Mwenyekiti wa UWT wilaya ya kibaha vijijini Leila
Hamoud Jumaa watatu kushoto akisikiliza maelezo ya mtaalamu kutoka Mamlaka ya
Chakula na Dawa nchini TFDA kanda ya Mashariki, John Mosha wa pili kulia, katika
maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo yanayoendelea mjini
Bagamoyo katika Viwanja vya shule ya Msingi Mbaruku, wa kwanza ni Katiba wa UWT
Bagamoyo Mwatabu Hussein na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la
Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo Teddy Alban Davis.
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya kibaha vijijini Leila
Hamoud Jumaa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo yanayoendelea katika viwanja vya shule y Msingi Mbaruku.
..............................
Wajasiliamali wanawake Bagamoyo wametakiwa kuacha
kukata tamaa katika kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto zinazowakabili
katika kuzalisha bidhaa, utafutaji wa masoko na ukosefu wa mitaji.
Akizindua maonesho ya siku tano ya Jukwaa la
Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mjini Bagamoyo, yanayoendelea katika viwanja vya
shule ya msingi Mbaruku, Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Kibaha Vijijini, Leila
Hamoud Jumaa alisema ili kuweza kujikwamua kiuchumi ni lazima uwepo uthubutu wa
utekelezaji wa malengo wanayojiwekea wanawake na kwamba katika kujikwamua
changamoto hazikosekani.
Alisema licha ya changamoto hizo bado wanawake
wanapaswa kusonga mbele katika kujikwamua kiuchumi.
Awali akitoa taarifa ya jukwaa hilo, Mratibu wa
Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Geofrey Magogwa alisema Jukwaa la
uwezeshaji wa wanawake kiuchumi Bagamoyo linakabiliwa na changamoto kadhaa
ikiwemo kukosekana kwa ujuzi wa uhakika, kukosekana kwa mitaji, na taasisi za
kifedha kuweka masharti magumu ambayo wajasiliamali wadogo wanashindwa
kutimiza.
Kwa upande wake Charles Wambura akizungumza kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo alisema Halmashauri ya Bagamoyo
itashirikiana na vikundi vya ujasiliamali ili kuhakikisha vinapiga hatua
kimaendeleo.
Wambura alisema tayari vikundi vingi vimefaidika
na asilimia tano inayotolewa na Halmashauri kwenda kwa kinamama na kuongeza
kuwa juhudi za kuwasaidia zinafanywa na halmashauri hiyo.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo
Bagamoyo, Athumani Stili alisema wakazi wa Bagamoyo wakiwemo wanawake
wanatakiwa kutumia fursa zinazoingia Bagamoyo katika kujiongezea kipato.
Alisema ujenzi wa Bandari unaotarajiwa kuanza
mwezi Januari 2018 ni miongoni mwa fursa za kujiongezea kipato endapo
zitatumika vizuri.
Aliongeza kuwa kufuatia ujenzi huo kutakuwa na
watu watakaofanya shughuli mbalimbali hivyo kutakuwepo na mahitaji ya aina
mbalimbali ambayo waandaaji wa mahitaji hayo ni wakazi wa Bagamoyo.
Akizungumzia lengo la maonesho hayo Mwenyekit wa
Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis alisema
lengo ni kuwaonesha wanawake fursa za kiuchumi zilizopo Bagamoyo ambazo zikitumika
vizuri zinaweza kuwanyanyua wanawake wa Bagamoyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa, Maonesho yatatoa fursa
kwa wajasiliamali kufahamiana na kubadilishana mawazo juu ya namna ya kufikia
malengo hasa kwa mjasiliami wa chini.
Teddy alisema viongozi wa Jukwaa hilo waliweza
kutembelea kata zote za halmashauri ya Bagamoyo na kubaini wajasiliamali ambao
wana uwezo wa kuzalisha vitu mbalimbali vyenye ubora lakini hawana masoko na
kwamba kupitia maonesho hayo fursa mbali mbali zitapatikana.
Kwa upande wao wajasiliamali waliozungumza na
bagamoyokwanza blog walisema wajasiliamali wadogowadogo wanakabiliwa na
chnagamoto ya kupata malighafi kwaajili ya kutengenezea bidhaa mbalimbali
ambapo hulazimika kununua kwa bei ya juu hali inayopelekea kukosekana kwa faida
katika bidhaa wanazozalisha.
Adha, walisema uelewa mdogo miongoni mwa wananchi
ni sababu inayopelekea kushindwa kufikia malengo kwakuwa wananchi wengi hawana
utamaduni wa kununua bidhaa za ndani hata kama zina ubora unaokubalika.
Nae muwakilishi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini
(TFDA) kanda ya Mashariki, John Claude
Mosha alisema wajasiliamali wanapaswa kufuata taratibu za Mamlaka ya Chakula na
Dawa ili kuzifanya bidhaa wanazozalisha kuwa na viwango vinavyokubalika katika
jamii.
Alisema kutumia bidha ambazo hazijasajiliwa na
mamlaka hiyo ni kunaweza kusababisha madhara kwa watumiajai hivyo ni vyema
kumuondoa wasiwasi mtumiajai kwa kuisajili bidhaa kwenye mamlaka ya chakula na
dawa.
Maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake
Kiuchumi Bagamoyo yameanza Tarehe 20 Desemba katika viwanja vya shule msingi
Mbaruku na yanatarajiwa kufikia kilele chake siku ya Tarehe 25 Desemba 2017
ambapo wajasiliamali wanawake kutoka kata zote 11 za Halmashauri ya Bagamoyo
wanaendelea kuonesha bidhaa zao.
Kikundi cha wajasilimali ambao ni wazee
wakishangilia baada ya kukabidhiwa shilingi laki moja na mgeni rasmi
No comments:
Post a Comment