Wednesday, May 13, 2020

WANAKIJIJI RUTAMBA HALMASHAURI YA MTAMA KUONDOKANA NA SHIDA YA MAJI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

HATUA  ya Serikali kupitia wakala wa Maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Lindi Mkoani humo kufanya ukarabati wa mradi wa maji katika kijiji cha Rutamba halmashauri ya Mtama kinaelezwa kitasaidia kunusuru Ndoa za wakazi wa kijiji hicho

Mradi huo ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 340 unatekelezwa kupitia mpango wa PFR (Payment for Result) kwa kutumia mafundi wa kawaida na umeanza kutekelezwa rasmi 22/04/2020 na unatarajiwa kukamilika  tarehe 30/06/2020

Akieleza  matumaini yake Mwanaidi Saidi Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho   mbele ya kamati ya ulinzi na usalama  ya wilaya hiyo iliyofika katika kijiji hicho ili kujionea maendeleo ya mradi huo, alisema kuwa  kinamama wa maeneo hayo  hutumia muda mwingi kuhangaika kutafuta maji hali ambayo inawafanya waume zao kukosa imani kwa  wanawake hao

“Kwa kweli swala la maji ni pigo sana kwa kina mama kwa sababu  yani mama mpaka saa sita ya usiku hajalala anasubiri maji  na kwa vile maji yalikuwa hayatoki tulikuwa tunaenda mtoni  ambako ni mbali na kijiji kilipo  ambako pia tulikuwa tunalazimika kutoka  saa kumi alfajiri ili tuweze kuwahi kufika  na kuchota maji na kuondoka” Alisema Mwanaidi.

“Kwa kuwa sasa maji yanatoka na kukatika  kwa muda  wa usiku, kwa hivyo  kinamama tunakaa kwenye vile  vilula  kuanzia saa mbili ya usiku  mpaka saa sita na wakati mwingine maji tunakosa, kiasi kwamba tunakata tama tunaamua kwenda kulala tuamke tuu saa kumi ili twende mtoni tukafuate maji”


Mwanaidi alisema  Hali hiyo inawafanya waume  walio wengi wa maeneo hayo  kukosa  imani kwa wanawake zao kuwa huwenda wanatumia mwanya huo wa kutafuta maji kuchepuka ndoa zao  

“Muda mwingi tunatumia kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za kimaendeleo , tunatumia zaidi ya massa sita mpaka saba kutafuta maji  mfano ukitoka nyumbani saa 10 alfajili utarudi nyumbani saa tatu au saa nne Asubuhi  tena ukiwa umepata kindoo kimoja ambacho hata hakitoshi kwa matumizi ya hapa nyumbani” alieleza mama mwingine Fatuma selemani.

Kwa mujibu wa meneja wa Ruwasa wilaya ya Lindi Iddy Pazi amesema kuwa  Mradi wa Maji Rutamba ni kati ya Miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa PFR katika wilaya hiyo  ambayo inaghalimu kiasi cha Bilioni 100.na milioni 1

Alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa matanki mawili ya maji ya lita laki moja , vituo vinne vya kuchotea maji  (vilula) ambavyo vitakuwa na koki mbili mbili pamoja na ukarabati wa koki kumi na saba ambazo zilikuwa zikitumia awali



Nae mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga  akiongozana  na kamati hiyo akizungumza mara baada ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo alimtaka Meneja huyo wa Ruwasa kuhakikisha miradi yote anayoisimamia inakamilika kwa wakati.


No comments:

Post a Comment