Thursday, November 22, 2018

MASHINDANO YA RIADHA KWA WANAWAKE KUFANYIKA DAR.


Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Mkenyenge (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitangaza mashindano ya riadha kwa wanawake yanayoitwa “Ladies First” yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24-25 Novemba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JICA) Bw. Toshio Nagase na kushoto ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Riadha nchini (RT) Bi. Ombeni Zavala.

Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JICA) Bw. Toshio Nagase akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza mashindano ya riadha kwa wanawake yanayoitwa “Ladies First” yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24-25 Novemba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katikati ni Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Mkenyenge na kushoto ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Riadha nchini (RT) Bi. Ombeni Zavala.

Katibu Msaidizi wa Chama cha Riadha nchini (RT) Bi. Ombeni Zavala akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza mashindano ya riadha kwa wanawake yanayoitwa “Ladies First” yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24-25 Novemba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katikati ni Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Mkenyenge na kulia ni ni Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JICA) Bw. Toshio Nagase.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JICA) Bw. Toshio Nagase (wa pili toka kushoto) wakati wa kutangaza mashindano ya riadha kwa wanawake yanayoitwa “Ladies First” yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24-25 Novemba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Picha na WHUSM- Dar es Salaam.

MHE HASUNGA AKABIDHIWA RASMI OFISI, DKT TIZEBA ASHAURI MAZITO KUHUSU KILIMO

Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Kulia) akifurahi jambo pamoja na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
..............................................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza leo tarehe 22 Novemba 2018 amemkabidhi rasmi ofisi Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb).

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa mikutano maarufu kama Kilimo IV Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu mawaziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, na Wakuu wa idara na Vitengo.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mhe Dkt Tizeba amempongeza Mhe Hasunga kwa kuteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo ambapo amesisitiza kusimamiwa kwa weledi huduma za ugani ambazo kwa kiasi kikubwa hakuna jambo la kujivunia katika eneo hilo kutokana na mgawanyo wa kimajukumu kuwa katika wizara mbili ya kilimo na TAMISEM jambo ambalo linapunguza ufanisi wa kiweledi.

Alisema kuwa wizara inapaswa kuendelea kusomesha wataalamu mbalimbali nchini wakiwemo wa ugunduzi na utafiti ili kuongeza tija ya kilimo na utoaji elimu kwa wakulima na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa wananchi sambamba na Taifa kwa ujumla.

Vilevile amesema kuwa Wizara ya kilimo ni tanuru muhimu kwa mahitaji ya wananchi hivyo inapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi na serikali ikiwa ni pamoja na kupewa fedha kwa wakati ili kukamilisha miradi mbalimbali ambayo tayari imeanzishwa.

Kuhusu mfumo wa uzalishaji wa mbegu alisema kuwa serikali ina Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) ambao wanafanya kazi nzuri ya uzalishaji wa mbegu lakini wanapaswa kuwezeshwa ili waweze kuzalisha mbegu kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji badala ya kuzalisha mbegu wakati msimu wa kilimo unaendelea.

“ASA wanazalisha mbegu wakati ambapo msimu wa kilimo umefika hivyo mbegu zao zinakosa umuhimu kwa wakulima, hivyo wanapaswa kuzalisha mbegu kabla ya msimu wa kilimo kufika” Alisisitiza Dkt Tizeba.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa unaendelea vyema lakini hausimamiwi ipasavyo na Taasisi zingine za serikali zilizopewa jukumu kubwa na muhimu la kusimamia shughuli hiyo wakiwemo Wakala wa majengo Tanzania (TBA).

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amempongeza waziri huyo mstaafu Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye wizara ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa weledi ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2018/2019 ambayo imekuwa kwa asilimia 7.1

Waziri Hasunga alisema kuwa Dkt Tizeba ni mfano wa kiongozi bora nchini ambaye ametekeleza majukumu yake kwa weledi na kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi wengine jambo ambalo linatoa chachu na kuonyesha jinsi alivyo mzalendo kwa Taifa.

