Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari
(hawapo pichani) dawa ambayo imetolewa na Madagascar leo Jijini Dae es Salaam.
........................................
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa dawa ambayo nchi ya
Madagascar imeitoa kama msaada wa Serikali ya Tanzania ni kwa ajili ya utafiti
kwanza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaambia waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuwa dawa hiyo inayojulikana kaitaalamu kama
“COVIDORGANICS” ni kwa ajili ya utafiti na siyo kwa ajili ya matumizi ya
binadamu.
“Huu mzigo (dawa) ni kwaajili ya
kufanyiwa utafiti…….na kazi kubwa tunayoianza leo ni na wataalamu wetu wa afya
ni kufanya utafiti,” Amesema Prof. Kabudi
Prof. Kabudi ameongeza kuwa dawa hiyo
siyo kwa ajili ya kugawa kwa wananchi, bali ni kwa ajili ya utafiti na mara baada
ya utafiti kukamilika wataalamu wa afya watatoa maelekezo ya jinsi ya utumiaji
wa dawa hiyo.
Aidha, dawa hiyo imegawanyika katika
makundi mawili ambapo kundi la kwanza la dawa ni kwa ajili ya kujikinga na
maambukizi ya COVID 19 kwa wale ambao hawajaambukizwa ugonjwa wa Corona. Kundi
la pili ni kwa ajili ya matibabu kwa wananchi ambao tayari wameathirika na
COVID 19.
“Dawa hii tuliyokuja nayo jana kutoka
Madagascar mara baada ya utafiti kukamilika na kupata ushauri wa kitaalamu
kutoka kwa wataalamu wetu wa afya itatumika kukinga wananchi ambao
hawajaathirika na kutibu wale walioathirika,” Prof. Kabudi
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa
serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa mara baada ya kupokea dawa hiyo kazi ya
kwanza ya ni kuanza utafiti ambao utaonesha kama dawa hiyo ni salama na haina
madara kwa wananchi na pili utafiti wa kuangalia ubora wa kutibu au kupunguza
makali ya COVID 19.
“Mara baada ya utafiti wa dawa hii
kukamilika itatumika katika makundi matatu ambayo kundi la kwanza ni wagonjwa
kutumia dawa ya kawaida, kundi la pili watapata dawa ya kawaida na hii
iliyotoka Madagascar na kundi la tatu wagonjwa watatumia dawa ya kawaida na ile
inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr),” Amesema
Prof. Makubi
Prof. Makubi pamoja na mambo mengine
ametoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari katika kujikinga na ugonjwa wa
COVID 19 na wasibweteke na lolote.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti
wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya amesema kuwa Nimr imejipanga
kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali hasa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali katika kuhakikisha inafanya utafiti wa kina juu ya matumizi ya dawa
hiyo.
“Nimr inafanya tafiti mbalimbali za
kupambana na ugonjwa huu wa COVID 19 na itaendelea kufanya tafiti hizo ili kuwasaidia
watanzania,” amesema Prof. Mgaya
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu inalo jukumu
lakuchunguza dawa au sumu zozote kwenye sampuli, kukadiria kwa usahihi kiasi
cha dawa, umetaboli au sumu.
Drkt. Mafumiko ameongeza kuwa,
kupitia utafiti wa dawa hiyo, ofissi yake kwa kushirikiana na wataalamu wa afya
watatafsiri matokeo ya uchunguzi katika dawa hiyo kutoa maelekezo sahihi juu ya
matumizi yake kwa mwananchi.
Mkutano huu ulihudhuriwa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
(Mb), Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya, Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili
Dkt. Paul Mkama.
Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi
akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika
leo Jijini Dae es Salaam
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu (NIMR) Prof. Yunus Mgaya akiongea na waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dae es Salaam
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko
akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano
Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili Dkt. Paul
Mkama akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati mkutano
ukiendelea
No comments:
Post a Comment