Monday, November 27, 2017

MAHAFALI YA TISA YEMEN SECONDARY SCHOOL 2017.


Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya shule za Yemen Hassan Akrabi, katikati ni Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Baraza la wakuu wa shule za Kiislamu Tanzania, Ansaar Abubakar Kachwamba na kulia ni Mkuu wa shule ya Sekondari Yemen, mwalimu Hamisi Togwa. 

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Baraza la wakuu wa shule za Kiislamu Tanzania, Ansaar Abubakar Kachwamba akizungumza katika mahafali hayo ya tisa yaliyofanika viwanja vya shule za Yemen Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
 ...............................

Vijana wanaohitimu katika shule za kiislamu hapa nchini wametakiwa kuendeleza maadili mema waliyopata katika shule hizo ili kuujengea heshima uislamu.

Akizungumza katika mahafali ya tisa ya shule ya sekondari Yemen, Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Ansar Abubakar Kachwamba alisema jamii imejenga imani kubwa kwa shule za kiislamu na waislamu kwa ujumla hivyo ni jukumu la vijana wanaohitimu katika shule za kiislamu kuilinda heshima hiyo mbele ya jamii.

Ansaar Kachwamba, ambae ni Mwenyekiti wa Baraza la wakuu wa shule za kiislamu hapa nchini alisema maadili mema yametoweka katika jamii hivyo shule za kiislamu ambazo miongoni mwa  majukumu yao ni kusimamia maadili kwa vijana zinapaswa kuungwa mkono na kila mtu na kwamba vijana wanaohitimu katika shule hizo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kudumu katika maadili mema.

Aidha, aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu ili kujenga timu moja inayoweza kusimamia taaluma na maadili kwa vijana na kwamba kazi hiyo wasiachiwe walimu peke yao.

Alisema kazi ya kukuza taaluma na kusimamia maadili sio ya walimu peke yao bali ni ushirikiano kati ya mzazi, mwalimu, mtoto pamoja na jamii kwa ujumla kwakuwa faida ya kuwa na maadili mema ni ya Taifa kwa ujumla na sio ya mtu moja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen, Hassan Akrabi aliwataka wazazi kuhakikisha wnalipa ada kwa wakati ili kuiwezesha shule kupiga hatua katika mambo na mikakati mbalimbali waliojiwekea ikiwemo kukuza taaluma shuleni hapo.

Alisema mikakati nayopangwa na shule haiwezxi kufanikiwa ikiwa wazazi hawatoi ushirikiano haswa katika swala la ulipaji wa ada.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa shule hiyo Hamisi Togwa alisema shule hiyo ni miongoni mwa shule wastani wa kati  hapa nchini na kwamba imeendelea kufanya vizuri kitaaluma tangu kuanzishwa kwake.

Alisema shule hiyo imefanikiwa katika kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne huku ikihuisha na kuendeleza darsa la Qur ani pamoja kukuza elimu ya kiarabu.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili shule hiyo, mwalimu Togwa alisema ni pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji hali inayopelekea kupanda kwa ada ili kukabiliana gharama za uendeshaji.

Aidha, alisema mikakati ya shule hiyo ni kuhakikisha inaongeza ufaulu kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu na kuondoa au kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne na sifuri.

Jumla ya wanafunzi 91 wamehitimu elimu ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Yemen mwaka huu wa 2017  ambao kati yao wavulana 45 na wasichana ni 46 . 
Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya shule za Yemen Hassan Akrabi, akizungumza katika mahafali hayo.
Meneja wa shule za Yemen, Jamila Awadhi, akizungumza katika mahafali hayo.
Baadhi ya wanafunzi waliomaliza katika shule hiyo ya Yemen ambao kwa sasa wanasoma katika vyuo vikuu mbalimbali walipojumuika na wadogo zao katika mahafali hayo.
Kiongozi wa wanafunzi waliomaliza shuleni hapo miaka ya nyuma ambao kwa sasa wanasoma katika vyuo vikuu, Salim Saidi Salim akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa kidato cha nne 2017 katka mahafali hayo yaliyofanyika viwanja vya za Yemen Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa kidato cha nne shule ya Sekondari yemen jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye mahafali yao.