“Kutokana na alama alizoziacha Dkt Tizeba kwenye wizara ya kilimo hakika tunastahili kumuona kama Mtakatifu kwani kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa chakula nchini lakini alisimamia kidete na kuhakikisha kuwa swala hilo linamalizika na sasa nchi ina ziada kubwa ya chakula hakuna njaa”

Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa“Dkt Tizeba alihakikisha kero ya Tozo na Kodi zinafutwa na kusaliwa na Tozo na Kodi chache jambo ambalo limeongeza ufanisi katika wizara, usimamizi huu mzuri uliofanywa hauwezi kusahaulika daima
Mhe Hasunga aliongeza kuwa mfumo wa uagizaji mbolea wa pamoja ulisimamiwa vizuri na Dkt Tizeba jambo hilo litasalia kuwa muhimu na alama kwa Taifa.

Aidha, Alisema kuwa katika uongozi wa Dkt Tizeba nchi imezidi kuimarika kupitia manufaa wanayoyapata wananchi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na mfumo wa ushirika ambao wananchi walipoteza imani kwa kiasi kikubwa na Ushirika lakini kwa kipindi cha muda mfupi umeimarika kwa kiasi kikubwa.
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya kilimo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. 

Picha ya pamoja waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Naibu mawaziri wizara ya kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, na Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wote wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. 

Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018.

Wednesday, November 21, 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA JUKWAA LA FURSA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI MKOANI TABORA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama chupa yenye ujazo wa nusu lita yA mkojo wa sungura wakati alipotembelea banda la wanawake wajasiriamali wasindikaji wa Tabora katika maonyesho ya Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji katika Mkoa wa Tabora yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Novemba 21, 2018. Kwa mujibu wa Mratibu wa Wajasiriamali hao, Bibi Ashura Mwazembe, mkojo wa Sungura unatumiwa kama mbolea ya mazao ya kilimo na pia ni dawa nzuri sana ya kuua wadudu waharibifu wa mazao. Lita moja ya mkojo huo inauzwa sh. 10, 000/=. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 
 Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji mkoani Tabora kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Novemba 21, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Imani Matabula  (kulia)  kuhusu sabuni zinazotengenezwa na Kampuni yake ya Matabula Soap Investment ya Kaliua mkoani Tabora katika maonyesho   ya Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji Mkoani Tabora yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Novemba 21, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sabuni za Kampuni ya Matabula Soap Investment ya Kaliua mkoani Tabora, Imani Matabula  (kulia)  katika  maonyesho   ya Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji Mkoani Tabora yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Novemba 21, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Imani Matabula. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo  kutoka kwa Saidi Kanimba  kuhusu viatu vya ngozi vinavyotengenezwa   katika Halmashuri ya wilaya Uyui mkoani Tabora katika Maonyesho ya  Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji Mkoani Tabora yailyofanyika kwenye Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Novemba 21, 2018. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakisalimina na Kaimu Mhariri Mtendaji wa  Magazeti ya Serikali (TSN),  Tuma Abdallah (kushoto) wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege  wa Tabora kushiriki katika  Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji Mkoani Tabora, Novemba 21, 2018.  Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

DKT. ABBASI AWATAKA WAANDISHI KUFUATA SHERIA YA HABARI.

 Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi 
....................................................
Na Grace Semfuko-MAELEZO

Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amewataka waandishi wa habari kutumia haki na wajibu wao katika kulinda maadili yao ya uandishi na kutotumia taaluma yao kukejeli na kuchafua watu wengine
Amesema Sheria mpya namba 12 ya mwaka 2016 ya huduma za vyombo vya habari kifungu cha 7  ingawa inawapa Waandishi wa Habari kukusanya,kuhariri na kusambaza habari lakini haiwapi fursa waandishi hao kuandika habari ambazo zinachafua wengine.

Dkt Abbasi aliyasema hayo katika mahojiano na kipindi cha Hallow Tanzania kinachorushwa na Radio Uhuru ya Jijini Dar Es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali Nchini.

“Sheria Mpya ya Habari inawapa fursa Waandishi kufanya kazi zao za kukusanya,kuhariri na kusambaza habari,sheria hii haijamnyima Mwandishi wa Habari kupata habari, lakini pia haijatoa fursa za kusambaza habari za kukejeli na kuchafua wengine, sheria itachukua nafasi yake kwa atakaebainika kufanya hivyo” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilichukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni sehemu ya kulinda maadili ya uandishi wa habari na kuvitaka vyombo vingine kuendelea kuheshimu,kulinda na kutetea maslahi ya Taifa.

Akihojiwa na Mtangazaji wa kipindi hicho Aggrey Manzi kuhusiana na baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii katika kuchafua wengine, Dkt Abbasi alisema sio sahihi kutumia mitandao hiyo katika kuona wengine hawafai, bali mitandao itumike kutangaza habari za Maendeleo.

Kuhusu wanaobeza Maendeleo ya nchi yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli swali lililoulizwa na Mkuu wa Vipindi wa Radio hiyo Bw. Abdallah Hussein ,Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi alisema Serikali itaendelea kufanya Maendeleo na kwamba wanaobeza hawazuii utekelezaji huo

“Walisema hakuna ndege, ziliponunuliwa pia walisema kuwa nani atapanda, wakasema hakuna miundombinu ya barabara inajengwa bado wanasema, pia daraja la Mfugale limejengwa, Mradi Mkubwa wa umeme wa Stiglers Gorge unajengwa, Reli ya Kisasa ya standard Gauge inajengwa lakini bado wanasema, waache waseme tu, hawatuzuii kufanya miradi ya Maendeleo kwa ajili ya wananchi”

Akizungumzia kuhusu ukuaji wa uchumi kwa wananchi mmoja mmoja swali lililoulizwa kwa njia ya simu na Abdallah Athumani Mkazi wa Chalinze Dkt Abbasi alisema ukuaji wa uchumi unatokana na kuimarisha miradi ya Maendeleo na kwamba wakazi wanaponufaika na miradi hiyo uchumi unakua kwa mtu mmpja mmoja.

“Unapoenda kutibiwa kwa gharama nafuu katika Hospitali ambazo zimejengwa na Serikali unakuwa umehifadhi fedha zako ambazo zitatumiwa kwa matumizi mengine hii ina maana umeepukana na matumizi makubwa ya gharama za hospitali, tunaposema elimu bure ina maana Mzazi halipii gharama za elimu na fedha hizo zinafanya kazi nyingine, kwa ujumla uchumi umekua kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali.

ASIYETAKA UMOJA, USHIRIKIANO NA UTIIFU AJIODOE CCM.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Pwani Farida Mgomi akizungumza na viongozi wa umoja huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Pwani Farida Mgomi akisisitiza jambo kwa wajumbe wa mkutano huo.
................................................. 

Na shushu Joel,Mlandizi.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Pwani Farida Mgomi amewataka wanawake wote katika mkoa huo kuacha majungu,fitina na chuki na badala yake amewatak kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu kwa viongozi wao ili kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola nchini kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.

Wanawake walio wengi wamekuwa wakiendekeza majungu katika jumuiya na kuacha kufanya kazi  za wanachama kwa kuhamasisha uhai wa jumuiya hiyo.

Akizungumza na wanawake wa wilaya ya kibaha mwenyekiti huyo aliwataka wanawake kuacha tabia za kinafiki na matokeo yake wapige kazi za uzalishaji kwa ajili ya kutimiza adhima ya serikali ya awamu ya tano kwenye kuhakikisha nchini yetu inakuwa katika uchumi wa kati kupitia uanzishwaji wa viwanda.

“Kama kuna mwanamke ajisikii kufanya kazi na umoja wa wanawake ni bora akajiengua na kutuachia chama chetu kisichohitaji majungu wala fitina za aina yeyote ile hivyo ni bora wanafiki wakajiondoa wenyewe bila kufukuzwa katika jumuiya hiyo”Alisema Mgomi.

Aliongeza kuwa uchaguzi ulishakwisha kupita hivyo kila mmoja anapaswa kuwaheshimu viongozi waliopo madarakani na si kutengeneza makundi ambayo hayana tija katika chama.

