Saturday, December 8, 2018

BANDARI YA BAGAMOYO YAPAA NI BAADA YA KURASIMISHWA NA KUSIMAMIWA NA TPA

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamiii

Baada ya kurasimishwa kwa iliyokuwa bandari bubu ya Bagamoyo Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza kiasi cha makusanyanyo yake hadi kufikia bilioni 1.2 kwa mwezi huku mamlaka ya usimamizi bandari TPA ikiingiza hadi sh milioni 33 kwa siku kutoka sh 600,000.

Hayo yameelezwa jana na Msimamizi wa bandari hiyo kwa upande wa TPA, Withara Jared Withara, wakati akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo kuhusiana na hatua walizopiga baada ya kurasimishwa na mpango uliopo wa kufanya maboresho ya bandari hiyo.

Alisema mapato hayo yanatokana na usafirishaji wa bidhaa kwenda na kutoka visiwa vya Zanzibar ambao hufanywa kwa kutumia majahazi ambapo kwa siku moja huweza kuhudumia hadi majahazi nane na shehena tani 1000.

Alitaja bidhaa zinazosafirishwa sana katika bandari hiyo kuwa ni mafuta ya kula, mbao, kokoto, vilainishi vya mashine pamoja na mazao ya chakula kama vile vitunguu, nyanya, hoho n.k. “na bidhaa nyingi zinatoka Zanzibar kuja bara kuliko zile zinazoenda kule kutoka huku.”

Akielezea historia ya bandari hiyo alisema ilianzishwa toka enzi za biashara ya utumwa mwaka 1892 baada ya utumwa kukomeshwa ilikuwa ikitumika kama bandari bubu na baadae ikiwa inasimamiwa na TRA kitengo cha forodha hadi mwaka 2009 ilipochukuliwa na TPA.

Kuhusu mpango wa maboresho ya bandari hiyo alisema kuna mpango wa kujenga ukingo kuzuia mmomonyoko pamoja na kuboresha gati iliyopo ambayo ni ya mda mrefu pamoja na kununua boti ya kufanya ulinzi ili kuzuia bandari bubu zinazozunguka bandari hiyo.

“Uwepo wa bandari bubu unapunguza majahazi yanayokuja kwenye bandari yetu na hivyo kupoteza mapato na kuhatarisha usalama wa nchi na wananchi kwasababu vitu vinaingizwa kimagendo,” alisema Withara.

Mpango wa kufufua bandari bubu ambazo zipo zaidi ya 250 nchi nzima utaongeza mapato ya mamlaka kwa kiasi kikubwa sambamba na kudhibiti bidhaa za magendo nchini.

Inakadiriwa kuwa jumla ya mapato ya bandari hizo yanaweza kufikia theluthi moja au nusu ya mapato ya Bandari ya Dar es Salaam.

Bandari ya Dar es Salaam ambayo imefikia kuhudumia shehena za tani milioni 16.2 kwa mwaka inaingiza Sh  bilioni 70 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za TPA za mwaka 2017.

Zipo hatua kadhaa zinazochukuliwa katika mpango wa kufufua bandari bubu ikiwemo kuzianisha, kuwashirikisha wadau, kuzifanyia tathmini, kuandika ripoti ya kuanisha bandari zenye sifa za kuweza kufufuliwa na kisha kuipeleka kwa wizara husika kwaajili ya mapitio na kupitishwa.

Kwa sasa zoezi la kuzitambua na kuzianisha zinaendelea na kwa mujibu wa TPA  zoezi hilo linatarajia mwezi huu na kwamba likikamilika zinaweza kufikia bandari bubu zaidi ya 300.”

Tayari vikao vimeshafanyikakati ya TPA na wakuu wote wa mikoa na wilaya  ambazo zina bandari bubu na nusu ya viongozi wote wa vijiji na kata katika maeneo hayo tayari wameshashirikishwa kwenye suala hilo na vikao vinaendelea.

Ushirikishwaji huo wa wadau umefanyika ili kupata ushirikiano katika utekelezaji wa usimamizi wa bandari hizo pindi zitakaporasimishwa na kutopata mapingamizi.

