Tuesday, October 8, 2024

WAJASIRIAMALI WANAWAKE BUKOBA WAPATIWA ELIMU.

 



Na Alodia Dominick, Bukoba


Wanawake wajasiriamali katika mji wa Bukoba wamepata elimu ya ujasiriamali, na kutakiwa kujiamini, kujithamini, kujiheshimu na kutojikweza.


Mafunzo hayo yametolewa na kampuni ya Stein Group inayojihusisha na shughuli za kijamii na  mafunzo hayo yamefanyika Octoba 06, 2024 katika manispaa ya Bukoba.


Meneja wa  Kampuni ya Stein Group mkoa wa Kagera Exavery Kyatwa ametaja lengo la kutoa mafunzo hayo kuwa ni kuwaelimisha wanawake wajasiriamali waliopo Manispaa ya Bukoba ili watoke hatua moja na  kwenda hatua nyingine kwa kujiendeleza kiuchumi.


Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo Taifa Mayamba Mbilinyi amesema, wameanza na wajasiriamali wa manispaa ya Bukoba yenye kata 14 na wajasiriamali wanawake wapatao 200 na baadaye wanatarajia kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 katika wilaya nyingine za mkoa wa Kagera kwa kutoa elimu ya ujasiriamali.


“Sisi tumelenga akina mama ili tuwajengee uwezo wa kujiamini katika kufanya biashara zenu, msiendelee kuwa tegemezi, na muache omba omba, baba akileta sukari mama ulete chunvi msaidiane katika familia” amesema Mbilinyi.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoa wa Kagera, Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) Ivona Bajumuzi amesema kuwa, wanahitaji wanawake wote wawezeshwe kiuchumi kwani mwanamke anapofanya biashara inamfanya ajiamini.


Ameeleza kuwa, wasiendelee kuitwa wajasiriamali wadogo wadogo wakue nao wawe wajasiriamali wa kati na wakubwa.


Akitoa mada ya wewe ni wa juu Grace Victor alisema mtaji mkubwa ni mtu mwenyewe kwani anavyo viungo vya mwili kama macho, masikio mikono na miguu vinavyomuwezesha kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.


“Wewe mwanamke kama unataka kuwa mjasiriamali lazima ujiamini, ujithamini, ujiheshimu na usijikweze na lazima uwaze kile unachotaka kukifanya kama kitazaa matunda” amesema Victor


Amesisitiza mwanamke anapopanga kufanya biashara asitazamie biashara ya wengine bali utashi utoke rohoni mwake kwamba anakwenda kufanya biashara fulani ili apate faida, na kuwa wanapoanza biashara wasikate tamaa wakomae nazo ili waone kama zitawapa faida au la.


Akitoa mada ya mama amka Anold Kikoyo amesema wanawake wanayo nguvu kubwa ya kufanya biashara na biashara zao zikakua nguvu hiyo ambayo ni uwezo wa kuatamia, hamasa, mlango wa sita wa fahamu, kujitolea katika jamii na uwezo wa kujadili hisia za wengine.


Kikoyo almewataka kuzingatia mahusiano sahihi, afya ya akili, kusimamia maamuzi ya ndoto zao bila kuangalia wengine wanasema nini, kuacha tabia ya kuahirisha mambo na vipaumbele vya matumizi sahihi ya muda.


Aidha kwa upande wake mtoa mada ya maswala ya uchumi Hamis Kashirima amewasihi wajasiriamali kuacha kuishi maisha feki na kuishi maisha halisi kutokana na kipato chao na wajiwekee malengo ya baadaye.


Amesema ili waweze kukua kiuchumi watengeneze mapato na matumizi ya kila mwezi katika familia zao, wajiwekee akiba na watakapoanzisha miradi wasitegemee chanzo kimoja cha mapato kwani kitakapo kwama kuendelea watakuwa wamerudi nyuma kiuchumi.      


Mada mbalimbali zizilizotolewa kwa wanawake hao ni pamoja na wewe ni wa juu, mama amka pamoja na mada ya maswala ya uchumi.

DC MWANZIVA NSSF: LINDI ONGEZENI KUTOA ELIMU KWA WANACHI UMUHIMU WA KUJIUNGA NA MFUKO NA FAIDA ZAKE

 





Na Hadija Omary, LINDI.


MKUU wa Wilaya ya Lindi Mkoani Humo Bi.Victoria Mwanziva  amewataka watumishi WA Mfuko wa hifazadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Lindi kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi wengi juu ya Umuhimu wa kujiunga na mfuko huo na faida zake


Mwanziva ametoa Rai hiyo oktoba 07/2024 wakati akizungumza na watumishi na wanachama wa Mfuko huo wa NSSF Mkoa wa Lindi Katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika huko manispaa ya Lindi .


Mwanziva Amesema wakati huu ambao Mfuko umeboresha mfumo wa sekta isiyo rasmi kwa wanachama waliojiajiri na kuandaa skimu maalumu kwa wafanyakazi walio Katika sekta rasmi ili kuweza kuchangia kwa hiari kupitia skimu hiyo ya (NISS NA SS)  pamoja na mambo mengine zinalenga kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya Jamii hivyo ni wajibu wao kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi .


Mifuko hii ya Watu kujichangia wenyewe ebu twendeni tukaongeze Elimu kwani tuna wananchi wengi Sana ambao wamejiajiri wafanyabiashara, wajasiriamali tuweke mpango kabambe Katika wiki hii ya huduma kwa wateja kuwafikia wengi na kuwaelimisha  namna ya kujichangia na faida za kujichangia .


Kwa kutumia wiki hii ya huduma kwa wateja wanaweza kuwavutia wananchi wengi ambao huwenda mpaka sasa bado hawafahamu faida za mifuko hii ya hifadhi ya Jamii kuanza kuchangia kwa  hiari .



Katika hatua nyingine Mwanziva pia aliwakumbusha wanachama  kuhakiki taarifa za michango wanapokuwa kazini ili kuepuka usumbufu wa kufuatilia michango wanapokuwa tayari kustaafu au nje ya ajira .


Kwa upande wake meneja wa NSSF Mkoa wa Lindi Juma Namuna Amesema Mfuko umekuwa unaweka mikakati ya kuongeza uandikishaji mwaka Hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023/2024 Mfuko huo uliweza kuandikisha wanachama wapya 291,266 huku mwaka 2024/2025 ukilenga kuandikisha wanachama wapya 324,321.


"Lakini pia kwa upande wa ukusanyaji wa michango tulikuwa tunalengo la kukusanya  Bilioni mbili Milioni miatisa na sitini na tatu  na tuliweza kukusanya Bilioni mbili milioni miatano na themanini na  saba sawasawa na ufanisi wa asilimia 87.30%"


Baadhi ya wanachama wa Mfuko huo wamesifu huduma wanazozipata kutoka Katika Mfuko na kuwasihi wananchi wenzao kujiunga ili waweze kupata manufaa.


Sunday, October 6, 2024

WAZEE WAASWA KUWA MBELE KATIKA KUHAMASISHA USHIRIKI WA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 




NA HADIJA OMARY, LINDI.


Wazee wa Nachingwea wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu 2024.


Wito huo  umetolewa na Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Nachingwea Robert Mmari alipokuwa akizungumza na wazee maarufu wa Wilaya hiyo ambapo amesisitiza   kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na msaada wa wazee utahakikisha zoezi linafanikiwa



Afisa Uchaguzi (W) ya Nachingwea ndugu Robert Mmari pia ameeleza kuwa sifa za mgombea na mpiga kura zimesha ainishwa, kwamba Mpiga kura lazima awe na akili timamu, awe na umri wa miaka 18 au zaidi, na awe mkazi wa kitongoji husika Wananchi wote wanatakiwa kupiga kura kwenye vitongoji walivyojiandikisha, huku zoezi la kuchukua fomu za kugombea likipangwa kuanza Novemba 1


Aidha, Msaidizi wa uchaguzi Joshua mnyang'ali Amesema kuwa kwa mwananchi  kushindwa kujiandikisha  kwa wakati uliopangwa, atapoteza haki ya kupiga kura 


Hata hivyo Alisisitiza kuwa Halmashauri imejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu uchaguzi na umuhimu wa kushiriki katika zoezi hilo


Kwa upande wake, Chief Nakotyo alibainisha kuwa kutakuwa na tukio maalum lenye ujumbe kuhusu maadili na hamasa ya uchaguzi litakalofanyika tarehe 7 na 8 Novemba na aliwataka wazee kuendelea kuhamasisha wananchi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mafanikio Vilevile, Joyce Chipanda, mkazi wa Kilimani Road, amewaasa wananchi kutopotosha wenzao na badala yake kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kulinda usalama na amani ya nchi


Thursday, October 3, 2024

BASHE AWAHAKIKISHIA WAKULIMA WA KOROSHO KUPATA BEI NZURI

 




NA HADIJA OMARY,  LINDI.

