NA HADIJA OMARY, LINDI.
Jumla ya Wananchi 10,378 kutoka halmashauri sita za Mkoa wa Lindi wamefikiwa na huduma ya Afya ya macho ambapo kati yao 9690 wamefanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu
Hayo yameelezwa na Dokta Sharifu Hamza kwa niaba ya Mganga Mfawidi wa hospital ya Rufaa MKoa wa Lindi Sokoine, Jana oktoba 10 wakati wa maadhimisho ya Afya ya macho yaliyofanyika kimkoa Katika hospital hiyo ya Rufaa Sokoine huko Manispaa ya Lindi .
Zoezi hilo la utoaji Elimu ya Afya ya macho sambamba na vipimo na matibabu limeendeshwa kwa ufadhili wa mashirika ya Heart to Heart foundation, CBM pamoja na Korea church .
Amesema zoezi hilo lililoendeshwa kwa siku saba kuanzia oktoba 4 hadi 10 wataalamu walipita katika shule mbalimbali kwa halmashauri zote sita kutoa elimu pamoja na kutoa matibabu kwa wananchi walioonekana na changamoto ya afya ya macho.
maadhimisho hayo ya Afya ya macho yanayohimiza vijana na watoto kupenda macho yao na kuitaka dunia kuongeza umakini katika upatikanaji wa huduma bora za macho kwa vijana, ambapo amesema kuwa ni faraja kubwa kwa mkoa huo ambapo zoezi hilo limefanyika kwa ufanisi mkubwa
Hata hivyo Dokta Sharifu Ameeleza kuwa huduma hiyo ya macho inaendelea kutolewa Katika hospital hiyo Hata baada ya wiki hiyo ya Afya ya macho kumalizika.
Edward Aloyce Afisa mradi kutoka shirika la heart to heart foundation amesema shirika lao limekuwa likifanya mradi wa macho katika Mkoa wa Lindi wakilenga kupata watoto 20 wenye changamoto ya mtoto wa jicho ambao watanufaika kufanyiwa oparesheni Bure
"Tumesukumwa kwa sababu watoto ndio wanapata changamoto kubwa katika tatizo la macho na tumefanya kwa ushirikiano pamoja na hospitali hii ya Lindi Sokoine lakini pia tutafanya na hospitali ya taifa ya muhimbili kwa kuleta madaktari bingwa baada ya watoto hao kuweza kuainishwa kutokana na changamoto zao za magonjwa ya macho"
Aidha Aloyce alitoa wito kwa Wazazi na walezi Mkoani humo kujenga tabia ya kuwahimiza watoto kufanya uchunguzi wa changamoto ya macho katika hospitali ya sokoine ili kuweza kuwasiliana na wataalam hao wa hospitali ya muhimbili
Dokt Mwacha Machaja Ni mtaalamu wa magonjwa ya macho Hospital ya Rufaa ya Lindi Sokoine amesema zipo sababu mbalimbali zinazopelekea matatizo ya macho ambapo miongoni kwa sababu hizo ni umri, ajali, lishe duni , maambukizi na sababu za kuzaliwa,
Hata hivyo Amesema sababu kubwa inayowafanya baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Lindi wamekuwa wakipata changamoto ya macho kutokana na kukosa lishe bora hali inayopelekea kuathirika kwa macho
" wakazi wengi wa Lindi wanaopata changamoto ya macho inatokana na kutokula vyakula vinavyolinda macho uwenda kwa kujua ama kutokujua kula mboga za majani zilizoiva sana ama pengine kutokula kabisa".
Nae Asha Matola mkazi wa Lindi amesema amefika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi baada ya kuugua macho kwa muda mrefu na kwamba imani yake atapata matibabu mazuri .
No comments:
Post a Comment