Na Alodia Dominick, Karagwe
Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera yenye maafisa kilimo wa kata wapatao 33 tayari wote wamepatiwa usafiri wa pikipiki kutoka Wizara ya kilimo ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ubora.
Maafisa kilimo hao wamepatiwa pikipiki kwa nyakati tofauti na Oktoba mosi, mwaka huu maafisa kilimo wapatao tisa ambao wameajiriwa hivi karibuni wamepatiwa pikipiki kama mwendelezo wa maafisa kilimo 24 ambao walitangulia kupata pikipiki hizo.
Akizungumza katika halfa hiyo ya makabidhiano Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Happiness Msanga ameishukuru serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kuendelea kuwakumbuka watumishi wa wilaya ya Karagwe hususani maafisa kilimo ngazi ya kata ambao shughuli zao kwa kiasi kikubwa zinategemea usafiri kutokana na ukubwa wa maeneo na umbali ili kuwafikia wananchi kwa wakati.
"Nichukue nafasi hii kuwasisitiza maofisa wote ambao mmekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kufanikisha kazi zenu mzitunze na kuzitumia kama ilivyokusudiwa, sitegemei kuona mnazitumia kufanya biashara ya usafirishaji (bodaboda) badala ya kufanya shughuli za kuwatumikia wananchi ambao ndio walengwa"
Pia amewakumbusha kuwa, wahakikishe wanakuwa na leseni halali na wahudhurie mafunzo ya udreva kwa wale ambao hawajui kuzitumia ili pikipiki hizo zisiwe sababu ya ajali, na kuwa zitumike kwa matumizi salama na wazingatie sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zisizo za lazima
Aidha Afisa kilimo wilaya ya Karagwe Adamu Salum amezitaja kata hizo tisa ambazo maafisa kilimo wamekabidhiwa pikipiki kuwa ni kata ya Kanoni, Igurwa, Kihanga, Nyaishozi, Kituntu, Nyakahanga, Kayanga, Ihembe na Chonyonyo.
Naye afisa kilimo kata ya Kayanga Fatuma Hashimu ambaye ni miongoni mwa waliopokea pikipiki hizo ameishukuru serikali kwa kuwapatia pikipiki ambazo zitawasaidia kuwafikia wakulima kwa haraka zaidi na kutatua changamoto zao kwa wakati.
Amesema awali walikuwa wanapata adha kuwafikia wakulima kutokana na changamoto ya usafiri na wakati mwingine wanashindwa kufika kwa wakati ili kuwahudumia lakini baada ya kupata usafiri huu wanatarajia kutoa huduma bora kwa wakulima na kuwafikia kwa wakati ukilinganisha na mwanzo ambapo hawakuwa na chombo cha usafiri.
Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wa umma katika kuongeza ufanisi na ubora katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.
No comments:
Post a Comment