Hatua hii ni miongoni mwa mabadiliko makubwa yanayofanywa na TPA katika kuhakikisha bandari zinachangia kwa kiasi kikubwq ukuaji wa uchumi wa taifa.

NYUMBA 38 ZAEZULIWA MAPAA KWA UPEPO LINDI.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Nyumba {38} yakiwemo majengo yanayomilikiwa na Serikali yamebomolewa na kuezuliwa  mapaa, kutokana na upepo mkali (Kimbunga) uliojitokeza mwanzoni mwa wiki hii, Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi,


na kusababisha hasara ambayo bado haijaweza kufaha mika mara moja.


Habari ambazo zimethibitishwa na Serikali ya Wilaya hiyo,inaeleza tukio hilo limetokea mchana wa Disemba 03 mwaka huu,Kata za Nangano na Ngunja.


Wakizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG ,baadhi ya wananchi akiwemo   Ashura Juma,Rehema Yusufu, Hemedi Ally Kindamba na Mohamedi Omari walisema upepo mkali wa Kimbunga uliovuma siku hiyo,umebomoa baadhi ya majumba pamoja na taasisi za serikali ikiwemo majengo ya shule na hata ghala la kuhifadhia mazao



Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Liwale,Sarah Chiwamba amekiri upepo wa Kimbunga hicho kuharibu Majengo ya Serikali, nyumba za wananchi, nyumba za watumishi pamoja na vyumba vya madarasa na Maabara.

Chiwamba amefafanua kwa kueleza kwamba kati ya Nyumba (38) zilizobomolewa (20) zipo kwenye ubora,zilizojengwa kwa matofari na kuezekwa kwa Bati,wakati (18) zilizosalia zimeizuliwa mapaa,kufuatia wananchi kujiwekea utamaduni wa kuezeka kwa Bati bila ya kupigilia Misumali.


‘’Hizi {18} zimejengwa kwa kutumia tope na Bati zilizoezekwa hazikupigiliwa Misumali,badala yake uziweka tu na kukandamizia vipande vya Miti’’Alisema Chiwamba.


Aidha,ameeleza Kimbunga hicho pia kimeezua paa za vyumba viwili vya Maabara Shule za Sekondari za Nangano na Ngunja, Nyumba mbili zinazotumika kuishi watumishi,Chumba cha Darasa na Choo kwa Shule ya msingi Nangano,pamoja na Ghala la kuhifadhia Mazao la Kata ya Nangano.


Aidha Chiwamba alieleza kuwa kufuatia tukio hilo,zile kaya zilizokumbwa na maafa hayo na kubainika ipo katika hali isiyo mzuri wamesaidiwa Debe moja la Mahindi kila moja na fedha kiasi cha Tsh,5,000/-.


Na kuongeza  kuwa kwa waliathirika zaidi wamepatiwa msaada wa kupatiwa Debe moja-moja la Mahindi na hela kiasi cha Tsh,5,000/-wakati uongozi wa wilaya ukiendelea na taratibu zingine za kuwasaidia wananchi hao.


Hata hivyo Chiwamba Alisema kuwa thamani ya nyumba hizo hazijafahamika. 


‘’Kuhusu kiwango cha hasara kilichopatikana naomba tuwasiliane baada ya siku mbili kupita,kwani wataalamu kwa sasa wapo huko wakitathimini kwanza’’Alisema Chiwamba.

JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LASHIRIKI SHUGHULI ZA UJENZI WA MAKAZI NA USAFI WA MAZINGIRA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya leo tarehe 08.12.2018 limeshiriki shughuli ya ujenzi na ukarabati wa nyumba za kuishi askari katika kambi ya Field Force Unit [FFU] Mbeya katika kuelekea maadhimisho ya miaka 57 ya uhuru wa Tanzania.

Ukarabati huo umefanyika katika nyumba za kuishia askari ambazo zilikuwa katika hali mbaya [chakavu] na kuzirejesha katika hali nzuri. Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limeadhimia kujenga nyumba za kuishi askari katika kambi zake zilizopo maeneo mbalimbali.

