Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiongea na wakurugenzi wa
Idara na vitengo vinavyojitegemea kuhusu mikakati ya utendaji kazi kwa mwaka
2018 moja ya mkakati huo ukiwa ni kuendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa
kiwango cha kimataifa katika kikao cha kwanza cha Menejimenti
kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Mwanasheria wa Taasisi hiyo Maulid
Kikondo.
Wakurugenzi wa Idara
na vitengo vinavyojitegemea vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi (hayupo
pichani) alielezea kazi zilizofanyika katika Taasisi hiyo kwa mwaka 2017
katika kikao cha kwanza cha Menejimenti kilichofanyika hivi
karibuni. Jumla ya wagonjwa 1025 walifanyiwa upasuaji wa kufungua
kifua na bila kufungua kwa mwaka 2017 na hivyo Taasisi kuokoa zaidi ya
bilioni 29 ambazo Serikali ingezilipa kama wagonjwa hawa wangefanyiwa upasuaji
wa moyo nje ya nch
Kikao cha kwanza cha
Manejimenti cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mwaka
2018 kikiendelea.
..................................
Uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umewaahidi watanzania
kuendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa kiwango cha kimataifa kwa
wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo
Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wakurugenzi wa Idara na vitengo
vinavyojitegemea katika kikao cha kwanza cha Menejimenti kwa mwaka 2018.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho alizitaja
ahadi zingine ni pamoja na kuendeea kupunguza kupeleka wagonja nje ya nchi,
kupunguza gharama za tiba, kuongeza idadi ya huduma, kuboresha usafi katika
Hospitali na kuendelea kushirikiana na wananchi.
Mwenyekiti huyo alisema kwa mwaka 2018 wamejipanga kutoa huduma kwa
wagonjwa wengi zaidi ukilinganisha na mwaka jana ambapo jumla ya wagonjwa
64,093 walitibiwa katika Taasisi hiyo kati ya hao wagonjwa wa nje walikuwa
60796 na waliolazwa 3297.
“Malengo tuliyokuwa nayo kwa mwaka huu wa 2018 ni kuona wagonjwa wengi
zaidi ya hawa tuliowaona mwaka 2017 katika kliniki zetu za kila siku.
Taasisi
imejipanga kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 400 na bila kufungua
kifua kwa wagonjwa 1000.Tunatarajia kuwa na kambi maalum za upasuaji wa moyo
zisizozidi 15”.
“Mwezi huu tunatarajia kuwa na kambi mbili zote ni za upasuaji wa bila
kufungua kifua. Tunaanza na kambi ya watu wazima kwa kushirikiana na
Taasisi ya Madaktari Afrika ya nchini Marekani. Mwisho wa mwezi
tutakuwa na kambi ya watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa
Mtoto (Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel”, alisema.
Kwa upande wa viongozi waliohudhuria mkutano huo Prof. Janabi aliwataka
kuwasimamia wafanyakazi wanaowaongoza ili waweze kufanya kazi zao
kwa ufanisi na uweledi huku wakifuata maadili ya watumishi wa Umma hii
itawafanya wananchi waweze kupata huduma bora zaidi.
Nao viongozi waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa watahakikisha
wanafanya kazi zao kwa kujituma, kufuata kanuni za kazi na kuwasimamia
wafanyakazi wanaowaongoza ili wananchi waweze kunufaika na matibabu ya moyo
yanayotolewa katika Taasisi hiyo.
Kwa mwaka 2017 jumla ya wagonjwa 1025 walifanyiwa upasuaji wa
kufungua kifua na bila kufungua kifua katika Taasisi hiyo ambapo zaidi ya
bilioni 29 (Tshs. 29,725,000,000/=) ziliweza kuokolewa kama wagonjwa hao
wangetibiwa nje ya nchi. Gharama za mgonjwa mmoja anayetibiwa nje ya nchi
ugonjwa wa moyo ni zaidi ya milioni 29.
No comments:
Post a Comment