Aidha alisema kuwa wanawake ni msingi mkubwa na wenye kutumainiwa katika chama hivyo hakuna sababu ya kuendekeza fitina wala majungu katika jumuiya kwani yatawasambaratisha na kupoteza dira ambayo wamejiwekea katika kukuza uchumi wa viwanda kwenye mkoa wa pwani.

“Wanawake wenzangu tutumie fursa zilizopo katika mkoa wetu wa pwani ili tuweze kujipatia fedha  za kuendeshea maisha na familia zetu kwani serikali inatoa mikopo ya bila riba kupitia halmashauri zetu kote nchini”

Aliongeza kuwa migogoro imekuwa ikichangia kutoendelea kwa jumuiya nyingi hivyo kutokana na nafasi yangu ya umwenyekiti wa Uwt sihitaji kuona wala kusikia  chembechembe wala harufu ya mgogoro kwenye jumuiya yangu kwani migogoro inarudisha nyuma maendeleo ya chama chetu.

Kwa upande wake Tatu Haji ambaye ni mwenyekiti wa Uwt kata ya mlandizi vijijini amempongeza mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa jinsi anavyijitolea katika ujenzi wa jumuiya kwani baadhi ya watu wasio na nia njema na viongozi kuanza kupenyeza chuki kwa wananchama ili wachukiane.

Aidha amemtaka mwenyekiti huyo kuongeza ukali wa kuwafukuza au kuwasimamisha uanachama wale walio na nia ya kuitaka jumuiya kusonga mbele na kuwa ya mfano katika jumuiya zote za chama.

Naye Lucy Zebedayo amesema kuwa chanzo cha migogoro mingi inayokuwepo katika jumuiya ni baadhi ya watu kuwa na tamaa ya kutaka nafasdi za watu ambazo uanza kupandikiza chuki na fitina na hivyo kupelekea kutengenezeka kwa majungu yasiyo na maana katika nyadhifa.

Hivyo aliongeza kuwa ili vitu hivi viondoke katika jumuiya zetu ni lazima viongozi wetu wafanye maamuzi ili kunusuru juiya zetu,tena ni kwa kuwafukuza watu uanachama au kuwasimamisha.

“Walio na nia mbaya na uongozi wetu ni bora wakaondoka kwenye chama chetu mapema ili pumba na mchele uweze kujulikana”Alisema.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa UWT Mkoa wa Pwani, wakimsikiliza mwenyekiti wao wa mkoa kwa makini wakati akizungumza nao kuhusu wasaliti wa chama kujiengua.

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 21, 2018.

Tuesday, November 20, 2018

RAIS DKT. MAGUFULI AAHIRISHA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kuhusu uamuzi wa Rais  Dkt. John Pombe Magufuli  wa kuahirisha Maadhimisho ya sherehe za Uhuru yaliyotarajiwa kufanyika  9 Desemba, 2018, Kwenye ukumbi wa Mkuu wMkoa wa  Lindi, Novemba 20, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi
………………..
*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya siku ya Uhuru, Disemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha shamrashamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma ambayo itaitwa Uhuru Hospitali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Amesema hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino  kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa  mkoani humo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. “Wanaweza kutumia siku hiyo kwa kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali.”

Kufuatia maagizo hayo, Waziri Mkuu amewataka wananchi katika maeneo yote nchini wajiandae kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazopangwa na wakuu wao wa mikoa na wilaya kufanyika katika maeneo yao.

WANANCHI WAMFANANISHA MNEC NA MAGUFULI.

Haji Jumaa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Pwani akisisitiza jambo kwa wananchi wa makulunge.
..................................................
 
Na Shushu Joel, Bagamoyo.
WANANCHI wa kata ya makulunge wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wamempokea mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa shangwe kubwa na matumaini wakiwa na maana watendaji wote wa CCM ni watetezi wa watu wanyonge na  wanaendana katika utendaji wake.

Kilichopelekea  wananchi wa kata hiyo kumpokea MNEC huyo na wajumbe wake kwa shangwe kubwa ni imani ya kuwa chanagamoto zao zilizokuwa zikiwabali kumalizika mara moja.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara kuhusu changamoto zao, wananchi hao  walimwambia MNEC huyo kuwa wamekuwa wakinyanyasika sana kuhusu jambo la Ardhi katika kata hiyo kwa kipindi cha muda mrefu sasa huku mahakama ilishakwisha kutoa hukumu kuwa maeneo hayo ni mali ya wananchi.

Akizungumza kwenye kikao hicho katibu wa wananchi wa winde Athumani Mkwasi alisema kuwa ujio wa MNEC huyo katika kijiji hicho umekuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na kunyanyasika muda mrefu huku kesi ya maeneo hayo yalikwisha kumalizwa na mahakama miaka mingi iliyopita kwani ni tangu enzi za mababu.

“Ujio wako katika kijiji hiki ni sawa na kumuona Rais wetu mpendwa Dkt John Pombe Magufuli asiyependa kuwaona wananchi wake  wanyonge  wakiteseka kwa kitu ambacho wenye fedha wakinufaika”Alisema.

Aliongeza kuwa mgogoro huo wa ardhi umekuwa ni kama kuwanyanyasa wananchi kulingana na kuwa kesi ya eneo hilo ilikwisha malizika na kuamuliwa wananchi kukaa katika maeneo hayo bila kubuguziwa, mbali na hilo amemuomba MNEC kupeleka ombi la wananchi wa winde kwa Rais kuwa watendaji wa idara ya ardhi katika wilaya ya Bagamoyo ni tatizo kubwa na ndio chanzo cha migogoro mikubwa katika sekta hiyo.

Naye zunaiya Mazige amewapongeza viongozi wa CCM walitembelea eneo hilo ili kujionea changamoto ambazo wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakizipata kwa muda mrefu kutoka kwa watu wa winde na bhaharesa juu ya malipo kwa kutokuwalipa stahiki zao na kuwapatia maeneo ya kuishi.

Aliongeza kuwa hatuna ytatizo la kupisha kwa mradi wa kiwanda cha sukari ila shida kubwa yetu ni kutokulipwa sitahiki zetu na kuonyeshwa maeneo yetu ya kujenga na kingine ni ulipwaji mdogo usioendana na usawa wa maeneo yetu.

Akijibu changamoto hizo za wananchi hao MNEC  Haji Jumaa aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa na subra kwani serikali ya awamu ya tano ni kwa ajili ya wananchi wanyonge waliokuwa wakinyanyaswa na matajiri kipindi cha nyuma.

Aliongeza kuwa tatizo lao amelichukua na amewahakikishia kuwa atahakikisha anawaletea waziri wa Ardhi William Lukuvu ili aweze kuwasaidia na kuwatatulia changamoto zao za muda mrefu.

Aidha Jumaa amewapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kuwa na uvumilivu hivyo amewataka kuwa na uvumilivu huo huo mpaka pale tatizo lao litakapokamilika,ila wale walioshinda ile kesi waendelee na ujenzi katika maeneo hayo kwani kutokana na hukumu hiyo hilo eneo ni mali yao.
MNEC wa mkoa wa pwani Haji Jumaa akipokea hukumu iliyotolewa na mahakama miaka hiyo kutoka kwa katibu wa wananchi wa winde.
MNEC wa mkoa wa pwani Haji Jumaa akionyeshwa ramani ya eneo hilo na wananchi wa kata hiyo ili kutambua mipaka ya maeneo yao.
Wananchi wa kijiji cha winde kata ya makulunge wakitoa changamoto zao mbele ya viongozi wa CCM kilichokuwa kikiongozwa na mjumbe wa Nec mkoa wa pwani.

KAWAMBWA KUFUATILIA WALIMU SHULE ZA AWALI.

 MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa
......................................................
Na Omary Mngindo, Yombo Bagamoyo

MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, ameahidi kufuatilia ombi la Wadau wa elimu, la kutaka kuwepo walimu maalumu wa shule za awali, badala ya kutumika wa shule za msingi.

Dkt. Kawambwa ametoa kauli hiyo mwishoni kwa wiki, akizungumza katika kongamano la wadau wa elimu lililoandaliwa na diwani wa Kata ya Yombo Mohamed Usinga, la kuwapongeza walimu katani humo, kwa ufaulu mzuri mwaka huu.

