NA MWANDISHI WETU, LUSHOTO.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaambia Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa ufanisi wao na utendaji wao wa kazi utapimwa kwa jinsi watakavyokuwa wanashughulikia majalada ya mashauri Mahakamani mara baada ya kuanza kazi hiyo mpya ya Ujaji.
Mhe. Prof. Juma amesema hayo leo tarehe 02/10/2023 wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wanne wa Mahakama ya Rufani na 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayofayika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mafunzo hayo ambayo kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yatachukua wiki moja na kwa Majaji wa Mahakama Kuu wiki tatu, yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA.
“Uwezo wako katika utoaji wa huduma utapimwa kila siku utakapoingia Mahakamani, na kwa kila jalada utakalolisimamia na kila utakalofanya na kusema litapimwa…viongozi wako watakupima, wananchi na wadau watakaofika mbele yako watakupima na kutoa tathmini juu ya utendaji wako,” amesema Jaji Mkuu.
Aidha Mhe. Prof. Juma amewataka Majaji hao kuishi maisha ya kawaida na kutotumia nafasi zao kwa ajili ya manufaa binafsi na amewakumbusha kujitayarisha kutoa huduma kwa njia ya kidigitali akisema kuwa kwa sasa mhimili wa Mahakama hautarudi nyuma kwenye matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Washiriki wa mafunzo hayo watapitishwa katika mada mbalimbali ambazo zitawasilishwa na wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania, Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi.
Nae Jaji Kiongozi Mhe. Mustapher Siyani akitoa neno la shukrani amewaambia Majaji hao kuwa Mahakama na wananchi wana matarajio makubwa kwao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi na kasi kubwa mara baada ya kumaliza mafunzo yao.
“Tuna matarajio makubwa kuwa mara baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtashuka kwenye vituo mlivyopangiwa mkiwa mnakimbia kama askari mpya, mfahamu sisi sote na watanzania kwa ujumla tunawasubiri kwa hamu kubwa utendaji kazi wenu,” amesema Mhe. Jaji Siyani.
Awali akitoa neno la ukaribisho, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul F. Kihwelo amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajenga Majaji hao katika kazi yao mpya ya Ujaji na kwamba mada zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki.
“Mada za mafunzo hayo zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki na kutimiza malengo ya Mahakama na taifa kwa ujumla ,” na kuongeza,
“Mafunzo haya yatawajenga Majaji kwa ajili ya leo na kwa ajili ya Mahakama ya kesho kwenye kazi yao hiyo mpya ya Ujaji.”
Majaji hao wapya waliteuliwa na Rais wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo tarehe 03/09/2023 na kuapishwa tarehe 14/09/2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kuteuliwa na kuapishwa kwa Majaji hao wapya kunaongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kufikia 30 na wa Mahakama Kuu kuwa jumla ya 105.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wasajili wa ngazi mbalimbali za Mahakama ya Tanzania, na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma.
Aidha, mafunzo hayo elekezi ya awali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha IJA wa mwaka 2023/24-2027/28.
No comments:
Post a Comment