Wednesday, May 13, 2020

KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI IMERIDHISHWA NA MAANDALIZI YA ULIPAJI FIDIA LINDI.


NA HADIJA HASSAN, LINDI.

KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini imesema imeridhishwa na kasi ya maandalizi ya ulipwaji wa fidia unaofanywa na Shirika la maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) kwa wananchi 693 wa Mtaa wa Likong’o , Masasi ya leo na Mto mkavu katika kata ya Mbanja halmashauri ya Manspaa ya Lindi Mkoani humo ili kupisha mradi wa Gesi asilia (LNG).


Kauli hiyo imetolewa na kaimu mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini ambae pia ni mbunge viti maalumu , Mkoa wa Lindi CCM, Hamida Abdalla mara baada ya kamati hiyo kufanya ziara katika mtaa huo wa likong’o ambako zoezi hilo la maandalizi ya ulipwaji wa fidia linaendelea.


Hamida amesema kulingana na maadalizi yaliyofanywa na shirika hilo yataweza kuondoa malalamiko kwa wananchi walioathirika na mradi huo kwani wamerahisisha kupatikana kwa watu na vitengo vyote muhimu kuwepo katika maeneo hayo.



“Sasa mambo yameiva hayawi hayawi sasa yamekuwa kwa hivyo ndugu zangu wanalikong’o, Masasi ya Leo na Mto mkavu, mambo yote yapo hapa tumerahisishiwa ofisi ya ardhi ipo hapa, watu wa benk wapo hapa wanasheria wapo hapa, wapiga picha pia wapo hapa kwa hivyo tunashukuru sana kwa utaratibu huu ambao Serikali kupitia (TPDC) umeufanya na umewarahisishia wananchi” Alisema Hamida.


Hamida pia alisema kuwa Wananchi wanapaswa kusoma kwa usahii mikataba wanayosaini pamoja na pesa wanazotakiwa kulipwa huku akisisitiza kuwatumia wataalamu waliopo kikamilifu ili kuondoa malalamiko mara baada ya zoezi hilo kukamilika.


Akielezea utaratibu wa zoezi hilo mbele ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Meneja wa uwendelezaji na uzalishaji wa Mafuta na Gesi (TPDC) Modestus Lumato Alisema kutokana na malipo hayo kuchelewa kulipwa kwa muda uliotarajiwa wananchi hao pamoja na fedha zao za fidia watapaswa kulipwa na fedha za ucheleweshaji wa miaka mitano.


Kwa mujibu wa Lumato wananchi hao walifanyiwa uthamini wa maeneo yao tangu mwaka 2014 ambapo kwa mujibu wa Sheria Mwananchi anatakiwa kulipa fidia ya Eneo lake lililofanyiwa uthamini ndani miezi sita.


Alisema fedha hizo zitalipwa kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya kwanza zitalipwa kwa ucheleweshwaji wa miaka mitatu yaani 2015,16 na 17 huku awamu ya ya pili zikilipwa kwa ucheleweshwaji wa miaka miwili iliyosalia ya 2018 na 2019.


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo la Lindi , Hassan Kaunje licha ya kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ulipaji wa fidia kwa wananchi hao pia aliwapongeza wananchi wa Maeneo hayo kwa kuwa wavumilivu kwa wakati wote ambapo Serikali ikishughulika na Madai yao.


Nae Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga alisema kuwa ili kuhakikisha wananchi hao wanapata maeneo ya makaazi tayari halmashauri hiyo ya lindi imeshapima zaidi ya viwanja 500 kwa ajili ya kuanzisha makazi mapya ya wananchi wanaopisha mradi huo wa gesi asilia wa (LNG).
 

PICHA ZOTE NAHADIJA HASSAN.

No comments:

Post a Comment