Na Athimani Shomari
Vijana 24 kutoka Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya wamehitimu mafunzo yao ya mwezi mmoja ya Sanaa na Utamaduni leo Tarehe 06 Novemba 2023, katika chuo cha TaSUBa Wilayani Bagamoyo na kufanikiwa kuongeza elimu yao ya Sanaa na Utamaduni,
ambapo sasa wanaweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na awali.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya kumaliza mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye, ametoa wito kwa vikundi mbalimbali nchini vinavyofanya shughuli za Sanaa na Utamaduni kufika chuoni hapo ili kupata elimu itakayowaongoza katika kazi za Sanaa na Utamaduni.
Dkt. Makoye alisema TaSUBa ni sehemu ya kulea wasanii wa aina mbalimbali ikiwemo wale wa ngoma za asili hivyo watanzania wasione uvivu kujiunga na chuo hicho kwa kukuza Taaluma zao ili waweze kufikisha kwenye jamii ujumbe unaolingana na maadili ya kitanzania kwa weledi uliotukuka.
Wakati huohuo Dkt. Makoye ameishukuru Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya kwa kugharamia mafunzo ya vijana hao ili wapate mafunzo sahihi ya Sanaa na utamaduni kwa lengo la kukuza vipaji vyao, kuongeza vipato vyao na kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia ya Sanaa na Utamaduni.
Alisema Tulia Trust, imekuwa msatari wa mbele katika kuwafadhili vijana mbalimbali kuendeleza vipaji vyao vya Sanaa na Utamaduni katika chuo hicho kinachotoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kilichopo chini ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambpo miongoni mwao
wapo wanaopata kozi fupi, ngazi ya cheti na Astashahada.
Awali wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi, wahitimu hao walismea wanaishukuru Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa
kuwapokea na kuwapa mafunzo bora yatakayowawezesha kufanya shughuli
zao kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na awali kabla ya kupata mafunzo hayo.
Walisema uwepo wa TaSUBa na vijana kupata fursa ya mafunzo chuoni hapo
kumewafanya vijana wengi hapa nchini kuiona thamani ya vipaji walivyonavyo kwani vinaendelezwa na hatimae wananufaika kupitia vipaji hivyo.
Waliongeza kwa kusema kuwa katika mafunzo hayo waliyopata wamefanikiwa
kujifunza ngoma mpya ambazo walikuwa hawazijui, lakini pia wameweza kujifunza namna ya kufanya maboresho ya ngoma zao za asili za mkoa wa Mbeya.
Aidha, sambamba na hayo, vijana hao pia walisema wameweza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Sanaa na Utamaduni wa Mwafrika kupitia Tamasha la 42 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambalo lilifanyika chuoni hapo (TaSUBa) mwezi Oktoba 2023.
Kupitia risala yao, vijana hao wamemshukuru Mbunge wa Mbeya Mjini na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na Taasisi ya Tulia Trust, kwa kutambua uwepo wa vijana na kuwashika mkono kwa kuwawezesha kutoka kwenye hatua moja kwenda hatua nyingine na kunufaika kupitia vipaji walivyonavyo.
Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya imeasisiwa na na Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini, ambae pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, lengo likiwa ni kuwasaidia
vijana na wakazi wa mkoa huo kwa ujumla kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Picha zote Na Herry Pesa
No comments:
Post a Comment