Monday, May 4, 2020

DKT. KAWAMBWA AKABIDHI NDOO ZA MAJI KWA MAKUNDI MBALIMBALI BAGAMOYO.


 Hizi ni baadhi ya ndoo za maji kwaajili ya kunawa mikono, pamoja na sabuni alivyokabidhi Mbunge wa Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa jana Mei 3, 2020 ikiwa ni harakati za kupambana na ugonjwa wa Corona.

 Mbunge wa Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa akizungumza na wananchi wakati wa kukabidhi ndoo za maji kwaajili ya kunawa mikono, pamoja na sabuni katika maeneo mbalimbali jimboni humo.
......................................... 


Na Selestian James.

Mbunge wa jimbo la Bagamoyo mkoani Pwani Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, amegawa ndoo za maji kwaajili ya kunawa mikono, pamoja na sabuni katika maeneo mbalimbali ya kata ya Dunda, Nianjema na Magomeni ikiwa ni muendelezo wa mapambano dhidi ya maamukizi ya  ugonjwa wa Corona.

Ziara hiyo iliyopitia vijiwe mbalimbali vya pikipiki na maeneo ya masoko, Dkt. Kawambwa amewatahadharisha wafanyabiashara pamoja na watu wanaokuja katika maeneo hayo kupata mahitaji mbalimbali kuwa ugonjwa wa Corona ni hatari sana kwani unaenea kwa kasi mno hivyo hakuna budi kuchukua tahadhari na maradhi hayo.

Aidha, Dkt. Kawambwa amewataka waendesha pikipiki kuhakikisha abiria zao wananawa vizuri mikono yao kwa kutumia maji tiririka na sabuni hizo kabla ya kupanda kwenye usafiri huo, kwani kwa kufanya hivyo kwa kiasi kikubwa watajiepusha na maambukizi hayo.

"Vijana wangu waendesha pikipiki na wafanyabiahara hakikisheni mnachukua tahadhari kwa kiasi kikubwa kuhusu ugonjwa huu ili uweze kujikinga wewe binafsi na familia nyumbani" Alisema Dkt. Kawambwa.

"Tunaona namna ambavyo maambukizi hayo yanavyoendelea siku hadi siku kwa nini nawe usiunge mkono juhudi za muheshimiwa Rais Dkt. Maghufuli na viongozi mbalimbali za kuhakikisha tunabaki salama"? Alimalizia kwa kuhoji.

Alisema ameongea na wahisani waliowahi pia kusaidia katika operesheni ya macho bure ambao ni Bilal eye camp, nao kwa kuona umuhimu wa tahadhari ambapo wamekubali kutoa ndoo za maji na sabuni ili zitumike kunawa mikono.

Dkt. Kawambwa amewatahadharisha juu ya namna ya kukaa kwa nafasi kidogo kutoka mtu mmoja na mwingine ili kujikinga zaidi.

Kwa upande wao madiwani wa viti maalum, Shumina Rashidi na Hafsa Kilingo wamewataka wafanyabiashara hao wa kata hizo kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanashinda vita dhidi ya corona.

Aidha,  madiwani wa kata ya Nianjema Abdul Pyallah na Diwani wa kata Dunda Dickson Makamba wamemshukuru na kumpongeza Mbunge Dkt. Kawambwa, kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu.

lakini pia wamewataka wafanyabiashara hao kutosahau umuhimu wa kuvaa barakoa  wakati wote katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wao waliopokea misaada hiyo ya ndoo za maji na sabuni kwaajili ya kunawa mikoni wamemshukuru Mbunge huyo kwa juhudi zake za kuwajili wananchi wake hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

Wamesema ndoo hizo zimepetaikana katika wakati muafaka ambapo matumizi yake ni muhimu sana katika jamii ili kujikinga na Corona.
 
Diwani wa kata Dunda Dickson Makamba, akinawa mikono mara baada ya kupokea ndoo za maji kutoka kwa Mbunge na yeye kukabidhi kwa wananchi wa kata yake hapo jana Mei 3, 2020.
 
Diwani wa kata ya Nianjema, Abdul Pyallah akikabidhi ndoo za maji kwa wananchi wake baada ya yeye kupokea kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Mei 3, 2020.
 
Diwani wa viti maalum, Hafsa Kilingo, akinawa mikono mara baada ya kukabidhi ndoo za maji kwa wananchi.
 
Diwani wa viti maalum, Shumina Rashid, akinawa mikono mara baada ya kukabidhi ndoo za maji kwa wananchi.
Madereva wa Bodaboda wakinawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara baada ya kupokea msaada wa ndoo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Mei 3, 2020. Picha zote Na Selestian James. 

No comments:

Post a Comment