kwa miguu, hawa OCD. washughulikie'' Alisema Mkuu wa wilaya Majid.

 Awali akiwasilisha mada mbele ya Mgeni Rasmi, Mratibu wa Huduma za Ushauri na Upimaji wa VVU Wilaya ya Bagamoyo, Mmanyi Philipo, alisema Tanzania katika kupunguza maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI Kitaifa kutoka asilimia 7% Mwaka 2003-2004 hadi Asilimia 5.1% Mwaka 2011 – 2012:

Aidha, Wilaya  ya Bagamoyo, Kiwango cha Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI ni Asilimia 5.9% ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kiwango cha Maambukizi ya VVU Kitaifa ambacho ni Asilimia (5.1%).
 Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP. Adam maro.


TAMKO LA WAZIRI WA AFYA KUHUSU MADHIMISHO YA SIKU YA TIBA ASILI YA MWAFRIKA

Waziri-Ummy-Mwalimu 

Ndugu wananchi,

Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yalianza rasmi mwaka 2003 baada ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo.  Maadhimisho haya hufanyika katika nchi 46 za kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani tarehe 31/08 ya kila mwaka.

Ndugu wananchi,

Tanzania, inaadhimisha maadhimisho haya kwa malengo makuu manne.

 Kwanza Tanzania ina nia ya kufufua ari na kujenga heshima ya huduma za tiba asili ambazo historia inatuambia kuwa zimekuwa zikikandamizwa na kudharaulika. Kwa kiwango kikubwa ukoloni pamoja na ukoloni mambo leo umekuwa ukikandamiza tiba zetu za asili na kufanya Waafrika wenyewe kuzinyanyapaa tiba hizo. 

Hali hiyo imetufanya tuyumbe, tukose dira na mwelekeo katika suala zima la kuboresha  Tiba Asili katika nchi yetu.

Pili kwa kupitia maadhimisho haya Serikali inawahamasisha Waganga wa Tiba Asili kujiepusha na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina na uchawi kama chanzo cha ugonjwa. Kuna taarifa  na migongano mingi ya kutisha juu ya hili.  Itakuwa jambo la busara kwa waganga wa tiba asili kupitia kwenye vyama vyao kupanga mikakati ya kudhibiti na kuondoa kabisa vitendo vibaya vinavyochafua  taaluma yao.

Tatu, maadhimisho haya yanahimiza masuala ya uboreshaji na usajili wa dawa za asili. Lengo ni kuweza kutengeneza dawa kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya utengenezaji dawa bora. Aidha  utafiti endelevu wa dawa za asili kwa magonjwa mbalimbali unahimizwa kwa madhumuni ya kupata dawa ambazo zinaweza kupatikana kiurahisi  ili mwenye kuhitaji aweze kuzipata.
Nne, kwa kupitia maadhimisho haya Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na huduma za afya.
Ndugu wananchi,

Kama mnavyofahamu katika kuadhimisha Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika kila mwaka tunakuwa na ujumbe maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu ni “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa” (“Integration of Traditional Medicine in Health Systems: The journey so far”).

Kauli mbiu hii inawalenga na kutoa majukumu kwa Viongozi na Wataalam wa Tiba ya Kisasa kuweza kushirikiana na Waganga wa Tiba Asili katika utoaji wa huduma za afya. Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafanikiwa kuijumuisha huduma za tiba asili katika utoaji wa huduma za afya; Serikali imerasimisha huduma za tiba asili kwa kujumuisha katika Sera ya Afya; kuwepo kwa Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu za utoaji wa huduma za tiba asili nchini.

Aidha, Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kusajiliwa, kusajili vituo na dawa zao zinazotumika hususan dawa zinazouzwa katika maduka ya dawa za asili.

 Hadi tarehe 30 Juni, 2017; waganga 16,200; vituo 212 na dawa za asili tatu zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. 

Huo ni mwanzo mzuri ijapokuwa juhudi zaidi zinahitajika kuwezesha “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa”. Vilevile; nitoe wito kwa Waganga wa Tiba Asili kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma za tiba asili kwa wateja wao. 

Nawataka wajiepushe na matangazo  yanayokizana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa pamoja na kuondoa mabango yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kwa mfano UKIMWI.

Ndugu wananchi,
Napenda kuwakumbusha wananchi kwamba kwa  sasa huduma za tiba asili zinatambuliwa rasmi kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Afya na Sheria namba 23 ya mwaka 2002. Madhumuni ya sheria hii ni kusimamia, kudhibiti na kuendeleza tiba asili ya Tanzania. Vilevile, udhibiti wa maadili ya uganga na ukunga wa tiba asili nchini umepewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala limeundwa kama chombo kikuu cha Serikali kitachosimamia na kuratibu shughuli hizo.

 Sheria hiyo  pia inalinda afya na haki za watumiaji wa tiba ya asili na tiba mbadala, kuboresha na kuendeleza tiba na dawa za asili, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuondoa utoaji holela wa Tiba Asili. 

