Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaandaa Mpango
wa Matumizi Bora ya Ardhi katika maeneo yote yanayozunguka vituo vya treni ya
mwendo kasi (SGR) ili kuwezesha ardhi ya maeneo hayo kuendelezwa kwa kuzingatia
shughuli zitakazokuwa zikifanyika sambamba na mahitaji muhimu kwa watumiaji wa
vituo hivyo.
01. Mhandisi
Yusuph kutoka kampuni ya Yapi Merkezi (wa kwanza kushoto) akiilezea timu ya
Maafisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, ramani ya ujenzi wa kituo kikuu
cha Morogoro pamoja shughuli zitakazokuwa zinafanyika katika kituo hicho ili wataalam
hao waweze kuandaa mpango wa kuendeleza eneo hilo kulingana na shughuli
zitakazokuwa zinatekelezwa katika kituo hicho. Kituo hiki cha Morogoro
kimezungukwa na shamba la mkongwe pamoja na makazi ya watu.
Hayo yalibainishwa juzi na Afisa Mipango Miji kutoka Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Edward Mpanda wakati timu ya Wataalamu
kutoka Idara ya Mipango Miji ilipotembelea mradi huo katika eneo la Kilimanjaro
mkoani Morogoro, sehemu kinapojengwa kituo kikuu cha treni ya mwendo kasi.
Alisema, Wizara yake imejipanga kwa kushirikiana na Tume ya
Matumizi Bora ya Ardhi pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha
inaandaa mpango maalum wa kuendeleza Ardhi inayozunguka vituo vya treni ya SGR ambayo
ujenzi wake ulishaanza.
Kwa mujibu wa Mpanda, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi pamoja na Tume ya Matumizi bora ya Ardhi itahakikisha pia reli ya kisasa
(SGR) inatunzwa kwa kuzingatia mpango uliowekwa ili kuleta ufanisi na maendeleo
kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.
‘‘Kama Wizara isiposimamia uendelezaji Ardhi inayozunguka eneo
la mradi, basi kila mmoja atakuja na ujenzi wake bila kujali athari
itakayotokea kutokana na shughuli zitakazokuwa zikiendelea katika vituo hivyo
vya treni’’ alisema Mpanda.
Aidha, Afisa huyo wa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi alisema Usimamiaji wa uendelezaji Ardhi katika maeneo
yanayozunguka mradi wa ujenzi reli ya kisasa (SGR) utasaidia kuondoa ujenzi
holela katika maeneo hayo na kuweka miundo mbinu itakayokuwa na tija kwa
watumiaji hasa katika vituo vyote vikubwa na vya kati
Kwa upande wake Mhandisi Hamza Said kutoka Shirika la Reli
Tanzania, aliishukuru timu ya Wataalamu wa Mipango Miji kwa kutembelea mradi
huo na kubainisha kuwa Wizara ya Ardhi bado haijachelewa kuandaa mipango yake
na kusisitiza muda bado upo kwa kuwa ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea.
‘‘Kuweka mpango wa kuendeleza maeneo kwenye vituo vya treni ya
mwendo kasi itakuwa na faida kwa sababu maeneo hayo yatakuwa na tija kwa
watumishi watakaokuwa wakihudumia vituo hivyo lakini pia na kwa wasafiri wa
treni ya mwendo ya kasi na ile ya kawaida’’ alisema Mhandisi Hamza
Timu ya Wataalamu wa Mipango Miji kutoka Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa lengo la kubaini aina ya Ardhi inayozunguka maeneo inakojengwa ili kuweka mikakati ya jinsi ya kuyaendeleza maeneo hayo.
01. Mhandisi
Hamza Said (mwenye kofia) kutoka Shirika la Reli Tanzania akiwaelezea wataalam
wa Mipango Miji Kutoka Wizara ya Ardhi ramani ya ujenzi wa kituo kikuu cha Dar es
Salaam na shughuli zitakazokuwa zinafanyika katika kituo hicho. Kituo cha Dar
es Salaam ndiyo kituo kikubwa zaidi na kituo namba moja cha treni ya mwendo
kasi. Treni ya mwendo kasi na ile ya kawaida zote zitakuwa zinaanzia safari
zake katika kituo hiki cha Dar es Salaam ambapo treni ya mwendo kasi itakuwa
inapita juu na ile ya kawaida itakuwa inapita chini bila kuathiri shughuli za
maendeleo za kila siku.
|
Mfumo wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa na Kampuni
ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki umegawanywa katika awamu mbili ambapo awamu
ya kwanza yenye vituo sita inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro huku awamu ya
pili ikianzia Morogoro hadi Makutopora Manyoni mkoani Singida ikijumuisha vituo
tisa.
01. Timu
ya Maafisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, wakijadiliana na wahandisi wa
ujenzi reli ya kissasa (SGR) jinsi gani wanaweza kushirikiana na Shirika la
Reli Tanzania kuendeleza maeneo yanayozunguka vituo kwa kuzingatia shughuli na
mahitaji ya vituo hivyo vya treni ili kuepuka ujenzi holela katika maeneo yote
yatakayokuwa na vituo vikubwa na vya kati vya treni ya mwendo kasi.
No comments:
Post a Comment