Sunday, September 29, 2024

RAIS DKT. SAMIA AHITIMISHA ZIARA YA SIKU SITA RUVUMA.

 

Awashukuru wananchi ushirikiano wao, ajivunia mafanikio makubwa utekelezaji wa Ilani ya CCM.


Asisitiza wananchi kujiandikisha Uchaguzi Serikaki za Mitaa.







Mhe. Rais Dkt. Samia amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi takriban elfu 50, katika Uwanja wa kihistoria, wa Kumbukumbu ya Majimaji, mjini Songea,  tarehe 28 Septemba 2024.


Katika hotuba yake mbele ya umati mkubwa wa watu waliofurika kumsikiliza Rais Dkt. Samia, pamoja na masuala mengine, ameendelea kusisitiza wito wake kwa Watanzania wenye sifa kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuanzia ratiba ya kujiandikisha kupiga kura iliyopangwa kuanza Oktoba 11 - 20, mwaka huu. 


Rais Dkt. Samia ametumia mkutano huo pia, kuendelea kuwashukuru Watanzania wanavyoshirikiana na Serikali ya CCM, chini ya uongozi wake, hali ambayo imesaidia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, kwa mafanikio makubwa hadi sasa, katika nyanja mbalimbali za maendeleo. 


Katika ziara hiyo, ambayo imemfikisha katika wilaya na halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma, akianzia Songea, kisha Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru, Mhe. Rais Dkt. Samia amekutana, kuwasikiliza na kuzungumza na wananchi kuhusu maendeleo na hali za maisha katika maeneo yao, huku changamoto zilizowasilishwa akizitolea maagizo ya ufumbuzi wa haraka, wa kudumu, na zingine akizichukua kwa hatua zaidi. 


Aidha, katika kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Dkt. Samia akielezea kisekta, amebainisha shughuli zote alizofanya ndani ya Mkoa wa Ruvuma, ikiwemo kilimo, maji, elimu, afya, miundombinu ya barabara na bandari, sanaa, mazingira, utamaduni na utalii.


No comments:

Post a Comment