Tuesday, October 22, 2024

TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO KUZINDULIWA TAREHE 23 OKTOBA 2024

 

Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Tamasha la sanaa Bagamoyo, leo tarehe 22 Oktoba 2024. katika ukumbi wa TaSUBa mjini Bagamoyo.

.................................

Na Athumani Shomari Mkwama.

Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linatarajiwa kufunguliwa rasmi Tarehe 23 Oktoba 2024 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)


Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa TaSUBa mjini Bagamoyo, Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, amesema wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) wamejipanga kupokea wageni na kuwaburudisha kutokana na burudani za sanaa na utamaduni zitakazowasilishwa kwenye Tamasha hilo.


Amesema TaSUBa imekuwa ikifanya tamasha kama hilo kila mwaka na kwamba kila mwaka linakuwa bora zaidi kuliko mwaka uliopita na mwaka huu pia litakuwa bora zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita.


Ameongeza kwa kusema kuwa, lengo la Tamasha hilo ni kutangaza kazi za wasanii kimataifa, kukuza vipaji na kutoa fursa kwa wasanii wa ndani kuweza kufanya kazi zao nje ya nchi kutokana na wageni kutoka nchi mbalimbali wanaohudhuria katika Tamasha hilo.


Alisema Serikali imejipanga kuinua kazi za  wasanii na kuimarisha utamaduni wa Mtanzania ili asili ya furaha isiyoharibu maadili ya utamaduni wa mtanzania ibakie kama ilivyopokelewa kutoka kwa wazee waasisi wa Taifa hili lakini pia ndio malengo ya serikali katika awamu zote ikiwemo awamu hii ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Aliongeza kwa kusema kuwa wapo vijana wadogo wameanza kuonesha vipaji vyao vya sanaa na utamaduni hivyo ni wajibu wa serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuwalea vijana hao ili kutimiza ndoto zao na kukuza vipaji vyao kwa kuzingatia maadili na utamadani wa kitanzania.


Naibu waziri huyo wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametumia nafasi hiyo kuwaalika watanzania wote kuhudhuria katika Tamasha hilo litakalodumu kwa muda wa siku nne ndani ya mji wa kihistoria Bagamoyo.


Akizungumza wakati wa kumkaribisha  Naibu waziri, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema wamejipanga kuimarisha ulinzi wakati wote wa Tamasha na kuwahakikishia wageni wote watakaowasili Bagamoyo kuwa wapo katika eneo salama.


Amesema maandilizi yameenda vizuri ya kuhakikisha kila mgeni atakaewasili Bagamoyo kwaajili ya Tamasha la Sanaa na Utamaduni atapata sehemu ya kulala iliyokuwa bora na salama.


Awali akitoa Taarifa ya Tamasha hilo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye, amesema Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo,  litahusisha shughuli mbalimbali za kisanii, kiuchumi na kijamii lengo likiwa ni kuvutia wadau na watazamaji kutoka ndani na nje ya nchi.


Amesema Tamasha hilo litahusisha jumla ya vikundi 74 ambapo vikundi 61 ni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar 2, na vikundi 11 vya kimataifa kutoka nchi za Afrika ya kusini, Zambia, India, Ujerumani, Brazil, Uhispania, Botswana na visiwa vya Mayote.



Ameeleza kuwa, vikundi hivyo vitafanya maonesho ya Sanaa za jukwaani ikiwemo ngoma, za asili na za kisasa muziki wa asili na wakisasa maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho na mazingaumbwe.


Alifafanua kuwa, Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo litafunguliwa rasmi tarehe 23 Oktoba 2024 na mgeni rasmi anatarjiwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Dkt. Damas Ndumbaro na kilele chake kitakuwa tarehe 26 Oktoba 2024 ambapo mgeni rasmi wa kufunga Tamasha hilo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Tulia Ackson.








No comments:

Post a Comment