Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema
ameshangazwa na tabia ya kukatika umeme mara kwa mara katika wilaya ya Bagamoyo
hali ya kuwa Serikali imeshaweka mikakati ya kuhakikisha umeme unakuwa wa
uhakika.
Naibu waziri huyo aliyasema hayo mjini Bagamoyo
alipokuwa akifunga maonesho ya wajasiliamali katika viwanja vya shule ya msingi
Mbaruku.
Alisema Serikali imeshaweka mikakati ya
kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika nchi nzima ili kuenda sambamba na mahitaji
katika kuelekea kuwa nch ya viwanda.
Aliongeza kuwa katika mikakati iliyowekwa na
serikali iliwahusisha mameneja nchi nzima ili nao waeleze changamoto
zinazowakabili na hatimae kuzipatia ufumbuzi ili kuondokana na tatizo la
kukatika umeme mara kwa mara.
Aliongeza kwa kusema kuwa, ujenzi wa viwanda,
wajasiliamali kujikwamua kiuchumi na maendeleo kwa ujumla vyote hivyo
vinategemea upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kufikia malengo.
Alisema kutokana na mikakati hiyo anashangaa
kuona mapaka sasa bado kuna tatizo la kukatika umeme Bagamoyo jambo ambalo
lilipaswa kuisha.
Alimuagiza meneja wa TANESCO wilaya ya bagamoyo
kuhakikisha
anashughulikia changamoto zinazomkabili ili kuondoa tatizo hilo ili
kuepuka kuwapa hasara wananchi ambao wanategemea umeme katika kuzalisha na
kuhifadhi bidhaa mbalimbali.
Naibu waziri huyo alikuwa na ziara katika wilaya
ya Bagamoyo ambapo alipata nafasi ya kuongea na wananchi katika kitongoji cha
sanzale kata ya Magomeni na baadae kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo
katika Uwanja wa shule ya msingi Mbaruku.
Aidha, aliwasikiliza wananchi wa kitongoji cha
Sanzale ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme na kuwahakikishia kuwa Mradi wa
umeme vijijini awamu ya tatu utawafikia ili nao wapate huduma hiyo ya umeme.
Naibu waziri huyo ameridhishwa na hali ya ujenzi
wa nyumba za kuishi zilizojengwa katika kitongonji cha Sanzale na kuahidi
kutatua tatizo la umeme.
No comments:
Post a Comment