Baadhi ya pikipiki zilizotolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Maafisa
Tarafa nchini ambazo zimekabidhiwa rasmi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bw. Jumanne Sagini Mei 08, 2020 Mjini Bariadi kwa maafisa tarafa wa mkoa wa
Simiyu.
.........................
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw.
Jumanne Sagini amewakabidhi pikipiki Maafisa Tarafa 15 wa Mkoa huo ambazo ni
utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli aliyoitoa mwezi Mei 2019 wakati alipokutana na Maafisa tarafa
wote nchini katika kikao kazi jijini Dar es Salaam.
Akiwakabidhi pikipiki hizo Mei 08,
2020 Mjini Bariadi Sagini amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa pikipiki hizo
zitakazorahisisha utekelezaji wa majukumu ya Maafisa tarafa huku akiwaagiza
kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa; ikiwa ni pamoja na
kufuatilia mkakati wa elimu wa Mkoa wa kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa
katika likizo ya dharura ya tahadhari ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
Tumeandaa mkakati wa mkoa wa
kuwawezesha wanafunzi kusoma kipindi ambacho wako likizo ikiwa ni tahadhari ya
maambukizi ya Virusi vya Corona; moja ya majukumu yenu katika kipindi hiki ni
kuhakikisha mkakati unatekelezwa kwenye maeneo yenu ya utawala; walimu, maafisa
elimu watatimiza wajibu wao nanyi pia mna sehemu yenu,”alisema Sagini.
Aidha, Sagini amewataka maafisa
tarafa hao kuzitumia pikipiki hizi kwa kuwafikia wananchi wote wakiwemo
wakulima hasa kipindi hiki cha mavuno na lengo kuu likiwa ni kuwaasa kutunza
chakula.
Awali akisoma taarifa katibu tawala
msaidizi utawalana rasilimaliwatu katika Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw.
Ekwabi Mujungu amewataka maafisa tarafa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa
madhumuni yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kusukuma shughuli za maendeleo ya
jamii ikiwemo kusimamia miradi ya elimu ,afya kilimo na hifadhi ya
mazingira.
Wakati huo huo Mujungu ametoa
maelekezo kwa makatibu tawala wa wilaya mkoani Simiyu kutenga fedha kwa ajili
ya mafuta na matengenezo ya pikipiki hizo kwa kila tarafa ili pikipiki hizo
ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Akiongea kwa niaba ya maafisa tarafa
mara baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo afisa tarafa ya Dutwa ,
Isabela Nyaulingo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwawezesha kupata usafiri huo
ambao utarahisisha utendaji kazi wao huku akiahidi kuwa watazitunza na kufuata
maelekezo yote waliyopewa na viongozi.
Jumla ya pikipiki 15 zimekabidhiwa kwa
maafisa tarafa mkoani hapa zikiwa na thamani ya shilingi milioni 33,285,000/=,
ambapo pikipiki moja inagharimu kiasi cha shilingi milioni 2,219,000.
Tarafa zilizonufaika mkoani
Simiyu ni Dutwa, Nkololo na Muhango(BARIADI), Kivukoni na Busega(BUSEGA), Itilima,
Kanadi, Bumela na Kinang’weli (ITILIMA) Mwagala,Sengerema,na Nung’hu( MASWA),
Kisesa Nyalanja na Kimali (MEATU).
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na
Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Bw. Ekwabi Mujungu akiwasilisha
taarifa ya pikipiki zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Maafisa Tarafa ambazo zimekabidhiwa Mei 08,
2020 Mjini Bariadi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini kwa
maafisa tarafa wote wa mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne
Sagini (mwenye suti nyeusi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi wa mkoa wa Simiyu na Maafisa Tarafa wa mkoa huo mara baada ya
kuwakabidhi maafisa tarafa pikipiki zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Maafisa Tarafa nchini
ambazo alizikabidhi Mei 08, 2020 Mjini Bariadi kwa maafisa tarafa wote wa
mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne
Sagini (mwenye suti kulia) akizungumza na Maafisa Tarafa wa mkoa huo
kabla ya kuwakabidhi pikipiki zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Maafisa Tarafa nchini ambazo
zimekabidhiwa Mei 08, 2020 Mjini Bariadi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bw. Jumanne Sagini kwa maafisa tarafa wote wa mkoa wa Simiyu.
No comments:
Post a Comment