Thursday, September 26, 2024

HAKIMU, WAKILI WA SERIKALI WAJA JUU WAKILI CHUWA KUCHELEWESHA KESI.

 



Na Mwandishi Wetu


HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aaron Lyamuya, ameelezea kukerwa na tabia ya wakili wa utetezi kwenye kesi ya jinai, Edward Chuwa kutaka kesi iahirishwe mara kwa mara.


"Hivi siyo vitu vya kutengeneza vipo kwenye rekodi za mahakama, hili shauri lazima liishe hatuwezi kuja hapa kila siku tunakaa tu hatuna cha kufanya hapa,  kuna polisi, kuna karani na mawakili wapo tu kila siku kuahirisha kesi hapana, “ alisema Lyamuya


Kesi hiyo ya tuhuma za kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inawakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54)  ambapo nathwani anatuhumiwa kuwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.


Hakimu Lyamuya alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba analipwa kwa hiyo anatakiwa kufanya kazi na pia Wakili wa Serikali analipwa anatakiwa afanye kazi.


"Sio kwamba nilikuwa sioni hii hali hapana nilikuwa naona udhuru unaotolewa mara kwa mara ila niliamua kuwa mvumilivu tu, lakini haiwezekani Chuwa acheleweshe shauri hili kila siku haliwezekani  hii kesi iendelee milele inatakiwa ifike mwisho,"alisema Hakimu Lyamuya


Aliwataka washtakiwa wamueleze wakili wao kilichoendelea mahakamani na wamwambie aje mahakamani shauri lisikilizwe ili maisha mengine yaendelee.


 Hakimu Lyamuya alipangia shauri hilo Oktoba 7, 2024 kwa ajili ya kusikiliza, ambapo shahidi alionywa afike tarehe hiyo.


Awali, wakili wa Serikali Faraja Ngukah aliiilalamikia mahakama hiyo kuwa Wakili wa utetezi  Edward Chuwa amekuwa na tabia ya kuchelewesha shauri hilo kwa kutoa udhuru kila wakati.


Aidha, wakili huyo amelalamikia kitendo cha mshtakiwa wa pili Sangita kudai anaumwa na shauri likaahirishwa lilipokuja hivi karibuni, lakini cha kushangaza alikwenda kukesha kwenye sherehe za tamaduni za kihindi.


Ngukah alidai kuwa usikilizwaji wa shauri hilo umeahirishwa mara saba kwa udhuru wa Wakili Chuwa ingawa  Mahakama ilimuachia nafasi apange tarehe ya kusikilizwa kesi.


“Haiwezekani shauri hili likawa linaahirishwa mara kwa mara  kwasababu ya wakili Chuwa, na yeye ndiye alipendekeza tarehe ya leo iweje tena aseme kwamba aka kesi nyingine leo wakati yeye ndiye alipanga tarehe ya leo,” alidai


Alidai kuwa katika vikao hivyo vitatu ni cha Agosti 30, 2024, Septemba 10, 2024 na kikao cha jana cha Septemba 26, 2024 vikao vyote hivyo walipata hudhuru kutoka kwa Wakili Chuwa.


Alidai kuwa tarehe 30  Chuwa alidai kuwa yuko Mahakama Kuu kwenye usikilizwaji wa shauri na Septemba 10, 2024 alieleza Mahakama kuwa hawawezi kuendelea kwa sababu mteja wake wa pili anaumwa ingawa anayedaiwa kuwa mgonjwa alionekana akiendelea na shughuli zake mitaani.


Wakili Ngukah alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa Sangita alikesha kwenye sherehe na pia hata alipoondoka eneo la Mahakama aliendelea na shughuli zake za kijamii na hakuwa anaumwa kama alivyodai wakili wake na badala yake walipanga shauri liendelee.


"Mlalamikaji na washtakiwa wanaishi eneo moja, kwa hiyo anaweza kuona kitu na kukisema, Mheshimiwa Hakimu haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa hili shauri linachukua muda mrefu sana lazimaa lifike mwisho,"alidai Ngukah


“Shauri hili  lilitakiwa kuanza kusikilizwa saa tatu asubuhi, kwa hiyo tulitarajia angefika mahakamani hapa mapema tukaanza na hili kwa sababu shauri la Mahakama Kuu linaanza kusikilizwa saa tano asubuhi,” alidai.


"Wakati kesi hii inaendelea Wakili Chuwa huwa anakuja na wakili Anna Lugendo, lakini cha kushangaza ikitokea ana udhuru Lugendo naye haji mahakamani,"


"Tunaomba Mahakama itoe amri iwapo itapanga tarehe ya kusikilizwa, basi siku hiyo upande wa utetezi uwepo kama kutakuwa udhuru yoyote basi aje wakili mwingine na shauri liendelee, tunaelekea mwaka sasa lilifika hapa Agosti 18,2023  na hadi sasa ni mashahidi wanne tu waliotoa ushahidi,"alidai Ngukah


Ngukah alisema kuwa jana walikuwa na shahidi mmoja ambaye ni mara yake ya tatu kufika  mahakamani lakini hakupata nafasi ya kusikilizwa na kuongeza kuwa hatendewi haki kwa sababu anaacha shughuli zake za kijamii kuja mahakamani.


"Siku shashidi huyu akichoka kufika mahakamani sisi upande wa Jamhuri ndiyo itakuwa imekula kwetu, hatumtendei haki tunaomba wakili wa utetezi Edward Chuwa aonywe,"alidai Ngukah


Hakimu Lyamuya aliwauliza washtakiwa kama wamesikia malalamiko ya wakili wa serikali kuhusu wakili wao Chuwa kutokufika mahakamani na walijibu kuwa wamesikia

No comments:

Post a Comment