Na Alodia Dominick, Bukoba
Daktari wa viungo Haruna Ayubu maarufu kama Rubai (63) mkazi wa kata ya Rwamishenyi manispaa ya Bukoba amepandishwa kizimbani kwa shitaka la ubakaji wa mtoto wa miaka 12.
Rubai amefikishwa katika mahakama ya wilaya Bukoba Oktoba 23 mwaka huu na kusomewa kesi ya jinai namba 30251/2024.
Upande wa mashtaka unaongozwa na mawakili wawili ambao ni Matilda Assey pamoja na Alice Mutungi.
Akisoma maelezo ya awali wakili upande wa mashtaka amesema kuwa, kati ya Desemba 2023 na Oktoba 19, mwaka huu mshitakiwa amekuwa akimuingiza mhanga katika moja ya chumba katika ofisi yake iliyopo mtaa wa Pwani, kata ya Miembeni manispaa ya Bukoba.
Assey ameeleza kuwa, alipoingia katika chumba hicho alimvua mhanga nguo zake za ndani kisha na mshitakiwa kuvua nguo zake na kuchukua uume wake na kuuingiza kwenye uke wa mhanga baada ya mshitakiwa kumwingilia au kumbaka mhanga amekuwa akimpatia sh. 10,000 au 5,000 kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake.
Aidha amesema, Oktoba 19, mwaka huu mhanga alikwenda tena katika ofisi ya mshitakiwa kwa lengo la kuchukua fedha ambayo amekuwa akimpatia kama msaada na baada ya mhanga kufika mshitakiwa alimpeleka katika chumba kisha kumbaka na baada ya hapo alimpatia sh.1,000 akanunue soda.
Vilevile, mhanga alipotoka katika chumba hicho ndipo alitokea askari polisi na kumuhoji mhanga ndipo mshitakiwa aliweza kukamatwa na kisha kupelekwa kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano.
Mhanga alipelekwa hospitali na daktari alithibitisha kuwa ni kweli aliingiliwa kutokana na michubuko sehemu ya uke wake akimaanisha kuwa mhanga alikuwa ameingiliwa.
Upelelezi wa shauri hilo umekamilika wapo tayari kuendelea na kesi na upande wa mashtaka wana mashahidi 10, vielelezo vya maandishi vitatu na ripoti ya daktari.
Wakili wa upande wa utetezi Frank John, ameeleza mahakama hiyo kuwa hawako tayari kuendelea na kesi jana na kudai kuwa ili mshtakiwa aweze kusikilizwa kikamilifu lazima awe amepewa maelezo ya mlalamikaji.
Wakili John, amesema pamoja na kusomewa shitaka bado mshitakiwa hajapewa hati ya mashtaka na hoja ya tatu apate muda wa kuongea na mteja wake ili aone ni jinsi gani ya kuweza kumtetea vizuri katika shtaka linalomkabili na ndiyo msingi muhimu wa haki ya kuwakilishwa na wakili.
Pia ameiomba mahakama kuahairisha shauri hilo kwa tarehe nyingine ambayo watakubaliana pande zote mbili upande wa utetezi na upande wa mashtaka kwa sababu siku moja kabla ya kesi hiyo alipata msiba wa kufiwa na kaka yake.
Akijibu hoja za wakili wa upande wa utetezi wakili wa Serikali Alice Mutungi,amesema mshitakiwa alifikishwa mahakamani tangu asubuhi hadi saa kumi jioni kama alitaka kuongea na mteja wake wangekuwa wameshaongea na kuiomba mahakama kuangalia maslahi ya mtoto ambaye ni mhanga katika shauri hilo ambaye pia amekuwepo mahakamani hapo tangu asubuhi kwa ajili ya kusikilizwa.
"Tukisema shauri hili liahirishwe mtoto aondoke na kurudi tena tunaona kwa mazingira haya sio salama kwa mtoto, tunaiomba mahakama yako tukufu kwa maslahi ya mtoto shauri hili lisikilizwe kwa haraka ili mtoto asiwe anakuja mahakamani na kurudi"amesema wakili Alice.
Amesema hati ya mashtaka amepewa wakili wa mshitakiwa na wakili hajakana amekiri kupokea hati hiyo kisheria, wakili ni muwakilishi wa mshitakiwa na yupo kwa ajili ya kumsemea.
Hakimu wa mahakama ya wilaya Endrew Kahabuka baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, upande wa wakili wa utetezi na upande wa mawakili wa mashitaka amewataka upande wa utetezi kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni wadhamini wawili wakazi wa manispaa ya Bukoba wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh.milioni nne kila mmoja na mtuhumiwa kutakiwa kutotoka ndani ya manispaa ya Bukoba labda kwa kibali maalum cha mahakama.
Vilevile upande wa utetezi wametimiza masharti hayo na mshitakiwa amedhaminiwa kesi yake itatajwa Oktoba 29, mwaka huu.
Hata hivyo, baada ya kudhaminiwa mshitakiwa amekamatwa tena akiwa amefika nyumbani kwake.
No comments:
Post a Comment