Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Mheshimiwa Halima Okash ametoa pongezi kwa Madiwani na wataalam wa halmashauri ya Chalinze kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika suala zima la ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri na kuvuka asilimia 27 ya malengo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Okash ametoa Pongezi hizo leo Tarehe 08 Novemba 2023 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.
Katika hotuba yake ya kutoa Salaam za Serikali amewataka madiwani na watendaji wa Halmashauri kuendelea na jitihada za ukusanyaji mapato ya ndani na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kufikia malengo ya ukusanyaji mapato ili kutoa huduma stahiki kwa Wananchi.
Okash Pia ametoa Pongezi kwa Halmashauri ya Chalinze katika suala zima la usimamizi wa mkataba wa lishe ulioiwezesha Halmashauri kushika nafasi nzuri kimkoa na kuwataka uongozi wa halmashauri kuifanya lishe kuwa ajenda ya kudumu kuanzia ngazi ya kitongoji mpaka wilaya.
Mkuu wa wilaya amewataka viongozi wa halmashauri kuzingatia utawala bora kwa kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa wakati kuanzia Kitongoji,kijiji na Kata ili kuweza kubaini changamoto na kero mbalimbali zinazoweza kutokea katika jamii na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati pasipo kuchelewa.
Aidha Okash ametoa rai kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuchukua tahadhali kutokana na mvua za Elinino zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Pwani hususan Chalinze, kwa kuondoka katika mabonde na kukaa maeneo yenye miinuko ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo.
Mkuu wa wilaya alimalizia hotuba yake kwa kuwataka viongozi wote katika Mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea kuisemea Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya katika kuboresha maisha ya watanzania kwa kujenga miundombinu mbalimbali katika sekta za afya,elimu,barabara na Maji ili watanzania wapate kufahamu yanayoendelea.
No comments:
Post a Comment