Aidha katika kuelekea maadhimisho hayo ya miaka 57 ya uhuru, licha ya kushiriki katika shughuli za ujenzi wa makazi ya askari, pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeshiriki katika shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo ya Mwanjelwa na Kabwe ikiwa ni hali ya kuhamasisha wananchi kushiriki usafi katika makazi yao na kuunga mkono jitihada za serikali za kuhamasisha usafi wa mazingira.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi  SACP. ULRICH MATEI ametumia fursa hii nawaomba wana Mbeya kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu na kudhibiti ajali za barabarani kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na za madereva wasiotaka kutii sheria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja.

Aidha amewaomba wadau wenye mapenzi mema, kuunga mkono jitihada za Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya za ujenzi na ukarabati wa nyumba za kuishi askari unaoendelea katika kambi ya FFU

RADI YAUA MTU MMOJA LINDI

Na Hadija Hassan, Lindi

Radi iliyoambatana na kiasi kichache cha Mvua iliyonyesha mwanzoni mwa wiki hii, Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi, imemuuwa mkazi mmoja wa Kijiji cha Mbuli, Kata ya Kichonda, Salima Kakole {42}.

Habari za uhakika kutoka Kijijini huko na kuthibitishwa na uongozi wa Serikali ya wilaya hiyo,imeeleza kwamba Kalole ameuwawa na Radi hiyo,Disemba 03 mwaka huu, majira ya saa 7-8 mchana.

Baadhi ya mashahidi wa tukio hilo akiwemo  Juma Selema, Kindamba Hemedi na Mwajuma Issaya,walisema kuwa siku ya tukio hill Mvua ndogondogo iliyonyesha ndipo Radi kali iliweza kujitokeza na kumfika Salima Kalole.

Walieleza kwamba wakati Mvua hiyo ikinyesha, Salima Kalole alikuwa amesimama nje ya Nyumba yake huko mashambani, akiendelea kutekeleza majukumu ya kazi zake ndogondogo.

“Mama huyu alikuwa akizifanya kazi zake ndogondogo nje ya Nyumba yake (uwanjani), hivyo Radi ilipopiga ilimfika yeye kisha kumuunguza Hali iliyopelekea   kupoteza Uhai wake Papo happy ”Walieleza Mashuhuda hao.

Mashuhuda hao alieleza  kwamba mwanamke huyo ameacha watoto watatu,wakiwemo wanawake wawili na mwanaume mmoja,mwili wake umezikwa juzi,Disemba 04 mwaka huu,saa 4:0 asubuhi.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo ya Liwale,Sarah Chiwamba,amekili kuuwawa mwanamke huyo kwa Radi iliyokuwa imeambatana na kiasi kidogo cha Mvua iliyokuwa inanyesha kwa siku hiyo.



Chiwamba pia amewaomba wananchi kujiepusha na utamaduni wa kukaa nje,ikiwemo karibu na Miti au uwanjani pale Mvua zinapoendelea kunyesha na badala yake,wawe wanajihifadhi kwenye Nyuumba zao.

TUMEANZISHA BENKI YA KILIMO ILI KUTOA MITAJI KWA WAKULIMA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.

Pia amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Desemba 7, 2018) alipotembelea shama la miwa Mkulazi na MbIgiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma.

Alisema lengo la kuanzishwa shamba la mwa la Mkulazi ni katika jitihada za Serikali za  kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.

Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee  ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.

Alisema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na Jeshi la Magereza, hivyo, aliiagiza Menejimenti mpya ya Mkulazi kuhakikisha shamba hilo linasimamiwa kikamilifu.

Waziri Mkuu pia, alimuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba hilo ili wasaidie kusimamia kitaalamu.

“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” alisema.

Kuhusu suala la maji hususan kipindi cha mvua ambayo huaribu shamba, Waziri Mkuu aliwataka watafute namna nzuri ya kuyahifadhi ili wayatumie kipindi cha kiangazi.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka watafute mashine nyingine zitakazotosha kumwagilia shamba hilo wakati wa kiangazi ili miwa isiharibike na iendelee kuwa ya kijani wakati wote.

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenistar Mhagama, alisema shamba la Mkulazi II ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomiilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na Jeshi la Magereza.

Alisema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.

Alisema wanaamini fedha zilizowekezwa kwenye mradi huo ambazo ni za wanachama zinatakiwa zirudishe faida kwa wanachama wenyewe na kujenga uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa sukari nchini linakuwa historia.

Alisema mbali ya shamba hilo la Mkulazi II pia kuna lingine la Mkulazi I ambalo ni kubwa zaidi, hivyo alishauri liendelezwe ili limalize tatizo la sukari nchini. Waziri Mkuu alimtaka ashughulikie shamba hilo kwa kuwa lipo Wizara ya Kilimo.

NYASA MATATANI FEDHA ZA UJENZI WA VITUO VYA AFYA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo(kushoto) akimkabdihi cheti cha kuhitimu na kufaulu mafunzo ya Uongozi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina Mndeme wakati wa kufunga mafunzo ya Uongozi.
....................................

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameinyooshea kidole Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa hali inayoendelea ya kusuasua kwa Ujenzi wa Vituo vya Afya.

Kutokana na hali hiyo Waziri Jafo amemuagiza Naibu Katibu Mkuu anayeshugulikia Afya Bi. Zainabu Chaula kufuatilia Halmashauri hiyo na kufahamu kwa kina sababu zilizopekea kushindwa kutekeleza ujenzi wa Vituo vya Afya kama walivyoelekezwa.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu  wa Mikoa na Makatibu Tawala yaliyofanyika kwa siku Tano katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Mhe. Jafo alisema  Fedha za Ujenzi wa Vituo zina miongozo na taratibu zake na kuna muda maalumu wa utekelezaji wa miradi hiyo sasa inakuwaje Halmashauri imekwishapata Fedha halafu hakuna utekekezaji nini kinakwamisha ilihali fedha ipo tayari kwenye akaunti ya Halmashauri husika

“Pale Nyasa kuna tatizo na nataka kufahamu kwa kina sababu zilizosababisha kukwama kwa ujenzi wa kituo cha Afya Timu ya Wataalamu iende huko mara moja ili tuweze kuchukua hatua stahili na kituo cha Afya kijengwa wananchi wapate huduma za Afya”

Aliongeza kuwa Wakuu wa Mikoa mambo haya yanatendeka katika maeneo yenu ya utawala ukiwa kama msimamizi wa shughuli zote za Serikali mnapaswa kufahamu na kuchukua hatua za stahiki na kuhakikisha malengo ya Wizara yanafikiwa.

‘Tusikubali mtu au kundi la watu likarudisha nyuma jitihada zetu za kumletea mtanzania maendeleo, Serikali imetoa fedha nyingi sana kwa ajili ya mwananchi tuzilinde fedha hizo na tusimamje miradi itekelezwe kwa kiwango’ alisema Jafo.

Awali akifunga mafunzo hayo Waziri Jafo aliwapongeza viongozi hao kwa ukomavu wa kiuongozi waliouonyesha wakati wote wa Mafunzo na kuwataka kufanyia  kazi elimu waliyoipata na  kuleta mabadiliko chanya na ya haraka katika jamii wanayoiongoza.

Aidha aliwataka kuongeza Wakuu hao wa Mikoa na Makatibu Tawala kuongeza umakini katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili thamani ya fedha iweze kuonekana.

Akitoa taarifa ya awali Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Prof. Joseph Semboja alisema kuwa viongozi hao wameonyesha kuelewa vizuri  mada zote walizofundishwa na wametoa ushirikiano wa hali ya juu wakati wakati wote wa mafunzo hayo.

Somo kubwa walilopewa viongozi wetu ni namna ya kuwa kiongozi wa kimkakati,  kusimamia rasilimali watu na kuitumia ipasavyo na namna nzuri ya kujijengea sifa binafsi alisema Pro. Semboja.

