Monday, December 25, 2017

RC PWANI ATEMBELEA KIWANDA CHA BETRI KIBAHA.


Mkuu wa Mkoa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo  jana Jumapili Tarehe 24 Desemba 2017. amekgua kazi ya ujenzi wa kiwanda cha kampuni ya China Boda Technical Group Ltd inayojenga kiwanda cha kutengeneza betri za magari katika Plot No 21 TAMCO Industrial Estate, Kibaha, Mkoa wa Pwani. 

Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani amefanya ziara hiyo ili kukagua kasi ya ujenzi na kupokea changamoto zozote wanazokabiliana nazo ili kuona namna ya kushirikiana nao katika kuzitatua ili kufikia malengo.

Katika ziara hiyo amefurahishwa na kasi ya ujenzi inavyoendelea na kusema kuwa ni ya kuridhisha.

Aidha alipata fursa ya kuwasiliana kwa simu na Kandarasi wa Ujenzi huo ambaye amemuhakikishia kwamba ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo atakuwa amekamilisha kazi ya ujenzi kama mkataba wake unvyoonesha. 

Alisema licha ya kazi nzuri inayoendelea katika kiwanda hicho bado kuna kazi kubwa ya ujenzi wa barabara kuingia kwenye kiwanda yenye upana wa meta 15 ambayo inatakiwa kujengwa na NDC kulingana na makubaliano ya Mkataba. 

Aliongeza kuwa, ili kukamilisha ujenzi Kiwanda hicho, kuna michoro ya ujenzi wa majengo mbalimbali inayotakiwa kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ili ujenzi wa miundombinu hiyo ianze mara moja.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ameahidi kushughulikia changamoto hizo mapema iwezekanavyo ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.

Kazi hiyo ya ujenzi inatakiwa ikamilike kabla ya mvua za masika zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Machi, 2018 ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kipindi cha mvua.

No comments:

Post a Comment