Waziri wa kilimo Hussain Bashe Amewahakikishia wakulima wa korosho kuwepo kwa bei nzuri ya zao Hilo Katika msimu wa mauzo 2024/2025 unaotarajiwa kuanza November 11 mwaka huu

Waziri Bashe ameyasema  hayo  November 02, 2024 akiwa Mkoani Lindi wakati anazungumza na Wadau wa kilimo ambapo Amesema kuwa kutokana  na mfumo rafiki unaotumika Katika uuzaji wa mazao wa Soko la Bidhaa (TMX) Hana Shaka kuwepo kwa bei zinazoridhisha Katika minada

" Tunaamini mwaka huu bei za korosho zitakuwa nzuri na kwa mara ya kwanza kwenye mfumo huu wa TMX tumeona makampuni ya kigeni ambayo yamejaribu kununua na zimepokea mzigo kama walivyotaka"

''Yaan wameshiriki wameiona katalog wameomba na kununua wakiwa huko huko nje na wameweza kupokea sasa maana yake   hamu imekuwa kubwa wanaweza kuuamini mfumo"

Hata hivyo Bashe ameviagiza Vyama vikuu vya ushirika Mkoa wa Lindi kufanya utambuzi wa maghara ya kuhifadhia korosho kabla ya msimu mpya wa mauzo ya zao Hilo kuanza rasm ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa korosho kwenye maghala 


"Nimewaagiza jukumu la usimamizi na uendeshaji wa maghala ni lakwao kwa sababu katalogi inatengenezwa na chama cha ushirika , sasa kama unatengeneza katalogi kwa nini kesho unapotokea upungufu Mimi siusiki?"

Amesema ili uingie mzigo hewa Katika ghala ni lazima uanzie kwenye chama cha msingi AMCOS ili kupata uthubitisho kutoka chama kikuu cha ushirika na mwendesha ghala hivyo ili kukabiliana na Hilo lazima vyamavikuu vikasimamia na endapo kutatokea udangajifu  wa Aina yoyote na wao watahusika 

MAAFISA KILIMO KATA KARAGWE WAPATIWA PIKIPIKI.

 


Na Alodia Dominick, Karagwe


Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera yenye maafisa kilimo wa kata wapatao 33 tayari wote wamepatiwa usafiri wa pikipiki kutoka Wizara ya kilimo ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ubora.


Maafisa kilimo hao wamepatiwa pikipiki kwa nyakati tofauti na Oktoba mosi, mwaka huu maafisa kilimo wapatao tisa ambao wameajiriwa hivi karibuni wamepatiwa pikipiki kama mwendelezo wa maafisa kilimo 24 ambao walitangulia kupata pikipiki hizo.


Akizungumza katika halfa hiyo ya makabidhiano Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Happiness Msanga ameishukuru serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kuendelea kuwakumbuka watumishi wa wilaya ya Karagwe hususani maafisa kilimo ngazi ya kata ambao shughuli zao kwa kiasi kikubwa zinategemea usafiri kutokana na ukubwa wa maeneo na umbali ili kuwafikia wananchi kwa wakati.


"Nichukue nafasi hii kuwasisitiza maofisa wote ambao mmekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kufanikisha kazi zenu mzitunze na kuzitumia kama ilivyokusudiwa, sitegemei kuona mnazitumia kufanya biashara ya usafirishaji (bodaboda) badala ya kufanya shughuli za kuwatumikia wananchi ambao ndio walengwa"


Pia amewakumbusha  kuwa, wahakikishe wanakuwa na leseni halali na wahudhurie mafunzo ya udreva kwa wale ambao hawajui kuzitumia ili pikipiki hizo zisiwe sababu ya ajali, na kuwa zitumike kwa matumizi salama na wazingatie sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zisizo za lazima


Aidha Afisa kilimo wilaya ya Karagwe Adamu Salum amezitaja kata hizo tisa ambazo maafisa kilimo wamekabidhiwa pikipiki kuwa ni kata ya Kanoni, Igurwa, Kihanga, Nyaishozi, Kituntu, Nyakahanga, Kayanga, Ihembe na Chonyonyo.


