WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa Onyo kwa watumishi wa umma na Madiwani wa
Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na akawataka
wajirekebishe mara moja.Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Desemba 23, 2017)
wakati akizungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao
kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Songea,
mjini Songea Mkoani Ruvuma
PICHA
NA OFISI YA WAZIRI MKUU
..............................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba (CDTF) na amegiza wahusika
wote wachunguzwe ili kubaini fedha walizokusanya zimetumikaje.
Alitoa agizo hilo mwishoni mwa
wiki (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye
kikao alichokiitisha mkoani Shinyanga kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo
alikwishakuyatoa. Waziri Mkuu alishafanya vikao vitatu na wadau mbalimbali wa
zao hilo.
Alichukua uamuzi huo baada ya
kubaini kuwa watendaji wa mfuko huo hawajatekeleza majukumu ya kuundwa kwa
mfuko huo lakini pia majukumu yao yanaingiliana na yale ya Bodi ya Pamba
Tanzania (TCB).
“Kuna CDTF katika zao la pamba
lakini hakuna inachofanya ambacho kinawalenga wakulima moja kwa moja.
Tunaiondoa CDTF na kazi zake kuanzia sasa zifanywe na Bodi,” alisema.
“Waziri wa Kilimo peleka timu ya
ukaguzi kuona wamefanya nini hadi sasa. Tunataka Bodi ifanye kazi na iulizwe
maswali kuhusu zao hili. Endapo kuna jambo halijafanyika, Bodi iwe na uwezo wa
kutoa majibu si kusubiri tena mtu wa chombo kingine aje kutoa majibu,” alisema
Waziri Mkuu.
“Kwa muundo huu, Mkurugenzi wa
Bodi anakaa tu, wakati akisubiri kazi yake ifanywe na CDTF,” aliongeza.
Mfuko wa CDTF unaundwa na wajumbe
sita ambao ni wawakilishi wa wakulima wawili, wawakilishi wa wenye viwanda vya
kuchambua pamba wawili, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi wa Mazao
kutoka Wizara ya Kilimo.
Mfuko huu uliundwa mwaka 1999 na
Bodi ya Pamba (TCB) ili uwashirikishe wadau wa zao hilo kuondoa matatizo
yaliyojitokeza kwenye sekta hiyo baada ya Serikali kujitoa kwenye uendeshaji wa
moja kwa moja wa mazao nchini ikiwemo uzalishaji na biashara kutokana na mfumo
wa soko huria.
Desemba mwaka jana, Waziri wa
Kilimo, Dk Charles Tizeba alifikia uamuzi kama huo na kuamua kusimamisha
shughuli zilizokuwa zinafanywa na Mfuko wa Kuendesha Zao la Korosho Nchini
(CIDTF) ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.
Akitangaza uamuzi huo jijini Dar
es Salaam, Waziri Tizeba alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mfuko huo
kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu pamoja na kuwapo kwa malalamiko
ya muda mrefu kuhusu utendaji wa mfuko huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 24, 2017
No comments:
Post a Comment