NA Alodia Babara, Bukoba.
Mvua kubwa iliyonyesha ikiwa imeambatana na upepo mkali katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera imesababisha kifo cha mtu mmoja huku nyumba zaidi ya 100 zikiezuliwa na upepo kutokana na mvua na upepo mkali.
Maafa hayo yametokea Oktoba 18,mwaka huu saa 11 alfajiri, na kata ambazo zimekumbwa na maafa hayo ni Kashai, Rwamishenye na Hamugembe.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema mtu mmoja ambaye amepoteza maisha hajafahamika majina yake na mwili wake ulionekana kuwa ulikuwa umesombwa na maji na ulikuwa haujatambuliwa.
"Maafa yamesababisha kifo cha mtu mmoja ambaye mwili wake ulipokutwa ulikuwa umeletwa na maji na katika paji la uso wake alikuwa na jeraha kama alipigwa na mti au kitu, jeshi la polisi linafanya uchunguzi juu ya kifo hicho" amesema Sima.
Siima amesema miongoni mwa nyumba zaidi ya 100 zilizokumbwa na maafa zimo taasisi za serikali kama shule na kituo cha afya pamoja na kanisa na nguzo za umeme na miti pia vimeathirika.
Aidha amewataka wananchi mkoani Kagera kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ili kuepukana na madhara.
Diwani wa kata ya Rwamishenyi Sued Kagasheki amesema, akiwa anajiandaa kwenda mazoezini asubuhi ametoka nje na kuona mvua kubwa inataka kuanza kunyesha alirudi ndani na muda mfupi mvua ilianza kunyesha ulipopita muda mfupi kama dakika 20 ameanza kupokea simu kutoka kwa wananchi wakimweleza juu ya majanga yaliyotokea.
Ametaja mitaa iliyoathirika kuwa ni mitatu kati ya minne ambayo ni Kamizilente, National housing na Rwamishenye.
Aidha mmoja wa mashuhuda padre Egidius Rweyemamu wa parokia Rwamishenyi kanisa katoliki amesema kuwa majira ya asubuhi akiwa kanisani anasali alishuhudia kanisa la Rwamishenyi likiezuliwa na upepo na waaumini watatu wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.
No comments:
Post a Comment