Naye afisa kilimo kata ya Kayanga  Fatuma Hashimu ambaye ni miongoni mwa waliopokea pikipiki hizo ameishukuru serikali kwa kuwapatia pikipiki ambazo zitawasaidia kuwafikia wakulima kwa haraka zaidi na kutatua changamoto zao kwa wakati.


Amesema awali walikuwa wanapata adha kuwafikia wakulima kutokana na changamoto ya usafiri na wakati mwingine wanashindwa kufika kwa wakati ili kuwahudumia lakini baada ya kupata usafiri huu wanatarajia kutoa huduma bora kwa wakulima na kuwafikia kwa wakati ukilinganisha na mwanzo ambapo hawakuwa na chombo cha usafiri.


Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wa umma katika kuongeza ufanisi na ubora katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

NACHINGWEA KUFANYA BONANZA LA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA

 

Na Mwandishi wetu, Lindi.


Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika November 27 mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi inatarajia kufanya bonanza la kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu Katika uchaguzi huo



Akizungumza na mwandishi wetu, kaimu mkurugenzi  halmashauri hiyo Joshua Mnyang'ali alisema kuwa bonanza hilo litafanya siku ya jumamosi 5/10/2024 katika uwanja wa majengo ambao michezo mingi itafanyika huku kukiwa na  wasanii mbalimbali wakipamba jukwaa la burudani kwa wakazi wa wilaya ya Nachingwea.


Amesema bonanza hilo linalenga kutoa elimu ya kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika wilaya ya Nachingwea, kuhamasisha maswala ya Amani pamoja na kuelezea shughuli mbalimbali za Maendeleo zilizofanywa na serikali


Mwenyekiti wa halmashauri ya Nachingwea Adinani mpyagila ametoa wito kwa wananchi wa Nachingwea pamoja na wa Maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki bonanza Hilo kubwa 



Sunday, September 29, 2024

TUKAJIANDIKISHE KWENYE DAFTARI LA MKAZI ILI TUPIGE KURA. RC LINDI

 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la Mkazi ambalo linatarajiwa kufanyika Oktoba 11 hadi 20, 2024 na upigaji wa kura 27, Novemba 2024 kuchagua viongozi wa serikali za Mitaa.


"Niwaombe vijana wote, niwaombe akina mama, akina Baba tuende tukajiandikishe kwenye daftari la mkazi ili tukaweze kupiga kura " 


Wito huo ameutoa leo tarehe 29 septemba 2024  katika viwanja vya Kilwa Kivinje ambako kivinje Jogging klabu wameandaa bonanza lakualika klabu mbalimbali kutoka maeneo na mikoa mbalimbali kama vile Dodoma, Mtwara, Pwani na Dar Es Salaam lenye lengo la kudumisha afya, ushirikiano, upendo, umoja na hamasa ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba 27, 2024.


Mhe. Zainabu Telack ametoa angalizo kwa wananchi ambao hawana taarifa sahihi kuhusu vitambulisho walivbyo navyo na zoezi la kujiandikisha katika daftari la mkazi.


"Wapo wenzetu ambao wanasema tayari wanavitambulisho vya kupiga kura  vitambulisho  kwahiyo hawaoni sababu ya kujiandikisha tena , vile vitambulisho ni kwa ajili ya uchaguzi wa Mwaka kesho lakini kwa uchaguzi huu wa serikali za mitaa, serikali zamitaa ,vijiji na vitongoji tunakwenda kujiandikisha kwenye daftari la mkazi " 


Aidha, amewasihii siku ya kupiga kura wajitokeze mapema kwa ajili ya kutimiza wajibu nahaki ya kupiga kura mapema.


Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary amesema kilammojaazishike tarehe hizo muhimu ambazo tarehe 11 hadi 20 Oktoba , 2024 kwa ajili ya kujiandikisha na tarehe 27 siku ya kupiga kura .






