Tuesday, January 23, 2018

SUBIRA MGALU ACHANGIA UJENZI WA SHULE KIJIJI CHA KONGO BAGAMOYO.


Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati akiangalia Jengo la madarasa mawili katika shule ya msingi Kongo iliyopo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, kulia ni Diwani wa Kata ya Yombo, Mohamed Usinga na katikati ni Diwani wa viti maalum Yombo Elizabeth Shija. 
..................................

Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu amechangia bati 30 katika ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Kongo iliyopo kijiji cha Kongo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo.

Subira Mgalu ametoa ahadi hiyo ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa alipotembelea katika shule hiyo hivi karibuni.

Mbunge huyo wa viti maalum mkoa wa Pwani ambae pia ni Naibu waziri wa Nishati alitembelea shuleni hapo ili kuona kazi ya kufikisha umeme katika shule hiyo inavyoendelea.

Alisema amefurahishwa na juhudi zilizofanywa na wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo hivyo nae anaungana nao kwa kutoa bati 30 kwaajili ya kuezekea madarasa hayo.

Akizungumza na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mbunge huyo ambae ni Naibu waziri wa Nishati alimtaka mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kongo kuboresha taaluma kwa wanafunzi wake ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Alisema kufuatia kuingia umeme katika kijiji hicho ambao utafika katika shule hiyo ni wazi kuwa elimu pia itaboreshwa katika shule hiyo ukilinganisha na awali kabla ya kuwa na umeme.

Aliongeza kwa kusema kuwa kutokana na jukumu lake la ubunge wa mkoa wa Pwani kupitia viti maalum atafuatilia maendeleo ya shule hiyo ili kuona kama kutakuwa na mabadiliko ya ufaulu baada ya shule hiyo kupata umeme.

Awali Mkuu wa shule hiyo Sadiki Abasi  alimueleza  Naibu waziri huyo kuwa kumekuwa na mazingira magumu katika kutayarisha maandalio ya masomo kwa walimu wa shue hiyo hivyo ujio wa umeme utawaongezea ubora katika kufundisha.

Akizungumzia ujenzi wa madarasa mawili yanayojengwa shuleni hapo, Mwalimu mkuu huyo alisema anamshukuru Diwani wa kata ya Yombo Mohamedi Usinga kwa kutafuta wahisani na kuwashirikisha wananchi na hatimae jengo limefkia hatua ya kupauliwa.

Mpango wa ujenzi wa kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za wilaya ya Bagamoyo umeasisiwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga kwa kushirikiana na madiwani wa Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze katika kuhakikisha kila shule inaondoa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa.

Katika mpango huo Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo pamoja na madiwani wa kata zote za Bagamoyo na Chalinze  wameweza kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo na kuweza kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa huku wananchi nao wakijitolea katika kazi zilizo ndani ya uwezo wao ili kufanikisha azma hiyo

Shule ya msingi Kongo ina zaidi ya wanafunzi 700 huku ikiwa na upungufu wa vyumba vya madarasa sita ambapo jengo hilo likikamilika kutakuwa na upungufu wa vyumba vinne ili kumaliza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.
 Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati, akipata maelezo kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuhusu ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, kulia mwenye kofia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa.
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati, (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kongo Sadiki Abasi wa kwanza kulia.
 Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati, akiondoka katika shule ya Msingi Kongo, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.


No comments:

Post a Comment