Saturday, October 28, 2023

ZAIDI YA BILIONI 4 KUTUMIKA UPANUZI WA BARABARA BUKOBA.

 

Na Alodia Babara


Bukoba. 


zaidi ya Shilingi bilioni 4.4 zitatumika katika upanuzi wa barabara ya lami ya njia nne yenye urefu wa kilomita moja katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.


Barabara hiyo ambayo tayari imeanza kutengenezwa itasaidia kuondoa kona kali na kupunguza mlima katika eneo la Nyangoye ambalo lilikuwa linasababisha ajali kwa wingi.


Kaimu meneja Wakala wa barabaraTanroads mkoa wa Kagera Mhandisi Ntuli Mwaikokesya akizungumza mbele ya waziri wa ujenzi Innocenti Bashungwa leo Oktoba 28, 2023 amesema, barabara hiyo inajengwa kilomita moja awamu ya kwanza kuanzia mzunguuko wa barabara ya Rwamisenyi hadi mtaa wa Mitagi.


Mhandisi Mwaikokesya amesema kuwa, mradi huo ulishaanza tangu Oktoba mosi, mwaka huu utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Oktoba mosi, mwaka 2024 na mkandarasi atakayetekeleza mradi huo ni Abemlo Contractors Ltd.


“Kwa sasa shughuli tunazofanya ni kuhamisha miundombinu ya maji, umeme na simu na wananchi  wameondoa kwa hiyari nyumba zao na mkandarasi anaendelea na shughuli za kusawazisha eneo la mradi” amesema mhandisi Mwaikokesya.


Ameongeza kuwa, barabara hiyo itajengwa awamu nne awamu ya kwanza imeanza, ya pili ni kutoka mtaa wa Mitaga hadi stend kuu ya Bukoba mita 600, ya tatu ni mita 650 ambapo mita 400 kutoka mzunguko wa barabara ya Rwamishenye kwenda Muleba na mita 250 kutoka mzunguko wa barabara ya Rwamishenyi kuelekea barabara iendayo wilaya ya Misenyi na awamu ya nne ni kutoka stend kuu hadi Bandari ya Bukoba.


Aidha Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa amesema kuwa, kipande cha mita 600 kutoka mtaa wa Mitaga hadi stend kuu ya Bukoba ambacho kitatengenezwa awamu wa pili ataenda kumuomba Rais ili serikali iongeze fedha za kipande hicho kitengenezwa kwa awamu moja ambayo tayari imeishaanza.


“Kwa jitihada nzuri za serikali katika ujenzi wa stend kuu ya Bukoba ngoja nikatoe mrejesho kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ule utamu wa barabara ya njia nne wa kilomita moja kuanzia Rwamishenyi usiishie Mitaga basi uje moja kwa moja ili awamu ya kwanza iishie stend kuu” amesema Bashungwa.


Jawil Mahamud ni mkazi wa manispaa ya Bukoba ambaye amesema kuwa, hata kama waliumia nyumba zao kubomolewa, lakini anapongeza kutengenezwa kwa barabara hiyo na kusema kuwa wanahitaji maendeleo na barabara hiyo ilishachukua maisha ya watoto na ndugu zao wengi, wanafurahi kupanuliwa kwake kwani itaepusha ajali zilizokuwa zinatokea eneo hilo.


Aresius Ntwara mkazi wa Hamugembe manispaa ya Bukoba alisema, barabara hiyo ilikuwa finyo hivyo serikali kuipanua kutoka njia mbili kwenda njia nne pamoja na kuondoa changamoto ya ajali pia itasaidia hata mji wa Bukoba kukua kimaendeleo





No comments:

Post a Comment