RAIS DKT. SAMIA AHITIMISHA ZIARA YA SIKU SITA RUVUMA.

 

Awashukuru wananchi ushirikiano wao, ajivunia mafanikio makubwa utekelezaji wa Ilani ya CCM.


Asisitiza wananchi kujiandikisha Uchaguzi Serikaki za Mitaa.







Mhe. Rais Dkt. Samia amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi takriban elfu 50, katika Uwanja wa kihistoria, wa Kumbukumbu ya Majimaji, mjini Songea,  tarehe 28 Septemba 2024.


Katika hotuba yake mbele ya umati mkubwa wa watu waliofurika kumsikiliza Rais Dkt. Samia, pamoja na masuala mengine, ameendelea kusisitiza wito wake kwa Watanzania wenye sifa kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuanzia ratiba ya kujiandikisha kupiga kura iliyopangwa kuanza Oktoba 11 - 20, mwaka huu. 


Rais Dkt. Samia ametumia mkutano huo pia, kuendelea kuwashukuru Watanzania wanavyoshirikiana na Serikali ya CCM, chini ya uongozi wake, hali ambayo imesaidia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, kwa mafanikio makubwa hadi sasa, katika nyanja mbalimbali za maendeleo. 


Katika ziara hiyo, ambayo imemfikisha katika wilaya na halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma, akianzia Songea, kisha Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru, Mhe. Rais Dkt. Samia amekutana, kuwasikiliza na kuzungumza na wananchi kuhusu maendeleo na hali za maisha katika maeneo yao, huku changamoto zilizowasilishwa akizitolea maagizo ya ufumbuzi wa haraka, wa kudumu, na zingine akizichukua kwa hatua zaidi. 


Aidha, katika kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Dkt. Samia akielezea kisekta, amebainisha shughuli zote alizofanya ndani ya Mkoa wa Ruvuma, ikiwemo kilimo, maji, elimu, afya, miundombinu ya barabara na bandari, sanaa, mazingira, utamaduni na utalii.


Thursday, September 26, 2024

HAKIMU, WAKILI WA SERIKALI WAJA JUU WAKILI CHUWA KUCHELEWESHA KESI.

 



Na Mwandishi Wetu


HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aaron Lyamuya, ameelezea kukerwa na tabia ya wakili wa utetezi kwenye kesi ya jinai, Edward Chuwa kutaka kesi iahirishwe mara kwa mara.


"Hivi siyo vitu vya kutengeneza vipo kwenye rekodi za mahakama, hili shauri lazima liishe hatuwezi kuja hapa kila siku tunakaa tu hatuna cha kufanya hapa,  kuna polisi, kuna karani na mawakili wapo tu kila siku kuahirisha kesi hapana, “ alisema Lyamuya


Kesi hiyo ya tuhuma za kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inawakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54)  ambapo nathwani anatuhumiwa kuwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.


Hakimu Lyamuya alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba analipwa kwa hiyo anatakiwa kufanya kazi na pia Wakili wa Serikali analipwa anatakiwa afanye kazi.


"Sio kwamba nilikuwa sioni hii hali hapana nilikuwa naona udhuru unaotolewa mara kwa mara ila niliamua kuwa mvumilivu tu, lakini haiwezekani Chuwa acheleweshe shauri hili kila siku haliwezekani  hii kesi iendelee milele inatakiwa ifike mwisho,"alisema Hakimu Lyamuya


Aliwataka washtakiwa wamueleze wakili wao kilichoendelea mahakamani na wamwambie aje mahakamani shauri lisikilizwe ili maisha mengine yaendelee.


 Hakimu Lyamuya alipangia shauri hilo Oktoba 7, 2024 kwa ajili ya kusikiliza, ambapo shahidi alionywa afike tarehe hiyo.


Awali, wakili wa Serikali Faraja Ngukah aliiilalamikia mahakama hiyo kuwa Wakili wa utetezi  Edward Chuwa amekuwa na tabia ya kuchelewesha shauri hilo kwa kutoa udhuru kila wakati.


Aidha, wakili huyo amelalamikia kitendo cha mshtakiwa wa pili Sangita kudai anaumwa na shauri likaahirishwa lilipokuja hivi karibuni, lakini cha kushangaza alikwenda kukesha kwenye sherehe za tamaduni za kihindi.


