Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na waandishi wa habari mara baada
ya kuhitimisha ziara yake katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Pangani
mapema jana tarehe 15 Desemba, 2017
......................
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaojenga
miundombinu ya usambazaji wa umeme vijijini chini ya Wakala wa
Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuongeza kasi ili
miradi yote iweze kukamilika ifikapo mwaka 2019.
Mgalu aliyasema hayo mapema jana tarehe 15 Desemba, 2017 katika
ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha Bwitini wilayani Korogwe mkoani Tanga,
lengo likiwa ni kukagua hatua ya utekelezaji wa miradi ya umeme
vijijini iliyopo chini ya REA Awamu ya Tatu na kutorishishwa na kasi ya utekelezaji
wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliambatana na watendaji kutoka
Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
Alisema kuwa, Serikali ilikwishawalipa wakandarasi wote malipo ya
awali na kuwataka kuanza kazi mara moja lakini wamekuwa wakifanya katika kasi
ndogo hususan katika hatua ya upembuzi yakinifu.
“ Wakandarasi wengi wamekuwa wakichukua muda mrefu kutekeleza miradi kwa
kisingizio cha kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi zimekwishatolewa, nichukue fursa hii kuwatangazia wakandarasi
wote nchini kuanza kazi mara moja,” alisema Mgalu
Aliendelea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayefanya kazi kwa kiwango
kisichoridhisha atanyang’anywa kazi na kupewa mkandarasi mwingine mwenye uwezo
wa kufanya kazi kulingana na kasi inayotakiwa na Serikali.
Alisema kuwa wananchi wengi kwa sasa hususan walipo katika maeneo ya
vijijini wanahitaji nishati ya umeme kwa gharama nafuu, hivyo wamechoka
na masuala ya michakato.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliwataka wakandarasi wote
nchini kununua vifaa kutoka ndani ya nchi hususan transfoma na
nguzo badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi kama ilivyoagizwa awali.
Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme
wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu
ya Tatu inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo ifikapo
mwaka 2019 karibia vijiji vote vitakuwa na umeme wa uhakika.
Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya
nishati jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na
umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme
kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wa Stieglers Gorge na
mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I na
Kinyerezi II.
Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kufufua mkoa wa Tanga
kiuchumi hivyo kuwataka wawekezaji ndani ya nchi kuwekeza kwenye viwanda
katika mkoa huo.
Alieleza kuwa kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi
la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania
katika mkoa wa Tanga, mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa hivyo Wizara ya
Nishati imejipanga katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inapatikana.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mgalu aliwataka wananchi wa Tanga
kutoharibu vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Pangani yanayotumiwa
katika uzalishaji wa umeme katika kituo cha kufua umeme cha Hale ili kutoathiri
uzalishaji wa umeme katika mkoa huo.
Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua hali za kisheria
wananchi watakaobainika wanaharibu mazingira.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa watendaji
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment