Sunday, December 30, 2018

CHAHUA WAKUMBUKA HOFU YA RIDHIWANI KIKWETE KUHUSU MAJI

Wakazi wa kitongoji cha Chahua, kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wao mara baada ya zoezi la usafi la kila mwisho wa mwezi ambapo wakazi hao walijumuika kwenye Zahanati yao kwaajili zoezi hilo, Picha na Omary Mngindo.
 ..............................................................


Na Omary Mngindo, Chahua 


MWENYEKITI wa Kitongoji cha Chahua, Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani Rashid Maisha, amekumbuka hofu iliyooneshwa na Mbunge wao Ridhiwani Kikwete, aliyeionesha wakati ikitolewa ahadi ya upatikanaji wa maji jimboni humo, ifikapo Des 31 mwaka huu.

Maisha ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, akizungumza na mwandishi wa habari hizi muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi wa mwishoni mwa mwezi, ambapo wakazi hao walijumuika kwenye jengo la Zahanati kwa ajili ya zoezi hilo.

Alisema kwamba, kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni mbele ya Makamu wa Rais Mama Samoa Suluu Hassani katika viwanja vya Polisi Bwilingu, Mtendaji Mkuu wa DAWASA lipotoa ahadi ya kupatikana kwa maji Des 31, Ridhiwani alionesha hofu ya kukamilika kwake, huku akimuomba Mtendaji huyo wafanye ziara ya kukagua namna ya utekelezwaji wa mradi unavyokwenda.

Alisema kwamba mradi huo mpaka sasa hauna matumaini ya kukamilika hivi karibu, ambapo wananchi wakiendelea kutaabika kupata huduma hiyo, huku matumaini ya kumalizika kwa adha hiyo yakigonga mwamba.

"Wakati Mbunge wetu Ridhiwani Kikwete akionesha hofu ya kukamilika kwa mradi, wengi wetu hatukumuelewa hiyo imetokana na ahadi hiyo kutolewa mbele ya Makamu wa Rais Mama Samia, lakini leo tumeamini, hofu yake imekuwa na mashiko, mradi hauna dalili za kukamilika leo wala kesho," alisema Maisha.

Kwa upande wao wakazi wakazi Mwanahamisi Lomano na Mariana Mtamani walielezea adha ya maji wanayokabiliana nayo huku wakisema kwamba mara ya mwisho kupata huduma hiyo ilikuwa mwezi wa Novemba na kuwa mpaka sasa hawana maji.

"Mpaka leo tuna mwezi mmoja hakuna maji, wananchi tunaendelea kuteseka kwa kutafuta maji kwenye malambo yasiyo safi na salama, hii kero si huku Chahua tu hata kwa wenzetu wa Chalinze pia wanakabiliwa na adha kama hii," alisema Lomano.

Mtamani aliiomba Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa huduma hiyo, ili wananchi waondokane na adha hiyo ya miaka kwa miaka.

MAJALIWA AWASILI MTWARA AKIWA NJIANI KWENDA RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara akiwa njiani kwenda Ruangwa, Desemba 30, 2018.
 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Jilly Elibariki Maleko  wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara akiwa njiani kwenda Ruangwa, Desemba 30, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bibi  Rehema Madenge.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akislimiana na viongozi wa mkoa wa Mtwara wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara akiwa njiani kwenda Ruangwa, Desemba 30, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

RAIS DKT.JOHN POMBE MAGUFULI AMJULIA HALI MAMA YAKE MZAZI BIBI. SUZANA MAGUFULI ANAYEPATIWA MATIBABU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Wasaidizi wake wakimuombea Mama yake Mzazi Bibi. Suzana Magufuli anayepatiwa Matibabu  Jijini Dar es Salaam. Desemba 30, 2018. 

Bibi Suzana Magufuli anasumbuliwa na ugonjwa wa Kiharusi ambapo amekuwa akipatiwa matibabu kwa takribani miezi mitatu sasa.

PICHA NA IKULU

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU AKAUNTI HALALI ZA MITANDAO YA KIJAMII YA INSTAGRAM NA TWITTER ZA KANGI ALPHAXARD LUGOLA, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Baada ya kuwepo kwa akaunti feki ya Mtandao wa Kijamii wa Instagram ambao ulikua unatoa taarifa mbalimbali kwa jamii kuhusu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara kwa ujumla, kuanzia leo Disemba 30, 2018, Wizara inatangaza rasmi kwa jamii, akaunti halali zilizosajiliwa kwa jina la Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola, kama ifuatavyo;
  • officialkangi_lugola (Instagram)
  • @kangi_lugola (Twitter)
Taarifa zote zitakazotolewa katika kurasa za akaunti hizi zitakua sahihi.
Kwa hatua hiyo, Wizara inaendelea kutoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayejihusisha kwa kutumia jina la Kangi Lugola kusajili akaunti yoyote na kutoa taarifa za Waziri huyo kupitia akaunti feki hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Aidha, Wizara inawaomba Watanzania waendelee kupata taarifa zake zaidi kupitia tovuti yenye anuani; www.moha.go.tz na twitter ya Wizara kwa akaunti ya Msemaji Mambo ya Ndani.

Friday, December 28, 2018

KIKOKOTOO KIPYA CHAMNG'OA MKURUGENZI SSRA

PROF. KABUDI ATEMBELEA SITE YA UJENZI WA OFISI ZA WIZARA DODOMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametembelea eneo linapojengwa jengo la Wizara yake na kuagiza timu maalum kupiga kambi eneo hilo ili kuhakikisha ujenzi unafanyika usiku na mchana huku wakizingatia viwango vya ubora katika ujenzi wa jengo hilo.

“Nataka ujenzi uharakishwe kama ambavyo Waziri Mkuu alivyogiza lakini viwango vya ubora katika ujenzi vizingatiwe” alisema Prof. Kabudi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amemtaka mkandarasi anayejenga jengo la Wizara hiyo kuhakikisha anakusanya mahitaji yote yanayotakiwa eneo la ujenzi ili kufanikisha kasi ya ujenzi inaenda kama inavyotakiwa.

Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Katiba na Sheria unatarajiwa kukamilika mapema ifikapo tarehe 15 Januari 2019.
 

WATUMISHI 13 ULANAG HATIANI KWA UBADHILIFU WA BIL. 2.9

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.

OFISI ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) imebaini matumizi mabaya ya fedha za serikali Sh. bilioni 2.98 katika halmashauri ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wakuu wa idara wote waliohusika wavuliwe nyadhifa zao huku watumishi wengine waondolewe majukumu ili vyombo vya dola viendelee na hatua kwa mujibu wa sheria dhidi yao.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais Twala za mikoa na Serikali za mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchunguzi maalum uliofanywa kwa halmashauri ya wilaya hiyo.


Jafo alisema kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imefanya uchunguzi maalum katika halmashari 12 nchini ambazo ni Ulanga, Same, Mbulu, Meru, Itigi, Misungwi, Nyang’hwale, Serengeti, Bahi, mpwapwa, Morogoro Dc na Kibaha Tc ambapo katika halamasahuri ya Ulanga uchuguzi ulianza Novemba 13 hadi 23 mwaka huu.


Alisema uchunguzi huo ulifanyika kufuatia malalamiko ya wanachi mbalimbali pamoja na mbunge wa jimbo la Ulanga Mhe. Goodluck Mlinga kutokana na ubadhirifu uliokuwepo.


Aidha alisema kiasi hicho kimebainika kupotea kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali ambapo watumishi wasio waadilifu katika halmashauri hiyo walikiuka taratibu na kufanya manunuzi hewa na kutumia vibaya fedha kinyume na malengo yaliyopangwa.


“Halmashauri hii imekuwa ikifanya udanganyifu katika taarifa za miradi ya maendeleo taarifa za mfuko wa wanawake na vijana, kwa ujumla inausimamizi mbovu wa mapato na kuwa na udhibiti hafifu wa makusanyo na matumizi ya fedha za Umma”alisema Jafo.


Jafo alisema kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ulanga, Yusufu Daud Semguruka kwa nafasi yake ya afisa masuhuli alishindwa kusiomamia sheria ya fedha za serikali za mitaa katika kudhibiti na kuweka mifumo dhabiti ya kuhakikisha fedha ziko salama kuanzia makusanyo hadi matumizi yake.


“Hii ni pamoja na kushindwa kumsimamia mweka hazina wa halmashauri katika kutekeleza majukumu yake na kwa kushindwa kutekeleza majuku hayo amesababisha hasara halmashauri ya shilingi 2,980,172,763.60″alisema Jafo.


Alifafanua kuwa Rajabu Siriwa,ambaye alikuwa ni mweka hazina wa halmasahuri hiyo alichangia kuhujumu mapato ya serikali kwa kuweka utaratibu ambao umeisababishia hasara serikali.


Alisema kuwa mweka hazina huyo aliidhinisha malipo ya sh. 225,586,400 nje ya bajeti bila idhini ya ofisi ya Rais Tamisemi ambapo malipo hayo yalihusisha posho ya safari ya mkurugenzi mtendaji Sh. 192,000,000.


“Pia kukusanya mapato na kutoyapeleka benki, katika mfumo wa LGRCIS umeonyesha halmashauri ilikusanya fedha ambazo hazikupelekwa benki kabisa shilingi 760,686,732.43 fedha hizi hazijulikani matumizi yake halisi ni nini”alihoji Jafo.


Aidha alisema kuwa mweka hazina huyo aliandaa taarifa zenye udanganyifu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotumia fedha za makusanyo ya ndani.


“Halmashauri imeripoti kupeleka shilingi 301,442,686 uhalisia wamepeleka 113,406,106.34 na udanganyifu katika mfuko wa vijana na akina mama halmashauri inaripoti kupeleka shilingi 120,000,000 uhalisia wamepeleka sh. 31,500,000 kwa mwaka 2017/18 na 2018/19 hadi novemba 2018 wakati uchunguzi unakamilika”alisema.


Aidha Jafo alisema kuwa Mhandisi David Kaijage akiwa anakaimu ofisi ya mkurugenzi februari mosi mwaka huu hadi Februari nane alihusika kwenye kuihujumu halmashauri kwa mapato ya Sh. 470,000,000 yaliyopolelewa kutoka kiwanda cha kilombero Valley Teak Company kwa kuzirejesha kwa mlipaji siku hiyohiyo waliyopokea.


“Pia alisaini hati ya malipo kumlipa bahari Phamarcy kwa siku ambayo hakuwa kaimu mkurugenzi na mkurugenzi alikuwepo”alisema.

Wakati huo huo Bw. Stanley Godwil Nyange na Bw. Isaack Mwasankope Salumu ambao wote ni wahasibu wameihujumu Halmashauri kwa kutumia akaunti zao binafsi kupokea fedha za makusanyo ya Halmashauri kiasi cha sh 203.398,700 aliongeza.

 
Waziri Jafo pia alisema kuwa uchunguzi huo pia umebainisha kuwa Isaack Mwasankope, Salehe Mbogoso pamoja na Johson Mwanyombole ambao wote ni wahasibu wa halmashauri hiyo walihusika kuchukua fedha taslim za makusanyo katika kituo cha kivukoni na kisha kuzitumia bila kuzipeleka Benki sh 168,000,000.

 
Yassin Galahenga na Mohamed Majaliwa Saidi wataalam wa mifumo (TEHAMA) walishirikiana na wahasibu kurekebisha Ankara na kufuta madeni bila idhini ya Mkurugenzi alibainisha Waziri Jafo.

 
Waziri Jafo aliongeza kuwa Bw. Willy Ndabila ambaye alikua afisa manunuzi alihusika na manunuzi hewa ya madawa yenye thamani y ash.


  73,212,909.40 pamoja na kulipa fedha zaidi yaani sh 146,425,818 huku Goodluck Mbata ambaye ni muhasibu wa hospital aliandaa malipo na kusainisha mara mbili kwa watu tofauti huku akijua kufanya hivyo ni kuandaa malipo mara mbili kwa hitaji moja (double paymet).


Waziri Jafo aliagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro kuhakikisha kuwa wakuu wa idara na vitengo waliohusika akiwemo Willy Ndabila ambaye amehamishiwa itilima,na Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa Gairo wavuliwe nyadhifa zao na mamlaka za nidhamu na vyombo vya dola viendelee na hatua kwa mujibu wa sheria.


Aliongeza kuwa watumishi wote waliohamishiwa Halmashauri ya ulanga wakiwa na makosa yaani DPMU Willy Ndabila na DT Rajabu Siriwa warejee halamashauri ya Ulanga ili kuiwezesha halmashauri na vyombo vya Dola kufanya kazi yake.

“Maelezo juu ya mkurugenzi huyu wa Ulanga yenyewe yatatolewa baadaye na serikali”alifafanua Jafo.


Hatahivyo Jafo alisema kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro ahakikishe kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imepata maelezo kwanini wataalamu hao hawakuchukuliwa hatua stahiki zenye tija dhidi ya taarifa za mkaguzi wa ndani ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha2017/18 kabla ya januari 15 mwakani.


MAGAZETI YA LEO DESEMBA 28, 2018.

Thursday, December 27, 2018

JENERALI MABEYO ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI JENERALI MABEYO ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jeneral Venance Mabeyo akipokea mkono wa Heri ya Krismasi kutoka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu, katika ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega mkoani Simiyu, iliyofanyika Desemba 26, 2018.

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu akimshuhudia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo wakati akitia saini kama shahidi katika Hati ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya, katika ibada ya kubariki na kutabaruku  kanisa hilo, iliyofanyika Desemba 26, 2018.
.................................................


Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini Jenerali Venance Mabeyo ametoa wito kwa Viongozi wa Dini nchini kuendelea kuhubiri amani ili kujenga jamii iliyo bora yenye kudumisha upendo na mshikamano.


