Friday, November 3, 2023

MZEE MBAGALA, MDAU WA MAENDELEO BAGAMOYO ATUA BUNGENI.

 

Mzee, Rajabu Selemani Mbagala (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha nje ya ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma leo tarehe 03 Novemba 2023, katikati ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mh. Muharami Mkenge, kitoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Nianjema ndugu Omar Makamba na katibu mwenezi CCM Kata, Mzee Marijani (Minjori.)


Mzee, Rajabu Selemani Mbagala (kushoto) akiwa katika picha nje ya ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma leo tarehe 03 Novemba 2023, kutoka kulia ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, wa pili kulia ni Katibu mwenezi CCM Kata ya Nianjema Bagamoyo, Mzee Marijani (Minjori.) Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani, Mh. Juma Aweso, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mh. Muharami Mkenge,  na wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Nianjema ndugu Omar Makamba
..........................................

Na Athumani Shomari- Dodoma

Leo Tarehe 3 November 2023, Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Mheshimiwa Muharami Shaban Mkenge, amemkaribisha Bungeni Mdau wa Maendeleo Jimbo la Bagamoyo Mzee, Rajabu Selemani Mbagala, ikiwa ni nafasi ya kipekee kwa Mzee Mbagala kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Bagamoyo.


Mzee Mbagala ni maarufu kwa wakazi wa Bagamoyo kutokana na kujitolea katika maendeleo ya huduma za jamii hasa ukizingatia ni mtu binafsi ambae hana cheo serikalini bali kinachomsukuma ni utu wake dhidi ya binadamu wenzie na kukereketwa kwake na Maendeleo ya mji wa Bagamoyo.


Miongoni mwa mambo aliyoyafanya katika kusaidia huduma za jamii, Mzee, Rajabu Selemani Mbagala ameweza kutoa eneo la kujenga Zahanati katika kitongoji cha Kimarang'ombe kata ya Nianjema, eneo la kuabudia (Msikiti) eneo la kuzikia (Makabuli) kwa waislamu na wakristo, eneo la kujenga ofisi ya Chama Cha Mapinduzi kata ya Nianjema ambapo maeneo yote hayo ameyapima pamoja na kugharamia michoro (survey plan), kwa fedha zake.


Mzee Mbagala aliweza kumiliki maeneo makubwa ya Ardhi ikiwa mji bado haujakua na baadae maeneo hayo kuyapima viwanja na kufanya maeneo kuwa na mitaa mizuri iliyopimwa kitaalamu jambo ambalo linaleta muonekano mzuri wa mji wa Bagamoyo.


Hali hiyo imepelekea Maeneo kadhaa ya Kitongoji cha Kimarang'ombe kuwa na viwanja vyenye muonekano mzuri wa mitaa ukilinginisha na maeneo ambayo hayajapimwa (unplanned areas).


Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge, amesema anamshukuru mzee Mbagala kwa kujitolea kwake katika mambo mbalimbali ya maendeleo hali inayoleta chachu ya maendeleo Kata ya Nianjema na Bagamoyo kwa ujumla.


Mbunge huyo Muharami Mkenge amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo Bagamoyo kuiga mfano wa Mzee Mbagala ili kuisaidia Serikali katika huduma mbalimbali za kijamii.


Katika safari yake hiyo ya Bungemi Mzee Mbagala amesindikizwa na Mwenyekiti wa CCM kata ya Nianjema ndugu Omar Makamba na katibu mwenezi CCM Kata, Mzee Marijani (Minjori.)



No comments:

Post a Comment