Wednesday, November 1, 2023

KIKWETE: SERIKALI ITALINDA VIJANA WAPATE AJIRA KWA VIGEZO VYA UTAALAMU NA SI UZOEFU KAZINI.

 

Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema serikali itahakikisha inawalinda vijana kwenye soko la ajira kwa kuhakikisha ajira zao za kwanza kwenye utumishi zinazingatia vigezo vya utaalamu wa kada husika na sio uzoefu kazini. 


Kikwete amesema hayo leo Jumatano Novemba 01, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ngwasi Kamani aliyehoji kigezo cha kutakiwa uzoefu katika kuomba kazi kwa vijana waliohitimu vyuo kuwa ni ubaguzi kwa vijana wanaoanza kuomba ajira. 


"Ajira za serikali zinatekelezwa kwa kuzingatia sera ya menejimenti na ajira ya mwaka 2008. Kwa mujibu wa aya ya 4 kifungu cha 2 (i) inaelekeza kwamba ajira ya kwanza hususani kwa wale wanaoajiriwa kwa cheo cha kuanzia kwenye miundo ya serikali itafanyika kwa kuzingatia vigezo vya utaalamu bila kujali uzoefu isipokuwa kama ajira husika itahitaji kuwa na uzoefu. Suala la uzoefu lipo kwenye madaraja ambayo si ya kuingilia kazini kama nafasi za waandamizi, viongozi au kada ambazo uzoefu ni sifa za msingi kuingia kama vile udereva ambao mtumishi lazima ajue kuendesha gari kwa viwango vilivyowekwa." Amesema Kikwete. 


Akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge Kamani aliyetaka kujua kauli ya serikali kwa waajiri wa sekta binafsi wanaoendelea kutumia kigezo cha uzoefu kutangaza ajira pamoja na serikali kuwatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu wote wanaojitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma, Naibu Waziri Kikwete amesema serikali kupitia kwa ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia vigezo vinavyotakiwa katika soko la ajira huku wakiendelea kutoa maelekezo ya mara kwa mara kuzingatia hilo.


"Pamoja na utaratibu wa kawaida wa kwenye soko la ajira, lakini kwenye sekta binafsi kinachoangaliwa ni tija ili mtu apate faida kwenye jambo lake lakini serikali itaendelea kusimamia utoaji wake wa ajira." Amesema. 


Sambamba na hilo, Kikwete alikamilisha majibu yake hayo bungeni kwa kusema kwasasa serikali inaendelea kukamilisha sheria na muundo wa utumishi ambao utawatambua vijana wote wanaojitolea ili waweze kuingia kiurahisi katika soko la ajira. 

No comments:

Post a Comment