Jenerali Mabeyo ametoa wito huo wakati wa ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwepo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Benard Kibese na viongozi wengine wa Chama na Serikali, ambapo alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo kwa Taifa lolote duniani.


“Suala la amani na utulivu ni la msingi sana katika nchi yetu, kwa vile kila mwananchi ana dini yake tunaamini kuwa viongozi wa dini zote kwa kuwa wanasikilizwa sana  na waumini  wakiweka msisitizo katika suala la amani, amani itatawala na kutakuwa na utulivu”


“Utulivu huu tunauhitaji sana ili tupate maendeleo,  kama  viongozi wetu wa kisiasa wanavyosisitiza kuwa tudumishe amani na utulivu  tupate maendeleo, bila utulivu watu wakiwa wanahaingaika hakuna maendeleo kwa sababu hakuna shughuli mtu anaweza kufanya kama hana amani na utulivu, hivyo hataweza pia kuleta maendeleo yake, familia, jamii na Taifa kwa ujumla” alisema Jenerali Mabeyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Simon Sirro amesema vitendo vingi vya uvunjifu wa amani na uhalifu ikiwemo ukataji wa mapanga na mauaji ya vikongwe na yanachangiwa na watu kukosa hofu ya Mungu; hivyo nyumba za ibada(makanisa na misikiti) zinapojengwa kwa wingi zitakuwa msaada mkubwa sana kwa watu kuwa na hofu ya Mungu.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema jamii inayoamini uwepo wa Mungu haiwezi kuwa na vitendo vya kisasi, kukatana mapanga na mauaji ya vikongwe huku akiwaasa Watanzania kukaa kwa amani na upendo bila kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha amani.


Akibariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu amewataka Watanzania kupendana na kuacha roho ya ubinafsi na visasi.


Aidha, Askofu Sangu ametoa wito kwa viongozi na waumini kufanya nyumba za ibada zibaki nyumba za sala kama yanenavyo maandiko matakatifu na kamwe zisitumike kama majukwaa la wanasiasa.


” Palipo na msamaha pana umoja, uelewano na usawa lakini palipo na  kisasi hapana maendeleo; nyumba ya ibada isitumike kama jukwaa la Wanasiasa alisisitiza Muhashamu Askofu Sangu.
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Benard Kibese, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka,Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo wakiwa katika ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayan Busega mkoani Simiyu, iliyofanyika Desemba 26, 2018.

RC NDIKILO AWAGEUKIA MAFATAKI YALIYOBEBESHA MIMBA WANAFUNZI 16 PWANI

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanawapa msukosuko na kuwakamata wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi 16 na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  ,pasipo kuwaachia wakiendelea kutamba kitaani. 


Aidha amewataka wazazi na walezi kuacha kumalizana kesi za mimba za utotoni majumbani na kurubuniwa fedha ili kuwaachia huru wanaobainika kuwapa mimba watoto wao wakike. 


Akizungumzia changamoto zinazodaiwa kusababisha kushuka kwa ufaulu, Ndikilo alitoa maelekezo hakuna kufanya masihala kwa wanaohusika kufanya vitendo hivyo,na wanatakiwa wakamatwe na kufungwa miaka 30 jela.


Alisema wanafunzi 223 ambao ni sawa na asilimia 0.74 hawakufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, kutokana na utoro 149,mimba 16 ,ugonjwa 15,vifo tisa na sababu nyingine 34.
Alitaja tatizo jingine kuwa ni utoro,mdondoko suala ambalo linachangia kushusha taaluma. 


“Tunakazi ya ziada kukabiliana na mdondoko mashuleni, tunalea watoto kuacha shule, wilayani Mkuranga mdondoko ulikuwa 67,Kibiti 36,Chalinze 36,”


“Kisarawe wanne, Bagamoyo 12,Mafia wanne, Kibaha Mjini tisa na Kibaha Vijijini wanne “alifafanua Ndikilo. 


Awali katibu tawala mkoani hapo, Theresia Mbando alieleza, idadi ya wahitimu waliosajiliwa kufanya mtihani ,walikuwa 30,010 kati yao wavulana 14,304 na wasichana  15,706 ambapo waliofanya mtihani huo ni watahiniwa 29,787 wakiwemo wavulana 14,182 na wasichana 15,605 sawa na asilimia 99.26.


Nae ofisa elimu mkoa Abdul Maulid alisema, halmashauri ya Chalinze waliopata mimba ni Tisa, Mkuranga wanne ,Bagamoyo mmoja, Kisarawe mmoja na Rufiji mmoja. 


Hata hivyo,kunaonyesha kupanda kwa ufaulu kimkoa kutoka asilimia 66.9 mwaka jana hadi asilimia 77.79 mwaka huu.