Na. Josephine
Majura na Saidina Msangi, WFM, Dodoma.
Serikali imeeleza kuwa Sheria ya Kodi imetoa msamaha wa kodi kwa
wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na wastaafu ambao mapato yao kwa mwaka hayazidi
Shilingi milioni nne.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Lupembe, Mhe.
Joram Ismael Hongoli, aliyetaka kujua sababu za Serikali kutoweka utaratibu wa
kutowatoza kodi wastaafu ambao biashara zao hazizidi mtaji wa Shilingi milioni
nne.
Dkt. Kijaji alisema kuwa wastaafu walioanzisha miradi midogo ya kilimo
na biashara ambayo inawaingizia kipato kisichozidi Shilingi milioni nne
hawapaswi kutozwa kodi kwa kuwa Sheria ya Kodi imetoa msamaha.
Alisema kuwa Kifungu cha nne cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinatoa
msamaha wa kodi ya mapato kwa mfanyabiashara ambaye mapato yake ghafi ya mwaka
hayazidi Sh. milioni 4, hii ikiwa ni pamoja na mapato ya wafanyabiashara
wastaafu ambao kiwango chao cha mapato hakizidi kiasi hicho kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment