Wednesday, November 8, 2023

WANUFAIKA MRADI WA KLIC WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA TEHAMA-TET

 

Na Andrew Chale,Dar es Salaam.

Shule zote nchini zilizonufaika na vifaa vya mradi wa KOREAN E-LEARNING IMPROVEMENT COOPORATION(KLIC) ulio chini ya Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan ya nchini Korea ya Kusini, wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA, wametakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri , kiusahihi na kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti,Habari na Machapisho waTaasisi ya Elimu Tanzania(TET), Bw. Kwangu Masalu leo tarehe 8/11/2023 katika shule ya Sekondari Kimbiji iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam katika ziara ya ujumbe wa watu kutoka korea ulipofika shuleni hapo kwa ajili ya kugawa vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia masomo pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo ya namna ya kuvitumia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo .

Mwakilishi wa walimu waliopo kwenye ziara hiyo kutoka nchini Korea Kusini, Bwana.Kim Chi Gon ameeleza kuwa , wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanakuza utumiaji wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini na kwani kwa sasa ulimwengu umebadilika sana hasa katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Twidike Ntima ameeleza kwamba shule hiyo kuwa moja ya shule za mfano wa kupata vifaa vya TEHAMA ni jambo kubwa ambapo imesaidia sana kwa walimu kuweza kufanya kazi kwa urahisi na kuwa endapo masuala ya TEHAMA yataendelea kusambaa nchi nzima basi wanafunzi nchini na walimu wataweza kupiga hatua katika masuala ya elimu.

Naye Mkuu wa shule hiyo Bi. Joyce Ndaona amesema kuwa kwa sasa walimu wa shule hiyo wamepata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa nchini Korea ya Kusini ambapo wameweza kupata ujuzi wa kurahisishiwa kazi hasa katika eneo la ufundishaji na kuwapa nafuu wanafunzi kutumia TEHAMA kwenye ujifunzaji tofauti na awali.

Hata hivyo ugeni huo wa walimu na wanafunzi ukiwa katika shule hiyo ya Kimbjiji, uliweza kujionea namna wanafunzi wanavyoonesha uelewa katika masomo yao ambapo waliweza kuonesha utaalamu wao kupitia masomo ya fikizia na Uchoraji na baadae wanafunzi hao kuweza kufanya mafunzo kwa vitendo.






No comments:

Post a Comment