Ni muhimu kwa kila mganga wa tiba asili kuzingatia Sera, Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kuachana na matangazo yasiyofaa, kuacha kuweka mabango hovyohovyo barabarani, matangazo katika vyombo vya habari ni lazima yapate kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Ndugu wananchi,
Tanzania tunayo mitidawa mingi na mingi inayotumika kutibu magonjwa mbalimbali.  

Wataalam mbalimbali ikiwa pamoja na waganga wa tiba asili sajilini dawa zenu ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengi. Pia, ni ukweli usiopingika kuwa  dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mitidawa, na elimu ya mwanzo kabisa juu matumizi ya miti hiyo kutumika kama dawa inatokana na waganga wa tiba asili. 

Tanzania ina rasilimali kubwa ya mitidawa na wapo waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema  waganga wa tiba asili kwa kushirikiana na Serikali kuendeleza ujuzi na utalaamu wao kwa madhumuni ya maendeleo yao na jamii nzima kwa ujumla.


Ndugu wananchi,
Mwaka huu 2017 maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika yanafanyika kwa kutoa elimu kwa wananchi kazi ambayo imeanza rasmi tarehe 28/08/2017 na itaendelea kutolewa hadi kilele tarehe 31/08/2017. Katika muda huo wote mada mbalimbali zitakuwa zinatolewa ili kuwaelimisha wananchi na hususan watoa huduma wa tiba asili na tiba mbadala kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo.  

Wananchi na wadau wa tiba asili nchini ni vema mkasikiliza taarifa hizo.
Ahsanteni

TFF YAREKEBISHA NGAO YA JAMII WALIOICHUKUA SIMBA.

 Hatimaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefanya marekebisho katika Ngao ya Jamii waliyoshinda Simba.

Simba walikabidhiwa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga kwa mikwaju 5-4 ya penalti, lakini ikawa na makosa katika maandishi.
 
Ngao hiyo ilikuwa imeandikwa, Community Sheild badala ya Community Shield.

Baada ya malalamiko kuwa makubwa, TFF iliomba Simba kuirudisha ngao hiyo kwa ajili ya marekebisho na sasa hilo, limefanyika.

UZINDUZI WA MPANGO MKAKATI WA MAAMBUKIZI YA VVU BAGAMOYO.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga,(kushoto), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu, (katikati) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issah, Wakionesha kitabu kuashiria kuzindua rasmi kwa
Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga, akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana Agosti 28, 2017. katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo.
 ..............................
Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo, umezinduliwa Rasmi hapo jana Tarehe 28 Agost 2017. huku wadau wa mpango huo wakitoka na azimio la utekelezaji ili kufikia malengo yake.

Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga, amesema vita dhidi ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI sio ya mtu maalum, na kwamba kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kupambana kwa namna itayosaidia kupunguza maambukizi mapya katika wilaya ya Bagamoyo na hatimae kufikia lengo la kitaifa la asilimia 5.1 

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inaongeza juhudi ya kupambana na maambukizi mapya kwa kuwashirikisha watu mbalimbali na makundi maalum lengo likiwa ni kufikisha ujumbe utakaosaidia kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI katika Wilaya ya Bagamoyo.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kumuomba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, kutenga kiasi cha fedha kutoka katika Asilimia 5 za vijana na asilimia 5 za kinamama kuangalia namna ya kuwawezesha watu wanaoishi na VVU ili waweze kuto Elimu kwa makundi mbalimbali kuhusiana na madhara yatokanayo na VVU na UKIMWI lakini pia namna ya kuhamasisha jamii isiweze kuingia kwenye vishawishi vitakavyopelekea maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Awali akiwasilisha mada mbele ya Mgeni Rasmi, Mratibu wa Huduma za Ushauri na Upimaji wa VVU Wilaya ya Bagamoyo, Mmanyi Philipo, alisema Tanzania katika kupunguza maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI Kitaifa kutoka asilimia 7% Mwaka 2003-2004 hadi Asilimia 5.1% Mwaka 2011 – 2012:

Aidha, Wilaya  ya Bagamoyo, Kiwango cha Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI ni Asilimia 5.9% ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kiwango cha Maambukizi ya VVU Kitaifa ambacho ni Asilimia (5.1%).
 
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga,(kushoto) akipokea kitabu kutoka kwa Afisa Vijana wilaya ya Bagamoyo, Hellen E. Kisanji, kwaajili ya uzinduzi wa Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo, wanaoshuhudia wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Isaha, na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu.
   Mratibu wa Huduma za Ushauri na Upimaji wa VVU Wilaya ya Bagamoyo, Mmanyi Philipo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.
 Afisa Mwitikio wa Taasisi za Umma Dr. Hafidh Ameir, kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania,(TACAIDS) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.
 Meza kuu, wa pili kushoto ni mgeni Rasmi (katika) uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga, wa kwanza kushoto ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu wa tatu kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Ally Ally, wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.
Wa kwanza kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Erica Yegela, wa pili ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP. Adam Amani Maro, wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.
 Makamo Menyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Saidi Ngatipula.
Washiriki kutoka asasi mbalimbali za kiraia.
Watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo.


Picha ya pamoja Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhajj, Majid Hemed Mwanga,(mwenye tai katikati) na washiriki wa mkutano huo wa kuzindua Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiayani Bagamoyo.