Monday, October 2, 2023

DKT MSAMBICHAKA AWAFUNDA WAZAZI MORO

 

Na Mwandishi wetu- Morogoro.


KATIBU Mkuu wa taasisi ya Tawheed Development Network ya jijini Dar es Salaam Dkt Badria Msambichaka ameitaka jamii kuwasaidia watoto kuchunga maadili wanayofundishwa shuleni hasa wakati huu wanaposubiri matokeo ya mitihani ya kumaliza darasa la saba.


Wito huo ameutoa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Morogoro wakati alipozungumza na wazazi katika hafla ya mahafali ya sita ya shule ya msingi Eastern Arc.


Mbali na hilo Dkt Msambichaka ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa juhudi kubwa wanayoichukua ya kuwafundisha watoto masomo ya sayansi, lugha na maadili katika kiwango asichokitarajia.


Aidha Dkt Msambichaka amewakumbusha wanaume jukumu lao kuu la kuisimamia familia kwenye eneo la malezi ili kupata jamii bora iliyojengeka vema kimaadili.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo iliyopata usajili wake mwaka 2017 Bwana Khalid Mfinanga amemshukuru Dkt Msambichaka kwa kuitikia ombi lao la kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo pamoja na kuwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kujitoa kwao licha ya malipo madogo wanayopata.


Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa Easten Arc Pre and Primary School bwana Idd Jengo alitaja nyezo tano ambazo zinatumika katika kujenga na kuimarisha tabia ya mtoto.


Jengo ambaye ni Afisa Mitihani Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, alitaja nyezo hizo kuwa ni Malezi, Mazingira, Teknolojia, Ujasiri na Umahiri, huku akiwataka wazazi wenzake na jamii kwa ujumla kuwa makini katika kuwajenga watoto kitabia.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya wazazi wa shule hiyo Bwana Nuru Said Mohamed alimuomba Dkt Msambichaka kuzichukua changamoto za shule hiyo kama fursa kwake ya kujijengea pepo ya Mwenyezimungu kwa kuzifanyia kazi yeye binafsi na hata kwa rafiki zake.


Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo Mwalimu Ismail Said Ahmad, katika kipindi chote cha miaka mitano tokea watoe wanafunzi wa darasa la saba, hakujawahi kufeli hata mwanafunzi mmoja.


Easten Arc Pre and Primary School ilifaulisha wanafunzi wote 12 mwaka 2018, wanafuzi wote 18 wa mwaka 2019, tulifaulisha wanafunzi wote 24 mwaka 2020, wanafunzi wote 26 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2021, wanafunzi 31 pia walifaulu wote katika mwaka 2022 na mwaka huu tunatarajia wanafunzi wote 38 watafaulu, alisema Mwalimu Ahmad. 


No comments:

Post a Comment