Tuesday, December 5, 2023

WAHITIMU ADEM WAPEWA SOMO NA PROF. MKENDA.

 

Wahitimu katika chuo cha Wakala wa Maendeleo ya uongozi wa elimu
­(ADEM) wametakiwa kwenda kusimamia vyema taaluma ya uongozi na utawala katika maeneo yao ili kutimiza malengo ya serikali katika
maboresho ya elimu hapa nchini.

Katika Mahafali ya 31 ya waahitimu hao yaliyofanyika tarehe 01 Desemba
2023, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. Adolf Mkenda, amesema katika kipindi hiki cha mageuzi ya elimu,
serikali inawategemea sana walimu hasa waliosomea uongozi na utawala
katika kuhakikisha yale yote yanayotakiwa kuboreshwa yanasimamiwa ipasavyo.

Amesema tayari serikali inaendelea na mchakato wa maboresho ya elimu
nchini kwa kuangazia mambo saba muhimu ambayo ni sera ya elimu,
mabadiliko ya sheria ya elimu ya mwaka 1978 ambapo sasa elimu ya
lazima ni miaka 10 kwa kila Mtanzania.

Prof. Mkenda ameongeza kwa kusema kuwa, katika maboresho hayo , kuna
marekebisho ya mitaala, kuwa na walimu, wakufunzi na wahadhiri kwa
mgawanyo uliokuwa sawa, Ubora wa walimu, wakufunzi na wahadhiri,
vitendea kazi pamoja na miundombinu.

Alisisitiza kuwa ili kuweza kupata matokeo mazuri ya utekelezaji wa
maboresho hayo viongozi wa elimu wa ngazi mbalimbali wana mchango
mkubwa katika kufikia malengo hayo.

Alisema walimu ni walezi kama walivyo wazazi, mwalimu anapokuwa na mtoto shuleni anapaswa kujiona yeye ni mzazi ambae atamuangalia mtoto sio tu kwa kumfundisha bali pia ni kwa kumpa ulinzi anaostahiki ili
asidhurike kimaadili na na kimwili kwakuwa mzazi anatarajia pia
usimamizi mahiri wa mwalimu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Siston Masanja, amesema
malengo ya ADEM ni kutekeleza azma ya serikali ya kuboresha Uongozi,
Usimamizi, na Uendeshaji wa Elimu nchini katika shule za Msingi,
Sekondari Vyuo vya ualimu na kwa maafisa elimu wote, ambapo mafunzo
yanayotolewa yanawawezesha kuimarisha utendaji katika ngazi zote za elimu.

Dkt. Masanja ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa
kuendelea na maboresho ya elimu hapa nchini kwa kuhuisha sera ya elimu
na mafunzo na kusema kuwa ADEM ipo tayari kutoa mafunzo ya Uongozi,
Usimamizi na uendeshaji wa Elimu pamoja na kufanya tafiti zitakazosaidia kutoa majibu mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika elimu.

Awali wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi, wahitimu hao walisema wamejifunza namna Uongozi bora unavyoweza kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya Elimu na kuleta tija na matokeo chanya katika ukuaji wa Taifa kwa ujumla.

Waliongeza kwa kusema kuwa wamejifunza jinsi ya kutoa elimu kwa watu wazima pamoja na kutambua mazingira rafiki kwao katika kujifunza. Hali hiyo  itasaidia uendelezaji wa vituo vya Elimu ya watu wazima katika vituo
vyetu vya kazi.

Mahafali hayo yalikuwa ya whitimu wa stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu, (DEMA), Stashahada ya uthibiti ubora wa shule (DSQA) na Astashahada ya uongozi, usimamizi na utawala katika elimu (CELMA)









No comments:

Post a Comment