Thursday, November 30, 2023

MAAMBUKIZI YA MALARIA KAGERA YAFIKIA ASILIMIA 18.

 

Na Alodia Babara 

Bukoba. 

Misimu miwili ya mvua ya vuli na masika inayonyesha mkoani Kagera imetajwa kama sababu ya mbu kuzaliana na hivyo kusababisha kiwango cha maambukizi ya malaria kufikia asilimia 18,  mkoani humo huku kiwango cha taifa kikitajwa kuwa ni asilimia 8.

Kufuatia kiwango hicho kuwa juu, wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa ambazo ziko pembezoni na vijiji viko umbali wa kuanzia kilomita tano kufika katika vituo vya afya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 38 wamepewa vifaa tiba.

Akizungumza leo Novemba 30,2023 katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya kutolea huduma za tiba katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo mkurugenzi wa mradi wa Shinda malaria Dk Dunstan Bishanga amesema wahudumu hao walipewa mafunzo ya awali jinsi ya kupima joto na kuwaelimisha wanachi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua.

“Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa mitatu hapa nchini yenye maambukizi ya juu ya malaria ambapo watu 18 kati ya watu 100 wameathirika na vimelia vya ugonjwa huo, pamoja na jitihada zote tunashukuru kuna upungufu wa visa hivyo, kwani mwaka 2019 Kagera ilikuwa na visa vya malaria 580,000 na mwaka 2022 visa hivyo vimepungua hadi 250,000”amesema Dk Bishanga

Dk Bishanga ameongeza kuwa, kiwango cha malaria mkoani hapa kimekuwa kikipanda juu zaidi katika vipindi viwili vya msimu wa mvua ambavyo ni vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba na msimu wa masika kuanzia Machi hadi Mei.

 Kwa upande wake mkurugenzi wa IHI taasisi ya afya ya Ifakara Honorath Masanja amesema kuwa, vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 60, vimegaiwa kwa wahudumu hao na vifaa hivyo ni vipima joto, buti, baiskeli, makoti ya mvua, mizani na kifaa cha kubebea vifaa (kit).

Katibu tawala mkoa wa Kagera Toba Nguvila akiwa amemwakilisha mkuu wa mkoa huo amesisitiza viongozi wa ngazi zote kuwa wanapaswa kushirikiana kupiga vita ugonjwa wa maralia kwani yeye kama kiongozi wa mkoa hajisikii vizuri kuona watu wake wanaugua maralia na kuwa jamii ielimishwe maatumizi ya vyandarua na mazalia ya mbu yateketezwe.

Jastini Jakson kutoka wilaya ya Kyerwa ni mmoja wa wahudumu ngazi ya jamii waliopokea vifaa hivyo amesema kuwa, walipatiwa mafunzo jinsi ya kumtambua mgonjwa wa maralia kwa kumhoji kwanza na baadaye kumpima joto la mwili.

Amesema kuwa, kutokana na mafunzo waliyopewa walifundishwa kuwa, baada ya kuona mgonjwa ana homa kali, anawangwa kichwa na anatapika wanapaswa kuchukua jukumu la kumpa rufaa kwenda kituo cha afya na wamejifunza utunzaji wa kumbukumbu na kutunza siri za mgonjwa. 

No comments:

Post a Comment