Makundi muhimu ya viongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa yamekwishapata mafunzo haya kwani  yalianza kutolewa kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote Nchini, Wakuu wa Wilaya na kwa kumalizia na Makatibu Tawala Mikoa pamoja na Wakuu wa Mikoa.

MAGAZETI YA LEO DESEMBA 08, 2018.

JIJI LA DAR KUONGOZWA NA CCM, UKAWA

UCHAGUZI wa Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam, umefanyika Desemba 07, 2018 ambapo wajumbe wa Baraza hilo wamekubaliana kwa kauli moja kuwa na Manaibu wawili kutoka Chama Cha Wananchi CUF  na mwingine  Chama Cha Chamapinduzi CCM.

Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa idadi sawa ya wajumbe kwa pande zote mbili ambapo Ukawa ulikuwa na wajumbe 12 huku CCM ikiwa na wajumbe 12.

Akizungumza wakati wakutangaza uamuzi huo ulioafikiwa   na wajumbe wa Baraza hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema kuwa kutokana na hali hiyo kila mmoja ataongoza kwa kipindi cha miezi mitatu hadi Juni 30 mwaka 2019.

Meya Mwita alieleza wajumbe wa baraza hilo kuwa, wamefikia uamuzi huo kwani viongozi wamechaguliwa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya waanchi bila kujali vyama vyao.

Alisema kuwepo kwa viongozi wa vyama viwili tofauti haita  wakosesha wananchi maendeleo kwakuwa wote wamechaguliwa kwa lengo la kuwatumikia wakazi wa jijini hapa.

 Meya Mwita alitumia nafai hiyo  kuwasihi manaibu hao walioteuliwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa ajili ya kuleta maendeleo jijini hapa kwakuweka itikadi ya vyama vyao pembeni.

“ Ndani ya ofisi hii kupata wasaidizi kutoka vyama tofauti sio dhambi, lengo langu ni kulifikisha jiji sehemu ambayo inatakiwa, ninaimani kuwa walioteuliwa leo tutasaidiana bila kujali itikadi za vyama vyetu” alisema Meya Mwita.

 Kabla ya kufanyika kwa maamuzi hayo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sita alitoa hoja baada ya kuwepo kwa mvutano mkali kuwa baraza lijigeuze kamati ili kufanya maamuzi ambayo yatakuwa na maslahi kwa wananchi kuliko kuendelea na mabishano.

“ Ndugu mwenyekiti hakuna haja ya kuendelea kubishana ,wote hapa tunafanya kazi kwa ajili ya wanachi wa jiji hili hapa, ningeshauri tujigeuze kamati ili kufikia muafa wa jambo hili.

 Baada ya hoja hiyo kutolewa, wajumbe wa baraza hilo walikubaliana kuwa kamati ambapo baada ya nusu saa, walirudi kuwa baraza na hivyo  Meya Mwita kutoa maamuzi ya uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umefanyika ikiwa ni baada ya aliyekuwa Naibu Meya Mussa Kafana kujiuzulu nafasi yake na kujiunga na CCM Septemba mwaka huu.

Friday, December 7, 2018

MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUTENGEZA JUISI YA SAYONA WILAYANI BAGAMOYO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama juisi aina ya Sayona Fruttis wakati alipotembelea kiwanda cha Sayona kilichopo eneo la Chalinmze Mboga wilayani Bagamoyo, Desemba 7, 2018. Wapili kushoto ni  Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Makapuni ya Motisun, Subash Patel na Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo,  Omari Mgumba. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kaitazama juisi aina ya Sayona Fruttis wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza juisi ya matunda cha  Sayona kilichopo eneo la Chalinze Mboga wilayani Bagamoyo, Desemba 7, 2018.    Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo na wapili kushoto ni  Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Makapuni ya Motisun, Subash Patel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha kutengeneza juisi ya matunda  cha Sayona kilichopo Chalinze Mboga wilayani Bagamoyo, Desemba 7, 2018,  Wapili kushoto ni Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Motisun, Subash Patel  na watatu kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo,  Omari Mgumba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI