Monday, June 22, 2026

KATAMBI AWAONYA WAHALIFU NA MAANDAMANO HARAMU YA TAREHE 07

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewaasa watu wanaotoa kauli za kichochezi katika mitandao ya kijamii, majukwaa ya kisiasa na maeneo mbalimbali ambapo kauli hizo za kibaguzi na kichochezi zinahusu Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi mbalimbali wa serikali au wa dini.

 

Waziri Katambi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waumini wa Msikiti wa Mukadam uliopo Kata ya Chang’ombe iliyopo wilaya ya Dodoma Mjini ambapo kumefanyika Mashindano ya Quran na Harambee ya Ujenzi wa Msikiti huo.

 

“Taifa hili limejengwa kwa maumivu makubwa ya waasisi, limejengwa kwa jasho na hata damu ilipobidi ili Taifa Tanzania liwepo, nitumie fursa hii kuwaomba sana na kuwaasa wale wote ambao wanatumia majukwaa ya kisiasa kuchonganisha wananchi, kuwajaza chuki, kuchochea lakini pia kuhamasisha kufanya uhalifu na wanaounda magenge ya uhalifu yanayolenga kuharibu taifa letu, niwasihi na kuwaomba waache mara moja kwasababu kufanya hivyo hakuna ambae atabaki salama tutaathirika sisi Watanzania wote na athari hii italiathiri taifa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.” amesema Waziri Katambi.

 

“Tutarudi nyuma kimaendeleo,tutashindwa kuswali, tutashindwa kwenda kanisani, tutashindwa kufanya kazi za kiuchumi, tutashindwa kujenga nchi yetu, tutashindwa kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, tuwakanye na kuwaelekeza vijana wetu wakaishi mwenendo mwema na uzalendo kwa taifa lao na pale yanapotolewa maonyo na maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama wasikaidi kwani kwenda kinyume ni kuvunja sheria, katiba na taratibu.” aliongeza Waziri Katambi.







No comments:

Post a Comment