Ngukah alidai kuwa usikilizwaji wa shauri hilo umeahirishwa mara saba kwa udhuru wa Wakili Chuwa ingawa  Mahakama ilimuachia nafasi apange tarehe ya kusikilizwa kesi.


“Haiwezekani shauri hili likawa linaahirishwa mara kwa mara  kwasababu ya wakili Chuwa, na yeye ndiye alipendekeza tarehe ya leo iweje tena aseme kwamba aka kesi nyingine leo wakati yeye ndiye alipanga tarehe ya leo,” alidai


Alidai kuwa katika vikao hivyo vitatu ni cha Agosti 30, 2024, Septemba 10, 2024 na kikao cha jana cha Septemba 26, 2024 vikao vyote hivyo walipata hudhuru kutoka kwa Wakili Chuwa.


Alidai kuwa tarehe 30  Chuwa alidai kuwa yuko Mahakama Kuu kwenye usikilizwaji wa shauri na Septemba 10, 2024 alieleza Mahakama kuwa hawawezi kuendelea kwa sababu mteja wake wa pili anaumwa ingawa anayedaiwa kuwa mgonjwa alionekana akiendelea na shughuli zake mitaani.


Wakili Ngukah alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa Sangita alikesha kwenye sherehe na pia hata alipoondoka eneo la Mahakama aliendelea na shughuli zake za kijamii na hakuwa anaumwa kama alivyodai wakili wake na badala yake walipanga shauri liendelee.


"Mlalamikaji na washtakiwa wanaishi eneo moja, kwa hiyo anaweza kuona kitu na kukisema, Mheshimiwa Hakimu haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa hili shauri linachukua muda mrefu sana lazimaa lifike mwisho,"alidai Ngukah


“Shauri hili  lilitakiwa kuanza kusikilizwa saa tatu asubuhi, kwa hiyo tulitarajia angefika mahakamani hapa mapema tukaanza na hili kwa sababu shauri la Mahakama Kuu linaanza kusikilizwa saa tano asubuhi,” alidai.


"Wakati kesi hii inaendelea Wakili Chuwa huwa anakuja na wakili Anna Lugendo, lakini cha kushangaza ikitokea ana udhuru Lugendo naye haji mahakamani,"


"Tunaomba Mahakama itoe amri iwapo itapanga tarehe ya kusikilizwa, basi siku hiyo upande wa utetezi uwepo kama kutakuwa udhuru yoyote basi aje wakili mwingine na shauri liendelee, tunaelekea mwaka sasa lilifika hapa Agosti 18,2023  na hadi sasa ni mashahidi wanne tu waliotoa ushahidi,"alidai Ngukah


Ngukah alisema kuwa jana walikuwa na shahidi mmoja ambaye ni mara yake ya tatu kufika  mahakamani lakini hakupata nafasi ya kusikilizwa na kuongeza kuwa hatendewi haki kwa sababu anaacha shughuli zake za kijamii kuja mahakamani.


"Siku shashidi huyu akichoka kufika mahakamani sisi upande wa Jamhuri ndiyo itakuwa imekula kwetu, hatumtendei haki tunaomba wakili wa utetezi Edward Chuwa aonywe,"alidai Ngukah


Hakimu Lyamuya aliwauliza washtakiwa kama wamesikia malalamiko ya wakili wa serikali kuhusu wakili wao Chuwa kutokufika mahakamani na walijibu kuwa wamesikia

RAIS SAMIA AFUNGUA BARABARA YA MBINGA - MBAMBA BAY (KM 66) - RUVUMA




 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua barabara  ya Mbinga - Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Ruvuma, Septemba 25, 2024.


Ujenzi wa Barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) umesimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara - TANROADS chini ya Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd kutoka China na Mhandisi Mshauri kutoka SMEC International Pty Ltd kutoka Australia kwa gharama ya Shilingi Bilioni 122.76.


Katika utekelezaji wa barabara hiyo, Kiasi cha shilingi Milioni 637.4 kilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi kwa mujibu wa sheria.


Barabara ya Mbinga - Mbamba Bay ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) yenye jumla ya urefu wa kilometa 826 inayoanzia Mtwara mpaka Mbamba Bay ambapo pia barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkoa wa Mbeya na nchi Jirani ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa.