Sunday, October 22, 2023

WAZAZI WAACHE TABIA YA KUELEWANA NA WABAKAJI, KUMALIZA KESI.

 

Anayezungumza akiwa amesimama ni diwani wa kata ya Bakoba Shaaban Said kulia kwake ni afisa elimu kata hiyo Anitha Mashulano katika mkutano na wananchi. Picha na Alodia Babara.
.............................

Na Alodia Babara

Bukoba. 

Diwani wa kata ya Bakoba manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Rashid Said amekemea wazazi ambao watoto wao wanafanyiwa vitendo vya ulawiti na ubakaji na wazazi hao wanachukua jukumu la kuelewana na watuhumiwa wa vitendo hivyo badala ya kuwachukulia hatua za sheria.


Diwani huyo akizungumza na wananchi wa kata hiyo kupitia mkutano uliofanyika hivi karibuni katika mtaa wa Forodhani alisema kuwa juhudi wanazochukua viongozi za kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa vitendo vya ulawiti na ubakaji zinakwamishwa na baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakielewana na watuhumiwa na kuyamaliza baada ya kutenda vitendo hivyo.


Amesema kata yake inazo shule mbili za msingi na moja ya sekondari, shule ya msingi Buyekera na Bunena na shule ya sekondari Bakoba, wanafunzi watatu wamebainika kulawitiwa na watuhumiwa wameshaanza kuchukuliwa hatua za kisheria na wengine kufikishwa mahakamani.


Amesema wanafunzi hao walibainika baada ya kikao cha maendeleo ya kata kuwaagiza afisa elimu kata na polisi kata kupita katika shule hizo na kutoa elimu mashuleni kuhusu madhara ya vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto ndipo baada ya elimu hiyo walienda kutoa taarifa kwa viongozi hao.


Amesema wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao kuwapa elimu na kuwauliza maswali bila kuwaonea aibu kwani wakishindwa kufanya hivyo watajikuta wamechelewa na watoto wao wataharibikiwa.


Aidha alipowahoji wananchi kama kuna mtu anakubali ushoga hakuna mwananchi hata mmoja aliyekubaliana na hilo hivyo amewasisitiza kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuendelea kukataa vitendo vya ushoga ambavyo vimeshamili katika nchi za Magharibi.


Shaaban amesema, bahati mbaya kuna matukio yanatokea katika jamii polisi kata na afisa elimu wanafanya wajibu wao lakini ajabu mzazi anakwenda kuelewana na mtuhumiwa ambaye anatuhumiwa kumfanyia mtoto wake kitendo cha ulawiti/ubakaji inasikitisha na kuumiza na inakatisha tamaa pia inarudisha nyuma mapambano ambayo tayari viongozi wameyaanza.


"Haiwezekani tuishi na watu katika mitaa yetu wanaofanya vitendo vya namna hiyo alafu tuendelee kukubali kuishi nao, tutambue vitendo vipo tuwabaini na kuwanyoshea vidole watu wanaohusika na mkiona viongozi wanashughulika nayo wapeni ushirikiano" amesema Shaaban.


Ameongeza kuwa wenyeviti wa mitaa wasikubali watu wazoee mitaa yao kwa kuishi tu bila wao kuwafahamu walikotoka kwani watu kama hao ndiyo wanafanya vitendo hivyo kwa watoto."Msikubali kuishi na watu wasiojulikana wametoka wapi na wanashughuli gani, yawezekana ndiyo wanatuharibia watoto wetu na vijiwe vinavyoonekana ni hatarishi futeni wakileta ubabe waleteni kwangu kwenye kata hii mimi ndiyo kiongozi mkuu" amesema Shaaban.


Kwa upande wake afisa elimu kata Bakoba Anitha Mashulano ameeleza kuwa wazazi wawatolee taarifa wanaume ambao hawana wanawake kwani hao ndiyo wanahusika katika kuwaharibu watoto.


"Tuna watoto wamebakwa shuleni wameishapata ukimwi wanaendelea na dozi unajiuliza mtoto yuko darasa la nne ameanza kumeza dawa za kufubaza virus vya ukimwi hadi afike utu uzima si shida kubwa! Lakini kwa sababu ya matamanio ya mtu katoka huko anabaka tu! Anamaliza haja zake" amezungumza kwa masikitiko Mashulano.


Amewasihi wazazi kutowaficha watoto wao kuwaeleza uwazi na ukweli juu ya madhara ya vitendo vya urawiti na ubakaji na kuwaeleza kuwa eneo hili matumizi yake ni haya, wasikubali kufanya katika umri wao mdogo na wakifanya hivyo wambie madhara yake.


"Kuna mambo au mazingira watoto wanaona kama hawajapata elimu ya hayo mambo lazima wajaribu kwa hiyo wazazi elimisheni watoto wetu tuondoe aibu hata katika vikundi vyenu vya ujasiriamali elimishaneni jamani na acheni tabia ya kuacha watoto peke yao ndani eti kwa kisingizio cha kufanya biashara mnatuma fedha kwenye simu za majirani zenu watoto wanatumika sana acheni" amesema Mashulano.


Aidha ameeleza kwamba, wanapokuwa wanaandika taarifa wanaelezwa mambo mengi na watoto hadi wanajikuta wanatoa machozi, na kuwa wazazi wawe karibu na watoto wao maana wanahangaika na kupambana kwa ajili yao hivyo wasiwaache wakaharibikiwa.


Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima akizindua program ya kupinga unyanyasaji na ukatiri wa kijinsia katika taasisi ya Tanzania Youth Development Organization (Tydo) iliyopo katika manispaa hiyo alisema kuwa wale wazazi wanaoelewana na watu wanaowafanyia vitendo vya ukatiri watoto wao kwa kuwapa chochote bila kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ipo siku watoto wakiwa watu wazima na wakajua mama au baba alikaa meza moja akakubaliana na mharifu kwa kumpa chochote, mtoto huyo hataweza kuelewana na wazazi wake.


Polisi kata, katika kata ya Bakoba Rashid Mminga amewatahadharisha wazazi wenye watoto sekondariya Bakoba na wamekuwa wakiwapatia simu wanapokuwa shuleni kuwa mtoto atakayebainika mzazi atatozwa faini na mtoto wake atafukuzwa shule.

Amewata kuwa wamoja katika swala la ulinzi na usalama na wanapobaini uvunjifu wa amani katika maeneo yao kutoa taarifa na wote wanaofungua vilabu (grosaries) na kuuza pombe muda wa kazi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment