Tuesday, October 8, 2024

WAJASIRIAMALI WANAWAKE BUKOBA WAPATIWA ELIMU.

 



Na Alodia Dominick, Bukoba


Wanawake wajasiriamali katika mji wa Bukoba wamepata elimu ya ujasiriamali, na kutakiwa kujiamini, kujithamini, kujiheshimu na kutojikweza.


Mafunzo hayo yametolewa na kampuni ya Stein Group inayojihusisha na shughuli za kijamii na  mafunzo hayo yamefanyika Octoba 06, 2024 katika manispaa ya Bukoba.


Meneja wa  Kampuni ya Stein Group mkoa wa Kagera Exavery Kyatwa ametaja lengo la kutoa mafunzo hayo kuwa ni kuwaelimisha wanawake wajasiriamali waliopo Manispaa ya Bukoba ili watoke hatua moja na  kwenda hatua nyingine kwa kujiendeleza kiuchumi.


Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo Taifa Mayamba Mbilinyi amesema, wameanza na wajasiriamali wa manispaa ya Bukoba yenye kata 14 na wajasiriamali wanawake wapatao 200 na baadaye wanatarajia kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 katika wilaya nyingine za mkoa wa Kagera kwa kutoa elimu ya ujasiriamali.


“Sisi tumelenga akina mama ili tuwajengee uwezo wa kujiamini katika kufanya biashara zenu, msiendelee kuwa tegemezi, na muache omba omba, baba akileta sukari mama ulete chunvi msaidiane katika familia” amesema Mbilinyi.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoa wa Kagera, Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) Ivona Bajumuzi amesema kuwa, wanahitaji wanawake wote wawezeshwe kiuchumi kwani mwanamke anapofanya biashara inamfanya ajiamini.


Ameeleza kuwa, wasiendelee kuitwa wajasiriamali wadogo wadogo wakue nao wawe wajasiriamali wa kati na wakubwa.


Akitoa mada ya wewe ni wa juu Grace Victor alisema mtaji mkubwa ni mtu mwenyewe kwani anavyo viungo vya mwili kama macho, masikio mikono na miguu vinavyomuwezesha kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.


“Wewe mwanamke kama unataka kuwa mjasiriamali lazima ujiamini, ujithamini, ujiheshimu na usijikweze na lazima uwaze kile unachotaka kukifanya kama kitazaa matunda” amesema Victor


Amesisitiza mwanamke anapopanga kufanya biashara asitazamie biashara ya wengine bali utashi utoke rohoni mwake kwamba anakwenda kufanya biashara fulani ili apate faida, na kuwa wanapoanza biashara wasikate tamaa wakomae nazo ili waone kama zitawapa faida au la.


Akitoa mada ya mama amka Anold Kikoyo amesema wanawake wanayo nguvu kubwa ya kufanya biashara na biashara zao zikakua nguvu hiyo ambayo ni uwezo wa kuatamia, hamasa, mlango wa sita wa fahamu, kujitolea katika jamii na uwezo wa kujadili hisia za wengine.


Kikoyo almewataka kuzingatia mahusiano sahihi, afya ya akili, kusimamia maamuzi ya ndoto zao bila kuangalia wengine wanasema nini, kuacha tabia ya kuahirisha mambo na vipaumbele vya matumizi sahihi ya muda.


Aidha kwa upande wake mtoa mada ya maswala ya uchumi Hamis Kashirima amewasihi wajasiriamali kuacha kuishi maisha feki na kuishi maisha halisi kutokana na kipato chao na wajiwekee malengo ya baadaye.


Amesema ili waweze kukua kiuchumi watengeneze mapato na matumizi ya kila mwezi katika familia zao, wajiwekee akiba na watakapoanzisha miradi wasitegemee chanzo kimoja cha mapato kwani kitakapo kwama kuendelea watakuwa wamerudi nyuma kiuchumi.      


Mada mbalimbali zizilizotolewa kwa wanawake hao ni pamoja na wewe ni wa juu, mama amka pamoja na mada ya maswala ya uchumi.

No comments:

Post a Comment