Kauli ya Kawambwa imefuatia ombi kutoka kwa Ofisa Elimu Msingi wilaya ya Bagamoyo Alex Mwakawago, aliyesema 
kuwa walimu wengi wanaofundisha elimu ya awali ni wa shule za msingi, hivyo walengwa kukosa elimu inayolingana na umri wao.

"Mheshimiwa Mbunge tukuombe ulibebe hili, ukakae na wakubwa wenzako kuona ni namna gani serikali inavyoweka mkakati maalumu, wa kuwepo walimu kwa ajili ya kufundisha madarasa ya awali, kuliko hivi sasa ambapo wanaofundisha ni wa elimu ya msingi," alisema Mwakawago.

Akizungumzia ombi hilo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa ni wazo jema ambalo linapaswa kufanyiwakazi, huku akiahidi kukutana na Waziri mwenye dhamana ya sekta hiyo, na kuwa anaimani kubwa kwamba serikali inaweza kulifanyiakazi.

Aidha Dkt. Kawambwa amewapongeza viongozi ngazi ya Kata wakiongozwa na diwani wao Usinga, kwa mikakati waliojiwekea katika elimu, kutoka nafasi ya mwisho msimu uliomalizika, na kushika nafasi za juu mwaka huu.

"Nakumbuka mwaka jana mlipokea zaeadi ya bendera nyeusi ikiashiria kufanya vibaya katika elimu, mlikaa mkatafakari wapi mlujikwaa, hatimae mwaka huu mmekuwa wa kwanza kiwilaya hongereni sana," alisema Dkt. Kawambwa.

Diwani Usinga alisema kwamva baada yaa kufanya vibaya msimu uliopita walika na kupanga mikaakati mbalimbali ikiwemo unumuzi wa mashine ya kudurufu karatasi za mithihani, hatua iliyoboresha ufauli kwenye shule zao.


SHULE KATA YA YOMBO KUFUNGWA KWA BONANZA

Diwani wa Kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo, Mohamed Usinga
.......................................................
Na Omary Mngindo, Yombo

SHULE za msingi katika Kata ya Yombo jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuanzia likizo za mwaka huu zitafungwa kwa siku moja, zoezi litakalotanguliwa na  michezo kwenye uwanja mmoja.

Diwani wa Kata ya Yombo Mohamed Usinga aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, akizungumza na walimu katani humo, mbele ya Mbunge jimbo hilo Dkt. Shukuru Kawambwa, kwenye hafla fupi ya kuwapongeza kwa kufanya vizuri.

Usinga alisema kuwa hatua ya kufungwa shule siku moja, kutaendana na ushiriki wa michezo mbalimbali, hatua itayowezesha wanafunzi na walimu kujumuika pamoja kwenye michezo, kisha kufungwa siku moja na kufunguliwa pamoja.

"Mheshimiwa Mbunge ndani ya Kata yetu kwa likizo ya mwaka huu wa 2018 tunataraji kufungwa shule siku moja, hatua itayotuwezesha kufungwa siku moja, likizo itatanguliwa na bonanza," alisema Usinga.

Akizungumza hatua hiyo ya kufungwa kwa kitanguliwa na bonanza, Mbunge Kawambwa alipongeza hatua hiyo, huku akieleza itaongeza umoja, upendo na mshikamano.

"Niwapongeze walimu kwa kupandisha ufaulu kwa msimu huu wa masomo, nimepata taarifa kwamba mwaka jana hamkufanya vizuri hatua iliyosababisha kupewa bendera nyeusi, hongereni sana," alisema Dkt. Kawambwa.

Kawambwa alisema, kwa utaratibu wa kushirikisha michezo katika siku za kufunga shule kutawahamasisha wanafunzi ambao wanapenda michezo, hivyo kuwasogeza katika masomo.

"Nikupongeze Diwani kwa hatua kubwa mliyopiga katika sekta ya elimu, kwa msimu uliopita katika elimu mlipata bendera nyeusi kutokana na kutofanya vizuri katika mitihani yenu, mkajiuliza mwaka huu mmeibuka vizuri kiwilaya na Mkoa," alimalizia Dkt. Kawambwa.