Thursday, November 30, 2023

MAAMBUKIZI YA MALARIA KAGERA YAFIKIA ASILIMIA 18.

 

Na Alodia Babara 

Bukoba. 

Misimu miwili ya mvua ya vuli na masika inayonyesha mkoani Kagera imetajwa kama sababu ya mbu kuzaliana na hivyo kusababisha kiwango cha maambukizi ya malaria kufikia asilimia 18,  mkoani humo huku kiwango cha taifa kikitajwa kuwa ni asilimia 8.

Kufuatia kiwango hicho kuwa juu, wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa ambazo ziko pembezoni na vijiji viko umbali wa kuanzia kilomita tano kufika katika vituo vya afya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 38 wamepewa vifaa tiba.

Akizungumza leo Novemba 30,2023 katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya kutolea huduma za tiba katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo mkurugenzi wa mradi wa Shinda malaria Dk Dunstan Bishanga amesema wahudumu hao walipewa mafunzo ya awali jinsi ya kupima joto na kuwaelimisha wanachi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua.

“Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa mitatu hapa nchini yenye maambukizi ya juu ya malaria ambapo watu 18 kati ya watu 100 wameathirika na vimelia vya ugonjwa huo, pamoja na jitihada zote tunashukuru kuna upungufu wa visa hivyo, kwani mwaka 2019 Kagera ilikuwa na visa vya malaria 580,000 na mwaka 2022 visa hivyo vimepungua hadi 250,000”amesema Dk Bishanga

Dk Bishanga ameongeza kuwa, kiwango cha malaria mkoani hapa kimekuwa kikipanda juu zaidi katika vipindi viwili vya msimu wa mvua ambavyo ni vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba na msimu wa masika kuanzia Machi hadi Mei.

 Kwa upande wake mkurugenzi wa IHI taasisi ya afya ya Ifakara Honorath Masanja amesema kuwa, vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 60, vimegaiwa kwa wahudumu hao na vifaa hivyo ni vipima joto, buti, baiskeli, makoti ya mvua, mizani na kifaa cha kubebea vifaa (kit).

Katibu tawala mkoa wa Kagera Toba Nguvila akiwa amemwakilisha mkuu wa mkoa huo amesisitiza viongozi wa ngazi zote kuwa wanapaswa kushirikiana kupiga vita ugonjwa wa maralia kwani yeye kama kiongozi wa mkoa hajisikii vizuri kuona watu wake wanaugua maralia na kuwa jamii ielimishwe maatumizi ya vyandarua na mazalia ya mbu yateketezwe.

Jastini Jakson kutoka wilaya ya Kyerwa ni mmoja wa wahudumu ngazi ya jamii waliopokea vifaa hivyo amesema kuwa, walipatiwa mafunzo jinsi ya kumtambua mgonjwa wa maralia kwa kumhoji kwanza na baadaye kumpima joto la mwili.

Amesema kuwa, kutokana na mafunzo waliyopewa walifundishwa kuwa, baada ya kuona mgonjwa ana homa kali, anawangwa kichwa na anatapika wanapaswa kuchukua jukumu la kumpa rufaa kwenda kituo cha afya na wamejifunza utunzaji wa kumbukumbu na kutunza siri za mgonjwa. 

Wednesday, November 15, 2023

EDU KWANZA WATOA FURSA YA MASOMO KWA VYUO VIKUU VYA CANADA & USA KWA WANAFUNZI WA TANZANIA

 

Na Andrew Chale, Dar es Salaam.


EDUKWANZA Consultants Limited ambao ni Mawakala wa Vyuo vya nje ya Nchi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya ushauri huduma za Wanafunzi ya ILLUME imeendesha zoezi kwa Wanafunzi wa Tanzania kupata fursa za masomo katika Vyuo vya nchi za Canada na Marekani (USA) tukio lililofanyika Jijini Dar es Salaam mapema leo Novemba 15,2023.


Akizungumza katika tukio hilo lililowakutanisha wanafunzi mbalimbali waliofika kupata muongozo sahihi wa Vyuo vya nje, Mkurugenzi wa Edukwanza, Bw. Sarfraz Kassam amesema taasisi yao hiyo ina ushirikiano na Vyuo zaidi ya 500 Duniani ikiwemo Vyuo hivyo vya Canada na Marekani.


"Edukwanza Consultants Limited leo Novemba 15,2023 tumefanya maonesho ya kuvinadi Vyuo vya Canada na Marekani katika mpango wa ‘Study in Canada & USA Fair 2023 ambao unasaidia kutoa fursa kwa in wanafunzi kusoma nje.


Wanafunzi mbalimbali wa Tanzania wamefika na kupata ushauri kutoka kwa Wawakilishi wa vyuo hivyo vya nje, wakipata ushauri wa kujiunga na vyuo hivyo, namna ya kupata visa za masomo, ama namna ya masomo ya kuchagua na muongozo mwingine kwa ajili ya taaluma yao." Amesema Sarfraz Kassam

 





Aidha, amesema kuwa, Vyuo hivyo vya Canada na Marekani ni miongoni mwa vyuo bora na wanafunzi wamepata namna bora ya kupata ushauri wa jinsi ya kuomba kusoma kwenye vyuo hivyo.


Lakini pia amewataka wanafunzi hao kuweza kupitia mitandao ya kijamii ya Edukwanza kupata muongozo sahihi kwa ajili ya hatma yao ya kuchagua Vyuo bora nje ya Nchi.


Edukwanza ni miongoni mwa Mawakala wa Vyuo vya nje ya Nchi iliyosajiliwa na Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU) imekuwa kinara katika kunadi na kuongoza kushauri wanafunzi kwenda kusoma nje.


UNESCO, WADAU WAKUTANA DAR KUJADILI UKATILI NA UNYANYASAJI KWA WENYEULEMAVU VYUO VYA UFUNDI NCHINI

 

Na Andrew Chale, Dar es Salaam.


SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limekutana na Wadau Wataalam kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali, Serikali na Mashirika ya watu wenye Ulemavu kupitia na kutolea maoni nyenzo za kukabiliana na vitendo vya kikatili na kinyanyasaji kwa wanafunzi walemavu wanaosoma Vyuo vya ufundi hapa nchini.


Mkutano huo wa siku mbili yaani Novemba 14- 15,2023 mbali ya Tanzania, pia unafanyika sambamba katika nchi zingine tatu za Namibia, Msumbiji na Zimbabwe kwa pamoja wakijadiliana kupitia video kwa mtandao wa ZOOM.

 

Mkutano huo ni mpango unaotekelezwa na UNESCO na Shirika la Kazi Duniani (ILO)kupitia mradi unaofadhiliwa na United Nations Partnership on the Rights of Persons with Disabilities (UNPRPD) wenye lengo la kukomesha unyanyapaa na ubaguzi wa watu wenye ulemavu katika vyuo vya ufundi na kazini. 


Katika majadiliano hayo, Wadau wameweza kutoa maoni yao na namna bora ya hatua za kuchukuliwa ilikufikiwa malengo, huku pia wakijifunza kutoka kwa wenzao wanchi za Msumbiji, Zimbabwe na Namibia.


Katika mazungumzo ambayo mengine yamefanyika kwa njia ya video.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya ameyashukuru Shirika la Kimataifa la UNESCO na ILO kwa mkutano huo wa wadau namna bora ya kukabiliana na vitendo vya kikatili ambavyo vinaendelea katika Vyuo vya Ufundi vya Tanzania.


Ambapo amesema mkutano huo ni muhimu kwani tayari kuna nyenzo zimeandaliwa ambazo zitasaidia kupata taarifa mbalimbali za vitendo vya kikatili na kinyanyasi kwa watoto walemavu ambavyo vinafanyika kwenye vyuo hivyo.


“Nyenzo hii imetumika kupata taarifa mbalimbali kwenye Vyuo vya ufundi nchini. Tumeijadili na tumeona ni muhimu kwani imeandaliwa vizuri.


Lakini pia italeta chachu namna bora ya kubaini ni aina gani ya vitendo vya kikatili ambavyo vinafanyika, lakini ni nani ambaye ni msababishi mkuu wa hivyo vitendo vya kikatili katika vyuo vya ufundi vya Tanzania.’’ Amesema Dk. Magreth Matonya.


Ameongeza kuwa kama Serikali itaendelea kuwasaidia vijana wote wenye Ulemavu Vyuo vya ufundi ambao wanatakiwa kusoma na kuepuka changamoto za ukatili.


‘’Vijana wenye ulemavu wanahitaji kusoma,wanapokutana na changamoto ya vitendo vya kikatili wanapata msongo wa mawazo kiasi kwamba hawawezi kusoma na wakafanikiwa na kutimiza ndoto zao. 


Lakini pia wanapata msongo wa mawazo kutoka kwenye jamii, kutoka kwenye familia, lakini upande wa mfumo wa vyuoni, wanapata msongo wa mawazo kutoka kwa Wanafunzi pamoja na Walimu kwani mpaka sasa wapo baadhi yao bado hawajawatambua wenye ulemavu, hivyo nyenzo hii inakuja kusaidia na muhimu zaidi.’’ Amesema Dk. Magreth Matonya 


Kwa Upande wake, Mshiriki kutoka (NACTVET) Taasisi ambayo inasimamia Vyuo hapa nchini, Bw. Eligius Bwalya, ambaye ana ulemavu wa aina mbili unaohusisha viungo na macho, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani wameweza kubainisha vitu mbalimbali ilikuweza kuchukuliwa hatua za haraka katika kumsaidia Kijana mwenye ulemavu yakiwemo masuala ya kuomba usajili wa vyuo ama kazi pamoja na matangazo mengi yanawabagua walemavu.


‘’Kuna shida katika masuala ya matangazo ama katika masuala ya kutuma maombi yawe ya kazi ama kujiunga na vyuo ama shule.


Matangazo haya yanawatenga walemavu ikiwemo mfano kujiunga na vyuo muombaji anawez kushindwa kufanya vizuri katika kujaza maoni yake mtandaoni ipo mifumo ambayo sio rafiki hali ambayo inaweza muombaji kujaziwa uongo,

 

Lakini pia Mfano unakuta matangazo haya yanaweka masharti fulani fulani ambayo yanawatenga walemavu, ama unakuta baadhi ya matangazo hasa ya kwenye televisheni mwanzo limeanza vizuri muombaji awe na sifa hii na zile, lakini kule mwishoni linamalizia kwa maoni zaidi wasiliana na mawasiliano yanayopita chini’’ hii inatenga walemavu hasa wasioona nchini hivyo, ameomba namna ya kuona hatua za kuchukuliwa ilikuwa katika usawa pande zote.’’ Amesema Eligius Bwalya. 


Aidha, Wadau hao kwa pamoja na wenzao kutoka nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Namibia wameweza kutoa maoni yao kwa kila nchi kuona jinsi ya kupata hatua sahihi za kuwasaidia walemavu katika vyuo vya ufundi.






TMDA YANG'ARA MASHINDANO YA SHIMMUTA, YAICHAPA LGTI MABAO 4 KWA 2.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


TIMU ya soka ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) maarufu kama TMDA FC imeicharaza timu yaChuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo ya LGTI FC kwa jumla ya mabao 4 dhidi ya 2 katika mashindano ya SHIMMUTA yanayoendelea Jijini Dodoma.


Mchezo huo umechezwa leo saa 2:00 asubuhi katika uwanja wa Humanity-1 uliopo Chuo Kikuu cha Dodoma.


Akizungumza mara baada ya mchezo huo kocha wa TMDA Bw. Brian Kyando ameeleza kuwa timu yake ilijiandaa vyema kupata matokeo katika mchezo huo.


"Tunamshukuru Mungu kwa kupata matokeo mechi ya leo. 

Tulijipanga kushambulia kuanzia dakika ya kwanza ili tuweze kupata magoli mengi lakini wapinzani wetu nao walijitahidi kutuzuia tukaishia magoli hayo manne. Mchezo huo umeshapita na sasa tunaangalia michezo iliyo mbele yetu ili nayo tufanye vizuri.


Mashindano ya SHIMMUTA yameanza kuanzia tarehe 12 Novemba, 2023 na yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 25 Novemba, 2023.





Thursday, November 9, 2023

MAKONDA ATOA MAAGIZO KWA MAWAZIRI, KAGERA

 

Na Alodia Babara 


Bukoba. 



Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda,  ametoa maagizo mbalimbali kwa Mawaziri wa wizara nne hapa nchini ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuwapigia simu mawaziri hao na kutoa majibu ya changamoto na kutatua changamoto hizo.


Mawaziri waliopigiwa simu ni pamoja na waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, Waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun, waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa.


Makonda ametoa maagizo hayo leo Novemba 9, 2023 wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara akiongea na wananchi mkoani Kagera uliofanyika uwanja wa mashujaa Mayunga.


Moja ya changamoyo zilizotajwa ni pamoja na ujenzi wa soko kuu, kingo za mto Kanoni, ujenzi wa stend kuu, uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Bukoba, tatizo la nida maeneo ya mipakani na ujenzi wa barabara za lami.


Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akijibu kuhusu changamoto za ujenzi wa soko kuu, stend kuu na kingo za mto Kanoni amesema kuwa maagizo ya katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Makonda ameyapokea na kufanyia utekelezaji haraka, mwezi Desemba 2023 atafika mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua maeneo itakapotekelezwa miradi hiyo


Akijibia changamoto ya vitambulisho vya NIDA kwa upande wa wananchi waishio mipakani waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun amesema kuwa, swala la vitambukisho vya NIDA katika maeneo hayo wizara inalifanyia kazi ili kuharakisha zoezi na wale wenye haki ya kupata kadi za NIDA waweze kuzipata. 


Amesema wameanza mkakati wa kutembelea mikoa iliyopo maeneo ya mpakani kwa kuanza na mkoa wa Mara na baadaye watakwenda Kagera.


Makonda amewataka Askari wa usalama barabarani wote nchini kutowaonea waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na badala yake watumie sheria wanapowakamata na kuwakuta na makosa.

 



HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAVUKA MALENGO UKUSANYAJI WA MAPATO

 

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imevunja rekodi ya kukusanya kiwango katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuaniza Julai mpaka Septemba 2023


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Bagamoyo Mhe. Halima Okashi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo tarehe 09 Novemba 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.



Akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani Mkuu huyo wa Wilaya aliwapongeza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuanzia Julai mpaka Septemba 2023. 



Katika kipindi hicho Halmashauri imekusanya zaidi ya shiling bilioni 1 sawa na asilimia 27.7 ambapo ni asilimia 2.7 zaidi ya malengo waliyojiwekea ya asilimia 25.



"Niwapongeze Madiwani wa Kata zote pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato kwenye taarifa yenu inaonyesha mapato yaliyopatikana ni asilimia 27.7 ambapo malengo yalikuwa ni asilimia 25 hivyo hongereni sana kwa ongezeko hilo la asilimia 2.7" alisema Bi Halima Okashi


Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliwataka Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kuongeza ubunifu zaidi ili kuweza kupata wigo wa kuongeza mapato utakaopelekea uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo akipokea pongezi hizo kwa niaba ya Baraza la Madiwani Mhe. Mohamedi Usinga aliahidi kuendelea kuboresha vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuboresha mapato kwenye Halmashauri hiyo.





MAGAZETI YA LEO TAREHE 09 NOVEMBA 2023.