Sunday, January 21, 2018

UMEME WAINGIA KIJIJI CHA KONGO BAGAMOYO.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na viongozi wa kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu.
  ...............................................
Kijiji cha Kongo kata ya Yombo Halmashauri ya Bagamoyo wilayani Bagamoyo, hatimaye kimepata matumaini ya kupata umeme baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Matumaini hayo yamekuja kufuatia ahadi aliyoitoa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu katika Mkutano na wananchi wa kijiji hicho hivi karibuni ambapo aliwaahidi umeme kupatikana kijijini hapo Tarehe kumi February 2018.

Naibu waziri huyo wa Nishati, leo tarehe 21 January 2018 alitembelea kijiji cha Kongo ili kujionea kazi ya uwekaji nguzo inayofanywa na mkandarasi Sengerema ambapo alisema ameridhishwa na kasi ya uwekaji nguzo na kuwataka wananchi wa kijiji cha  Kongo kuwa na subira kwani zimebaki siku chache ili wapate umeme.

Mgalu alisema katika kutekeleza sera ya kuwahudumia wanyonge chini ya Rais Dkt. Magufuli kila kijiji kitapata umeme ili wananchi wote wapate huduma zinazotolewa na serikali kwa nchi nzima bila ya kubagua.

Aidha, amemuagiza meneja wa  TANESCO wilaya ya Bagamoyo kuandaa fomu kwaajili ya kuwapatia wananchi ili wafanye mchakato wa kulipia na kuunganishiwa umeme haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Naibu waziri, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa alisema anamshukuru Naibu waziri huyo wa Nishati kwa kushughulikia kero ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji hicho na hatimae utekelezaji umeanza.

Alisema kufuatia utekelezaji wa kuingiza umeme kijijini hapo ni wazi kuwa wananchi hao wataendelea kujenga imani na serikali yao ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.

 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu, kushoto ni Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.
 
Baadhi ya Viongozi wa Kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakimsikiliza Naibu waziri wa Nishati (hayupo pichani) akizungumza wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme.
 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akielekea kuangalia nguzo za umeme katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu, kushoto ni Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, na kulia ni Diwani wa kata ya Yombo Mohamedi Usinga.
 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Diwani wa kata ya Yombo Mohamedi Usinga pamoja na viongozi wa kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakishika moja kati ya nguzo za umeme zilizowekwa kijijini hapo kupitia mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu.

No comments:

Post a Comment