Wednesday, January 10, 2018

WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA USAFIRISHWAJI WA MBOLEA.



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.  kushoto akiongea na Waziri wa Viwanda na  Biashara  (kulia).Bwana Charles Mwijage na  Waziri wa Kilimo (katikati) Dkt. Charles Tizeba pamoja na Maofisa wa JWTZ wakati alipo tembelea Kikosi cha 95KJ kinacho Safirisha Mbolea kwenda Mikoani.
 ....................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na usafirishaji wa mbolea kutoka wa wasambazaji wa pembejeo nchini kwenda kwa wakulima.

Pia ameitaka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuwa na mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakati wote nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akikagua usafirishaji wa mbolea kwenye maghala makubwa matatu jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kuona wakulima wote nchini wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea kwa wakati ili kilimo kiweze kuwaletea tija.

Amesema TFC inatakiwa ianze maandalizi ya usambazaji wa mbolea mapema kwani Serikali inataka wakulima wapate pembejeo miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba akutane na wadau na kufanya mapitio ya gharama za usafirishaji wa mbolea.

Amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha mkulima aliyeko kijijini anapata  mbolea hiyo kwa gharama nafuu bila ya kumuathiri mfanyabiashara.

Pia amemtakaDkt. Tezeba ashirikiane na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba ili kuhakikisha malori yanayobeba mbolea yanafika katika mikoa husika kwa wakati.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo awasiliane na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbawala ili malori yanayobeba mbolea yakifika kwenye vituo vya mizani yapewe kipaumbele.

“Si kwamba yaongeze uzito hapana, bali yapewe kipaumbele cha kupima haraka ili yaweze kuwahisha mbolea kwa wakulima kwani tayari msimu umeshaanza.”

Naye Waziri wa Kilimo, Dkt. Tizeba alisema watahakikisha mbolea ya kutosha inakuwepo nchini na kwamba wakulima wote wanaipata kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Maghala aliyoyakagua Waziri Mkuu ni ghala la Mohammed Enterprises lililoko Mbagala, ghala la  Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) lililoko Kurasini na ghala la Premium lililoko Vingunguti ambako kote amekuta malori yakipakia mbolea kwa ajili ya uisafirisha katika mikoa mbalimbali nchini.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 10, 2018.

 


No comments:

Post a Comment